Kama vipi, Daraja la Kwanza tulikabidhi kwa Mungu

Muktasari:

Uislamu, Ukristo na kundi kubwa la dini nyingine linaamini kuwa Mungu ndiye muweza wa yote, anaweza kufanya jambo lolote kwa wakati wowote ule hata kama binadamu kwa maarifa yake yote ameshindwa kulifanya.

NI imani ambayo imejengeka kwetu wanadamu kuwa jambo au tatizo ambalo tumeshindwa kulitatua kwa akili zetu, Mungu anaweza kulitatua.

Uislamu, Ukristo na kundi kubwa la dini nyingine linaamini kuwa Mungu ndiye muweza wa yote, anaweza kufanya jambo lolote kwa wakati wowote ule hata kama binadamu kwa maarifa yake yote ameshindwa kulifanya.

Kwa kuwa karibu watu wote tunaamini Mungu yupo, bila shaka wakati umefika kumkabidhi aisimamie Ligi Daraja la Kwanza ambayo inaonekana vyombo vilivyopewa mamlaka ya kusimamia mpira wa miguu nchini, vimeshindwa kuiendesha.

Changamoto zile zile zimekuwa zikijirudia kila kukicha katika ligi hiyo na hakuna juhudi za dhati zinazofanywa na mamlaka husika katika kuziondoa, ili kuleta ushindani wa kweli katika ligi hiyo.

Mapema kabla hata haijafika kwenye nusu ya mzunguko wa kwanza, ligi hiyo tayari imeanza kuonyesha dalili mbaya ambazo kama zisipofanyiwa kazi tunaweza kushuhudia vurugu kwenye soka letu.

Kuna mifano michache ambayo inathibitisha ni kwa namna gani ligi hiyo inaanza kuharibika mapema. Hali hii inaashiria kuwa uwezekano wa kupata timu bora zitakazopanda Ligi Kuu Bara msimu ujao haupo.

Muda mfupi baada ya kumalizika kwa mchezo baina yao na Rhino Rangers ambao waliibuka na ushindi wa bao 1-0 nyumbani, Alliance Academy ilitoa malalamiko ya kufanyiwa vurugu na mashabiki wanaosadikiwa kuwa ni wa timu mwenyeji.

Mwanzoni taarifa hizo zilichukuliwa kama ni mbinu ya Alliance kutengeneza mazingira ili Rhino Rangers ionekane ni timu yenye vurugu na korofi inapocheza kwenye uwanja wake wa nyumbani, Ali Hassan Mwinyi, uliopo mjini Tabora.

Lakini baadaye kulisambaa kipande cha video kwenye mitandao ya kijamii kikimuonyesha mmoja wa mashabiki, akimtisha Meya wa Jiji la Mwanza aliyekuwa miongoni mwa watu walioambatana na Alliance kwenda Tabora kwa ajili ya mechi hiyo.

Wakati watu wakitafakari vurugu za Tabora, kukaibuka malalamiko mengine kutoka Toto Africans ya Mwanza iliyodai kufanyiwa vitendo visivyokuwa vya kiungwana ilipokuwa ugenini kwenye mchezo wao dhidi ya Biashara FC ya Mara ambao Toto walifungwa bao 1-0.

Kwa waliobahatika kutazama mchezo wa Kundi A siku ya Jumatatu baina ya Friends Rangers na Mshikamano FC, watakuwa mashuhuda wa jinsi mwamuzi wa mechi hiyo alivyoshindwa kuumudu mchezo kiasi cha kuwanyima penati mbili za wazi Friends Rangers baada ya washambuliaji wake; Haruna Moshi na Ramadhan Chombo ‘Redondo’ kuchezewa rafu na beki pamoja kipa wa Mshikamano.

Bado tusisahau kituko cha mechi ya Mvuvumwa na African Lyon na timu imesubiriwa kwa zaidi ya dakika 30 kinyume na utaratibu wa kanuni ambao unataka timu ipewe pointi iwapo timu nyingine imechelewa kufika uwanjani kwa dakika zinazozidi 15.

Matukio kama haya yanapoanza kutokea mapema kiasi hiki, yanapoteza ladha ya mashindano na ni wazi yanazidi kuleta hisia mbaya kwa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) pamoja na Bodi ya Ligi Kuu, kuwa kuna timu zimeandaliwa kupanda kwa gharama yoyote ile. Miaka na miaka kumekuwa na malalamiko kwa mechi zinazochezwa viwanja vya ugenini kuwa timu zinazokuwa nyumbani zimekuwa zikifanya vitendo vya hujuma na fujo kwa timu pinzani. Bahati mbaya ni kwamba hakuna hatua stahiki ambazo zimekuwa zikichukuliwa na mamlaka husika.

TFF na Bodi ya Ligi wanapokaa kimya au kuchukua muda mrefu kushughulikia malalamiko yaliyopo Ligi Daraja la Kwanza, wanatengeneza roho ya visasi ambayo itakuja kuleta madhara na maafa siku za usoni na kusababisha majuto ambayo yanaweza kuepukika.

Kama inafika hatua hata kiongozi mkubwa kama Meya anatishiwa usalama wake na shabiki, vipi kwa mashabiki wa kawaida ambao wanajitokeza viwanjani kutazama mechi? Ni shabiki gani atakuwa tayari kwenda kuhatarisha usalama wake viwanjani kisa kutazama mechi ya daraja la kwanza wakati muda huo anaweza kuutumia kufanya shughuli nyingine za kipato?

Ifike wakati mamlaka zinazosimamia Ligi Daraja la Kwanza zianze kubadilika na kutimiza majukumu yao ipasavyo ili tuweze kuwa na ligi bora itakayotoa timu sahihi ambazo zitakwenda ligi kuu.

Tukilea hizi fitna, mizengwe na hujuma kwa lengo la kunufaisha timu fulani, ni wazi kuwa klabu zenye uwezo zitakosa nafasi.