Kama tulimzomea Msuva kwanini isiwe Chirwa?

Muktasari:

Kuanzia kwenye siasa, uchumi mpaka michezo. Ni mara ngapi Watanzania wanazuiwa kuingia ndani ya benki wakiwa wamevalia pensi huku wazungu wakiingia nazo? Huwa inatokea mara nyingi, nimewahi kushuhudia kwa macho yangu.

WATANZANIA tunayo kasumba ya kuvidharau vitu vyetu na kutukuza vya nje. Hili lipo kila sehemu nchini. Lipo pia kwa watu wa rika zote pia.

Kuanzia kwenye siasa, uchumi mpaka michezo. Ni mara ngapi Watanzania wanazuiwa kuingia ndani ya benki wakiwa wamevalia pensi huku wazungu wakiingia nazo? Huwa inatokea mara nyingi, nimewahi kushuhudia kwa macho yangu.

Hii ndiyo sababu mashabiki wa Yanga walikuwa wakimzomea aliyekuwa winga wao, Simon Msuva, kila wakati. Msuva alikuwa kama shetani anayependwa. Alipofunga walimshangilia, alipokosea walimzomea.

Mashabiki wengine walikwenda mbali hadi kumtukana. Kuna kipindi alipata wakati mgumu wa kucheza. Hakupewa heshima aliyostahili klabuni hapo.

Uwanjani Msuva alikuwa akifanya kazi ya maana. Msimu wa 2014/15 alifanya kazi kubwa na ya kutukuka. Alikuwa ndiye staa wa Yanga japo jina lake halikupewa nafasi kubwa sana. Alikuwa chachu ya ubingwa wa Yanga msimu huo.

Mwisho wa msimu, Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) lilimtangaza kuwa Mchezaji Bora wa Ligi Kuu Bara. Alikuwa pia ameibuka Mfungaji Bora kwa mabao yake 17. Msuva alikuwa moto.

Ajabu ni kwamba msimu uliofuata aliendelea kuzomewa na kutukanwa. Haukuwa msimu mzuri sana kwake lakini mashabiki hawakumwelewa kabisa. Msuva alizomewa kama vile hakustahili kucheza Yanga.

Bahati nzuri ni kwamba Msuva alikuwa na nidhamu ya hali ya juu. Hakuwahi kujibizana na mtu yeyote klabuni hapo. Hakuwahi kugoma wala kuonyesha vitendo vyovyote vya utovu wa nidhamu.

Mungu akampatia haki yake na sasa anacheza soka la kulipwa huko Morocco. Hazomewi tena na muda si mrefu atapiga hatua kwenda mbali zaidi.

Msuva ameondoka na kutuachia Obrey Chirwa. Jumatano aliingia uwanjani kucheza dhidi ya URA. Hakuwa fiti hata kidogo. Alikuwa ametokea kwao Zambia siku chache tu, lakini akapewa dakika kwenye mchezo huo.

Chirwa hakuwa amefanya mazoezi na timu hiyo kwa zaidi ya mwezi mzima. Inadaiwa kuwa alikuwa na mgomo baridi licha ya kwamba mwenyewe anakanusha. Kuna fedha zake anaidai Yanga hivyo moyo wa kucheza ni kama umepungua.

Matokeo yake akakosa mkwaju muhimu wa penalti ambayo iliigharimu Yanga nafasi ya kwenda fainali ya Kombe la Mapinduzi. Chirwa alipiga penalti ya hovyo. Ni kama hakuwa na uchungu na nafasi hiyo. Nani alimpa penalti? Wanajua watu wa Yanga.

Ndani ya mwaka 2017 Chirwa alikuwa amegoma mara mbili. Kuna wakati aligoma tena timu yake ikiwa na mechi muhimu dhidi ya MC Alger ya kule Algeria.

Hata hivyo Yanga wala hawamzomei. Wanamtukuza tu na kumfanya kuwa staa wao. Kuna wakati alimpiga Mpigapicha wa kampuni ya New Habari. Kwa sasa amesimamishwa pia kwa tuhuma za utovu wa nidhamu kwenye mechi dhidi ya Prisons.

Watu wa Yanga wala hawaoni Chirwa kama ni mbaya. Walimzomea Msuva aliyekuwa akifanya vizuri, lakini Chirwa huyo aliyewagharimu hadi nafasi ya kwenda fainali, wanaona ni kawaida tu.

Iko wapi heshima ya Yanga. Klabu hiyo imewahi kutumikiwa na wachezaji wengi mahiri kuliko Chirwa. Kwanini sasa anawasumbua na kushindwa kucheza hata kwa moyo?

Donald Ngoma na Amissi Tambwe ni wazuri kuliko Chirwa. Tambwe ana rekodi nzuri kuliko Chirwa. Tambwe ametwaa tuzo ya Mfungaji Bora wa Ligi Kuu mara mbili. Tangu ajiunge na Yanga hajawahi kufunga mabao chini ya 11 msimu mmoja.

Msimu wa 2015/16 alifunga mabao 21, ikiwa ni idadi kubwa zaidi ya mabao yaliyofungwa na mshambuliaji wa Yanga katika kipindi cha miaka 15 iliyopita. Nani anajali. Tambwe hakuwahi kugoma ila Chirwa anagoma.

Chirwa bado hajaukaribia uwezo wa Ben Mwalala au Boniface Ambani. Kwanini watu wa Yanga wanamtukuza?

Ambani alikuwa mfungaji bora wakati anacheza Yanga, Chirwa hajawahi. Labda kwenye Kombe la FA.

Ifike hatua tuheshimu wachezaji wetu. Kama mashabiki wa Yanga walikuwa wakimzomea Msuva kuwa anakosea, ifike wakati wamfanyie hivyo na Chirwa. Inaweza kumsaidia akabadilika.

Hata huko Ulaya tumeona wachezaji wanaozingua katika timu zao wakizomewa. Alexis Sanchez anazomewa pale Arsenal. Philipe Coutinho aliwahi kuzomewa pale Liverpool kwa kitendo chake cha kulazimisha uhamisho kwenda Barcelona.

Wachezaji wenye tabia hovyo ni lazima waonyeshwe wazi kuwa mashabiki hawakubaliani nazo. Vinginevyo tunamlea Chirwa kama yai na mwishoe ataendelea kuwa hivyo hivyo.