Kinachofanyika kabla ya dakika 30 za nyongeza

Muktasari:

  • Taifa hilo maarufu lenye ligi bora duniani liliaga Kombe la Dunia kwa kichapo cha mabao 2-1 katika mchezo ulioongezwa dakika 30 za baada ya dakika 90 za kawaida matokeo kuwa sare ya bao 1-1.

ILE timu pendwa ya mashabiki wa wengi wa soka hapa nchini, Timu ya Taifa ya England juzi Jumatano ilifungashwa virago na Croatia katika mchezo wa nusu fainali ya Kombe la Dunia kule Russia.

Taifa hilo maarufu lenye ligi bora duniani liliaga Kombe la Dunia kwa kichapo cha mabao 2-1 katika mchezo ulioongezwa dakika 30 za baada ya dakika 90 za kawaida matokeo kuwa sare ya bao 1-1.

Kucheza dakika za nyongeza katika mchezo huo ilikuwa ni jambo la kawaida kabisa kwa Timu ya Taifa ya Croatia kwani tayari ilishafanya hivyo mara tatu katika fainali hizo.

Ushindi huo, uliipa Croatia tiketi ya kucheza fainali dhidi ya Ufaransa kwa mara yakwanza hapo keshokutwa, Jumapili.

Kitendo cha Croatia kucheza muda wa nyongeza kwa mara ya tatu kunaifanya kuwa timu ya taifa ya nne duniani kufika hatua hiyo kwa mtindo wa kucheza dakika 120 kwa zaidi ya mara tatu mfululizo na kufika fainali.

Jambo hili si kazi ndogo, kwani linahitaji hamasa ya hali ya juu, kujituma, kutumia nguvu na akili nyingi, nidhamu na mbinu za kiufundi za hali ya juu.

Mtakumbuka kumaliza dakika 90 pekee ni kazi kubwa na baadhi ya wachezaji watakuwa wamechoka. Aidha umakini na uimara hupungua kwa baadhi ya wachezaji.

Tumezoea kuona kabla ya kuanza kwa dakika za nyongeza, yaani dakika 30 baada ya kipyenga cha kumaliza dakika 90 kupulizwa wachezaji hutoka nje ya uwanja na kujilaza.

Wachezaji hao huvamiwa na kundi la madaktari, walimu wa viungo, wachezaji wa akiba na wasaidizi wengine ili kuwapa huduma ya chapchap ambayo huwafanya kurudi tena uwanjani wakiwa na nguvu mpya.

Ni kawaida kuwaona wachezaji hao wakijalaza chini na huku wakipata usaidizi wa wa kunyanyuliwa mapaja yao na huku yakitikiswatikiswa, kunywa maji au kumwagiwa maji mwilini. Pia, wengine hufutwa mwilini na vipande vya barafu ambavyo vimewekwa kwenye mfuko maalumu.

Watazamaji wengi hawajui ni kwanini wachezaji hao hufanyiwa huduma kama hiyo. Leo nitawapa dondoo za huduma zinazotolewa katika kuelekea dakika za nyongeza.

Umuhimu wake

Wachezaji wanapotoka baada ya dakika 90 haraka hukabidhiwa chupa za maji ya kunywa ambayo mengine huwa ni maji maalumu yanayojulikana kitaalamu kama sports drinks.

Vinywaji hivyo huwa na maji, madini, sukari na protini pamoja na vitu vinavyoleta ladha nzuri mdomoni. Wakati mwingine hupewa maji tu ya kawaida ambayo huwa na madini mbalimbali. Wakati wa dakika 90, wachezaji hupoteza maji na madini (chumvi chumvi) mengi kwa njia ya jasho na upumuaji, hivyo huitaji maji kiasi kupunguza tatizo la upungufu wa maji mwilini.

Wengi wanakuwa na upungufu wa maji na chumvichumvi ndio maana hupewa maji mara tu wanapotoka uwanjani, lengo ni kukabiliana na upungufu huo. Endapo mchezaji atacheza dakika za nyongeza akiwa na upungufu wa maji anaweza kucheza chini ya kiwango hii ni kwa sababu upungufu wa maji mwilini unaathiri misuli ya mwili na utendaji kazi wake kwa jumla.

Madhara ya upungufu wa maji ni pamoja kukakamaa au kubanwa na misuli ya miguu, kupata uchovu, mwili kuuma, kupata majeraha kwa urahisi, kutoona vizuri, kukosa umakini na kutofanya vitendo kwa usahihi.

Vilevile humwagiwa maji mwilini au kufutwa na vipande vya barafu ili kuupoza mwili ambao joto huwa juu kutokana na misuli kufanya kazi sana.

Ikumbukwe kwa sasa kule Russia joto ni kali kwani ni majira ya kiangazi, hivyo wachezaji hupoteza maji mwilini kwa njia ya jasho.

Pia, kucheza dakika 90 huambatana na misuli ya mwili kutumia nguvu nyingi, hivyo misuli hiyo hufanya kazi kupita kiwango chake na kutawaliwa na uchovu na maumivu.

Misuli inapofanya kazi sana huchoma sukari ya mwili ili kuweza kujikunja na kukunjuka na kuleta mijongea ya mwili kama vile kutembea, kukimbia, kuruka, kukaba na kupiga mpira.

Kipindi hiki mchezaji hupoteza nguvu nyingi, hivyo hupewa maji hayo ambayo huwa na sukari ambayo hurudishia kiasi fulani cha nguvu iliyopotea. Kwa kufanya hivyo, wachezaji hurejewa na nguvu mpya za kucheza dakika za nyongeza.

Uwepo wa protini katika maji hayo huwa na lengo la kuisaidia misuli kufanya kazi kwa ufanisi. Protini ndiyo inayotumiwa na misuli kuweza kukunjuka na kujikunja ili kujongesha maungo ya mwili.

Misuli ikifanya kazi sana na protini iliyopo katika misuli hiyo hupungua, hivyo kuna faida kubwa kwa wachezaji hao kupewa kinywaji maalumu vyenye virutubisho vya protini.

Katika dakika hizo 90, wachezaji huambatana na majeraha ya misuli na kumfanya kuhisi maumivu ya mwili ambayo yanaweza kumfanya ashindwe kucheza vizuri.

Kukabiliana na tatizo hilo hasa kwa wale wachezaji waliojeruhiwa na kurudi uwanjani huweza kupewa huduma maalumu za kuyadhibiti maumivu ya misuli.

Huduma hizo ni pamoja kuwekewa barafu katika eneo lenye maumivu, kusingwa (massage), kuwekewa barafu, kupuliziwa dawa za maumivu au ganzi au kupewa dawa za kunywa za maumivu.

Mapaja yao hutikiswa kwa lengo ni kuifanya mishipa ya damu kufunguka na kupeleka damu kwa wingi na kuifanya misuli hiyo iliyofanya kazi kuondokana na mkazo au kukakamaa.

Miguu hiyo kunyanyuliwa na kutikiswa ni kusaidia damu iliyotumika na misuli (Deoxyginated blood) kurudi kirahisi mwilini na kusafishwa katika mapafu.

Vilevile mtindo huo husaidia kuondolewa kirahisi kwa taka sumu za mwilini zilizorundikana katika misuli ambazo huwa ni zao la sukari baada ya kuvunjwavunjwa. Taka hizo endapo zitarundikana katika misuli husababisha uchovu na kukakama kwa misuli na kumfanya mchezaji kushindwa kucheza kwa kiwango.

Baada ya hayo kufanyika dakika chache kabla ya kuingia uwanjani kucheza dakika za nyongeza wachezaji hukusanyika kama ilivyoonekana kwa timu zote mbili lengo ni kupeana hamasa ili kupata ari ya ushindi. Ufanyaji wa huduma kama hizo baada tu ya dakika 90 kuisha ni moja ya mambo yanayochangia timu kama Croatia kuibuka na ushindi kabla ya dakika za nyongeza kuisha au kupata ushindi kwa njia ya matuta.