MTU WA PWANI: Kichuya atacheza Zamalek ya Mwananyamala

Muktasari:

Kwa ufupi Kichuya amekuwa na bahati ndani ya kikosi cha Simba na amefanikiwa kuteka hisia na mioyo ya mashabiki

NDANI ya kipindi kifupi alichoichezea Simba baada ya kusajiliwa hapo akitokea Mtibwa Sugar mwaka 2016, Shiza Ramadhan Kichuya, amekuwa miongoni mwa wachezaji mastaa pale Msimbazi. Sidhani kama yupo anayeweza kupingana nami katika hili.

Ndiye alikuwa mfungaji wao bora msimu uliopita akiwa na mabao 12, yaani ni mawili tu pungufu ya yale yaliyofungwa na Simon Msuva na Abdulrahman Mussa waliokuwa wafungaji bora wa Ligi Kuu Bara msimu uliopita.

Ni katika msimu huohuo, Kichuya aliifunga Yanga mara mbili pindi walipokutana na Simba kwenye ligi, tena mabao yake aliyofunga kwenye mechi hizo ndiyo yale yaliyoamua matokeo.

Kichuya pia ndiye aliyeipatia Simba ubingwa wa mashindano ya Azam Sports Federation Cup baada ya kuifungia bao la ushindi katika fainali dhidi ya Mbao FC kwenye Uwanja wa Jamhuri mjini Dodoma, Mei 31 mwaka jana.

Kama haitoshi akaendeleza utemi wake dhidi ya Yanga baada ya kuifunga tena walipokutana kwenye mchezo wa kwanza wa ligi msimu huu ambao ulimalizika kwa sare ya bao 1-1, lakini pia amekuwa miongoni mwa nyota muhimu kwenye kikosi cha ‘Taifa Stars’.

Kwa ufupi Kichuya amekuwa na bahati ndani ya kikosi cha Simba na amefanikiwa kuteka hisia na mioyo ya mashabiki wa timu hiyo ambayo ni miongoni mwa timu kongwe na zenye mafanikio na heshima katika medani ya soka nchini.

Baada ya kutamba akiwa na Simba pamoja na Stars, kuliibuka tetesi mshambuliaji huyo yuko kwenye rada za klabu ya Zamalek inayoshiriki Ligi Kuu Misri. Zamalek inatajwa kuwa mbioni kumsajili Kichuya baada ya kukoshwa na kiwango chake.

Inasemekana Waarabu wa Misri wamekuwa wakifanya mawasiliano ya mara kwa mara na Simba juu ya uwezekano wa kumsajili Kichuya, lakini kinachochelewesha mpango huo ni dau kubwa la usajili ambalo vigogo wa pale Msimbazi wamewatajia Zamalek ili wafikie makubaliano.

Inaonekana hata Kichuya mwenyewe amevutiwa na mpango huo, lakini mchezaji huyo hajafurahishwa na kitendo cha uongozi wake kushindwa kukamilisha usajili huo. Inaelezwa kuwa ndio maana hadi sasa amegoma kusaini mkataba mpya wa kuendelea kuichezea Simba, jambo ambalo linamfanya awe huru kuzungumza na klabu nyingine yoyote inayomhitaji ambayo atajiunga nayo kwa uhamisho huru baada ya mkataba wake na Simba kumalizika.

Lakini wakati tukisubiria kuona majaliwa ya Kichuya kujiunga na Zamalek, ghafla mshambuliaji huyo ambaye alikuwa miongoni mwa nyota wenye nidhamu ya hali ya juu, amebadilika na sasa ameanza kufanya vitendo vya utovu wa nidhamu ambavyo vinaanza kumjengea sifa mbaya.

Katika mechi ya Kombe la FA linalodhaminiwa na Azam TV, dhidi ya Green Warriors ambapo Simba ilifungwa na kutolewa, Kichuya alionyeshwa kadi ya njano na mwamuzi, Israel Nkongo, kwa kinachosemekana alimtukana aliyekuwa Kocha wa Simba, Joseph Omog.

Ndani ya kipindi kisichozidi hata mwezi mmoja tangu alipofanya kosa hilo, jina la Kichuya tena limekamata vyombo vya habari baada ya kufanya utovu wa nidhamu kwa kususa kukaa kwenye benchi la Simba baada ya kufanyiwa mabadiliko katika mchezo dhidi ya URA kwenye Kombe la Mapinduzi. Hakuridhishwa na uamuzi huo.

Ingawa benchi la ufundi la Simba limejaribu kumtetea, kitendo cha baadhi ya viongozi kwenda kumbembeleza baada ya tukio hilo, kutovaa sare ya timu wakati ilipowasili jijini Dar es Salaam wakitokea Zanzibar pamoja na kutopanda basi la timu, vinaashiria wazi mshambuliaji huyo aligoma.

Inaonekana Kichuya anaamini amekuwa mkubwa kuliko Simba na yuko juu ya kila mmoja wakiwamo makocha na viongozi ambao wamediriki wazi kumtetea licha ya kosa hilo kubwa la kinidhamu alilolifanya ambalo lilitosha kumfanya aadhibiwe ili iwe fundisho.

Labda pengine Kichuya anaamini hana maisha marefu  Simba kutokana na ofa hiyo ya Zamalek au anaamini anaweza kusajiliwa na kucheza kwenye klabu yoyote ile ya soka kutokana na kipaji chake.

Hata hivyo, ni vyema Kichuya akafahamu kuchezea klabu inayoendeshwa kisasa kama Zamalek, hakuhitaji kuwa na kipaji pekee, bali pia nidhamu na jitihada za mchezaji husika.

Klabu kubwa na yenye mafanikio Barani Afrika kama Zamalek, haiwezi kumpa nafasi mchezaji mwenye utovu wa nidhamu na asiye na adabu kama Kichuya kwa sababu kwa kufanya hivyo, kutaharibu jina na thamani ya klabu husika. Kichuya asijiamini kipaji pekee ndicho kitamfanya acheze soka la kulipwa Misri au kokote kule duniani jambo ambalo ni ndoto ya mchezaji yeyote wa soka ulimwenguni.

Zamalek hii ya Misri haiwezi kumvumilia mtovu wa nidhamu kama Kichuya. Kwa nidhamu yake mbovu anayoionyesha, Zamalek inayomfaa ni ile ya Vingunguti Kiembembuzi au mtaani kwetu kule Boko Basihaya. Kama ni ile ya Misri, asahau kabisa.