Karia akichemka hapa tu, amefeli

KAZI imeanza sasa ndani ya Shirikisho la Soka Tanzania (TFF). Uongozi mpya wa shirikisho hilo chini ya Rais, Wallace Karia umeanza kupata presha kubwa.

Kauli ya Waziri wa Habari, Sanaa, Utamaduni na Michezo, Harrison Mwakyembe kutaka uchunguzi ufanyike kwenye michezo ya Ligi Daraja la Kwanza (FDL), ni ishara tosha uongozi huo sasa unatakiwa kuwajibika.

Licha ya Karia kukaa madarakani kwa miezi minne tu, wadau wa soka wametaka kuona kile ambacho uongozi wake unataka kufanya. Imeanza kuonekana kuwa baadhi ya mambo bado yanafanyika kienyeji kama ilivyokuwa kwenye uongozi uliopita.

Swali kubwa kwa sasa ni kwamba, je, Karia ataweza kuleta mabadiliko hayo yanayotazamiwa na wengi? Mwanaspoti linaangazia baadhi ya mambo ambayo yanaweza kumwangusha Karia na uongozi wake pale TFF.

Usimamizi wa FDL

Haijalishi Karia aliahidi kufanya mambo gani, lakini hili linaweza kumtia doa kubwa. Kuna madudu mengi yanaendelea katika Ligi Daraja la Kwanza (FDL) na yanatakiwa kupatiwa ufumbuzi. Yalikuwepo tangu uongozi uliopita na yapo hadi sasa. Hasa tatizo la waamuzi.

Kama mtakumbuka, timu za JKT Oljoro, Polisi Taboro, JKT Kanembwa na Geita Gold Sport ziliwahi kupata kashfa ya kupanga matokeo katika ligi hiyo na kushushwa madaraja. Inaonekana kama kuna uchafu bado unaendelea ndani ya FDL.

Kitendo cha Waziri Mwakyembe kutaka uchunguzi katika mechi za Dodoma FC dhidi ya Alliance na ile ya Biashara dhidi ya Pamba, ni ishara kuna tatizo bado katika usimamizi wa mechi au mashindano husika.

Katika hali ya kawaida, TFF ilikuwa wapi hadi ifikie hatua ya waziri kutoa tamko? Je, ni kweli TFF haikuona tatizo hilo? Ni hatua gani zilizokuwa zimeanza kuchukuliwa? Bila kujali utetezi unaotolewa na TFF, ni dhahiri usimamizi wa FDL bado siyo mzuri.

Pia, TFF inatakiwa kufahamu inawajibika kwa mpira wa nchi hii. Hata kama Bodi ya Ligi imekasimu madaraka ya uendeshaji na usimamizi, bado Katiba ya TFF inaeleza wazi Bodi itapokea maelekezo kutoka TFF.

Wakati huu ambao Bodi ya Ligi bado haijawa huru, lawama zote zinakwenda TFF ambayo ndiyo baba wa mpira wa Tanzania. Katika akili ya kawaida, familia ikikosea, anayelaumiwa ni mama au baba?

Uteuzi wa Katibu Mkuu

Hapa ndipo kwenye utata sasa. Kaimu Katibu Mkuu wa TFF, Wilfred Kidau pamoja na kuelezwa kuwa anasifa, lakini inaonekana kama hatoshi  kimsingi.

Kuna sababu kadhaa zinazotolewa kumwona Kidau hatoshi. Kwanza kabisa, ni kitendo chake cha kumtetea Kocha Ammy Ninje ambaye alikwenda kulitia taifa aibu kwenye michuano ya Kombe la Chalenji kule Kenya.

Kilimanjaro Stars ilishika mkia tena kwa kupokea vipigo vya aibu kwelikweli.

Ilishangaza sana watu waliopaswa kumwajibisha Ammy Ninje ambao ni TFF, walisimama na kumtetea kocha huyo. Ilileta ukakasi. Pili, ni uteuzi wa Ammy Ninje wenyewe ulipitishwa na nani. Kwanini Katibu Mkuu hakuishauri TFF kuwa kocha huyo hafai kupewa nafasi hiyo?

Pia, hakuna mipango mikubwa yoyote ambayo ameitoa pale TFF mpaka sasa.

Pia, amekuwa siyo mtu wa kujichanganya sana kama ambavyo watendaji wakuu wengine wa TFF walikuwa wakifanya.

Kutokana na kuonekana kutotosha katika nafasi hiyo, Karia amewekwa mtegoni kwa kutazamwa kama atamwidhinisha kuwa Katibu Mkuu moja kwa moja ama atatafuta mtu mwingine? Hakuna shaka kwamba wawili hawa ni maswahiba wakubwa, je, ataweza kumtosa rafiki yake huyo? Mtihani kwake.

Usimamizi Taifa Stars

Asikwambie mtu Taifa Stars ndio nembo ya soka la Tanzania. Hata timu za Azam, Simba na Yanga zifanye mambo gani makubwa, kama Taifa Stars inavurunda basi soka la Tanzania litaonekana kuwa chini.

Uongozi uliomaliza muda wake chini ya Jamal Malinzi haukuwapa Watanzania ile raha wanayoipenda. Katika miaka yao minne, Stars ilionekana kibonde na ilipoteza mipango kabisa. Kuna kipindi hadi basi la wachezaji wa Stars lilipopolewa mawe.

Huu sasa ni mtihani kwa Karia. Tangu ameingia Stars haijawa na lolote jipya. Kwenye viwango vya Fifa imeshuka hadi nafasi ya 146. Kwa kifupi uongozi wake unatakiwa kuinyanyua timu hiyo lakini kama makocha wenyewe ni hawa kina Ammy Ninje, kazi ipo.

Ligi ya Vijana, Wanawake

Ligi hizi mbili zilikuwa na changamoto kubwa mwaka jana. Zilionekana kama ligi ambazo hazina mvuto sana. Zilikosa msisimko mkubwa.

Msimu huu tayari Ligi ya Wanawake imeanza lakini bado haijakuwa na jipya sana. Ligi ya Vijana pia itaanza muda wowote. TFF ya Karia inatakiwa kupambana ili ligi hizi zipate mvuto, akishindwa, basi atakuwa amekalia kuti kavu.

Maandalizi Afcon

Mtihani mkubwa wa mwisho upo hapa. Tanzania itakuwa mwenyeji wa michuano ya Kombe la Mataifa ya Afrika kwa Vijana chini ya miaka 17, yatakayofanyika mwakani.

TFF ndiyo muhusika mkuu katika hili. Inatakiwa kufanya kazi karibu na serikali ili kujenga mazingira ya kuliwezesha taifa kuandaa mashindano hayo.

Mpaka sasa bado hakujawa na maandalizi makubwa na huenda wakaguzi wakija nchini baadaye mwaka huu wakakuta mambo hayajachangamka licha ya uwepo wa kamati mbalimbali.

Licha ya TFF na Serikali kuunganisha nguvu za 2019, mambo yakiparaganyika, taswira itaelekezwa TFF na itaonekana  imefeli sana.