NINACHOKIAMINI: Tunahitaji Katibu Mkuu TFF mwenye viwango 2018

Muktasari:

Kwa sababu ya kukosa mtu makini katika nafasi ya Katibu Mkuu ndio maana kwa mara ya kwanza ndani ya miaka mingi, tumeshuhudia timu ya taifa ya Tanzania Bara ‘Kilimanjaro Stars’ ikifanya vibaya katika mashindano ya Chalenji yaliyofanyika Kenya.

NI kawaida Mwaka Mpya unapoanza kwa kila mtu au taasisi kuwa na malengo au maazimio kwa ajili ya miezi 12 ijayo.

Kila mtu au taasisi huwa na malengo yake kwa ajili ya kuboresha zaidi mambo ya mwaka uliopita na kufanya yawe mazuri zaidi kwa mwaka mpya.

Nilifarijika kusikia tangazo la Rais wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), Wallace Karia, kuwa hivi karibuni watamtangaza Katibu Mkuu wa shirikisho hilo.

Licha ya mambo mengi aliyoyasema, kwangu jambo la msingi ilikuwa ni hilo la kumpata Katibu Mkuu wa TFF, kwani yeye ndiye Mtendaji Mkuu wa shughuli za kila siku.

Katika makampuni mengine huwa anaitwa Ofisa Mtendaji Mkuu (CEO) na kazi yake kuhakikisha kampuni inapata faida, huku masilahi ya wafanyakazi yakiwa mazuri bila kusahau huduma bora kwa wateja na wadau.

Tangu uongozi mpya wa Karia, kumekuwa na ombwe la nafasi ya Katibu Mkuu, ndio maana hatujaona mabadiliko makubwa kati ya uongozi wa sasa na ule uliopita.

Kwa sababu ya kukosa mtu makini katika nafasi ya Katibu Mkuu ndio maana kwa mara ya kwanza ndani ya miaka mingi, tumeshuhudia timu ya taifa ya Tanzania Bara ‘Kilimanjaro Stars’ ikifanya vibaya katika mashindano ya Chalenji yaliyofanyika Kenya.

Haiwezekani akaletwa kocha wa timu ya taifa, halafu Katibu Mkuu akasema yeye hahusiki na kuletwa kwake, huyo atakuwa hajui kazi yake.

Katibu Mkuu ni Mtendaji Mkuu, anamshauri Rais wa TFF, anaishauri Kamati ya Utendaji na kwa hoja zake nzito anaweza kwa kutumia ushawishi wake akaeleweka.

Hatuwezi katika miaka ya leo tukawa na Katibu wa TFF ambaye anadhani ana sifa kwa sababu ya elimu. Tunaposema sifa hatumaanishi elimu. Kuna sifa nyingi za kuwa Katibu Mkuu wa TFF ikiwa ni pamoja na uzoefu wa kuendesha makampuni au taasisi kubwa.

Sifa nyingine ni ushawishi, uwezo wa kujenga hoja, uwezo wa kushawishi wengine wakakuelewa, uwezo wa kukaa mbele ya Waandishi wa Habari kufanya mahojiano na vyombo vya habari.

Pia, mwenye uwezo wa kuweka mikakati ya muda mfupi na mrefu, uwezo wa kujua biashara ya soka, kuzungumza na makampuni makubwa na sifa nyingine zinazoendana na hizo.

Tunapozungumzia sifa za Katibu Mkuu hatutaki mtu aibuke ajipige kifua na kutamba anasoma Shahada ya Uzamili ya Ugavi na vikozi vingine vya siku mbili au tatu ambavyo mtu hupewa cheti cha mahudhurio.

Ili TFF ipige hatua, tunataka tuwe na Katibu Mkuu ambaye akikosolewa na vyombo vya habari anapokea ushauri na kufanyia kazi au kupuuza, hatutaki Katibu Mkuu ambaye anatishia waandishi wa habari na kujiona anajua.

Hatutaki Katibu Mkuu ambaye anaendesha shirikisho kikomandoo. Tanzania imeshuka mpaka nafasi ya 147 huku wafanyakazi wa TFF wakiwa wanadai masilahi yao kwa miezi kadhaa. Miongoni mwa kazi za Katibu Mkuu iwe ni kuhakikisha kuwa, kuna mikakati ya muda mfupi ya kuifanya Tanzania kushika nafasi ya ndani ya 100 katika viwango vya Fifa.

Wafanyakazi na maofisa wa TFF wanatakiwa kufurahia utendaji wao kazi, walipwe mishahara yao kwa muda na tena waache kutishwa na kupigwa mikwara bila sababu za msingi. Huko nyuma nilisema tunahitaji Katibu Mkuu ambaye anaweza kuchukuliwa na makampuni makubwa kama TBL, Vodacom au Tigo kuwa Ofisa Mtendaji Mkuu (CEO). Hatuhitaji Katibu Mkuu ambaye anataka nafasi hiyo pia anataka kuwa kiongozi wa Chama cha Makocha Tanzania (Tafca). Mtu anayejielewa hawezi kuwa na kofia mbili. Tunaposema sifa hatumaanishi kuwa na elimu tu. Kucheza mpira huenda sio sifa ya kuwa Katibu Mkuu. Sifa ambazo nimezitaja hapo juu zinaweza kutufanya kumpata Katibu Mkuu mwenye maono (vision) ya kuupeleka mpira wetu katika dunia ya kwanza. Wakati bado hatujaanza kupata mashaka na uongozi wa Karia, ngoja kwanza tusubiri aina ya Katibu Mkuu atakayetuletea.