Kakolanya sio langoni tu, hata homu yuko fiti

Muktasari:

  • Kakolanya aliyejiunga na timu hiyo miaka miwili iliyopita akitokea Prisons ya Mbeya na msimu uliopita alikuwa na mchango mkubwa katika ubingwa wa Yanga akidaka katika mechi tano za mwisho zilizowapa taji hilo.

JUMATATU nyingine ya Mpaka Home imewadia na safari hii Mwanaspoti ilitimba pande za Mabibo, Dar es Salaam kumtembelea kipa Beno Kakolanya, anayekipiga Yanga.

Kakolanya aliyejiunga na timu hiyo miaka miwili iliyopita akitokea Prisons ya Mbeya na msimu uliopita alikuwa na mchango mkubwa katika ubingwa wa Yanga akidaka katika mechi tano za mwisho zilizowapa taji hilo.

Kwa siku za karibuni amekuwa na matatizo mengi, kwanza alipata majeraha ya muda mrefu, aliporejea akagoma akishinikiza kulipwa fedha zake za usajili na sasa amerejea na kujikuta akisugua benchi.

Pamoja na yote, Mwanaspoti limepiga stori mbili tatu na kipa huyo aliyewahi kuidakia pia Taifa Stars.

Mwanaspoti: Habari za siku nyingi Beno, umeadimika kimtindo?

Kakolanya: Nipo ndugu, sionekani tu uwanjani ila uraiani nipo.

Mwanaspoti: Wachezaji wengi hupenda kukaa sehemu ambazo wanakaa watu maarufu, imekuaje wewe unakaa huku Mabibo (uswahilini fulani hivi).

Kakolanya: Mimi ni mtu wa kawaida sana, pia hapa ni sehemu ambayo kwangu imetulia, pia ilikuwa na urahisi kwenda mazoezini kipindi Yanga inafanyia mazoezi katika uwanja wa Shule ya Loyola.

Mwanaspoti: Ukisema wewe ni mtu wa kawaida una maana gani?

Kakolanya: Sijawahi kuigiza maisha niwe juu au la, kikubwa najichanganya na watu wa hapa na muda mwingine nikichoka kukaa ndani huwa natoka nje napiga stori na vijana wenzangu ili kuweza kubadilishana nao mawazo, hawa ndio wananisaidia ikitokea nimepata matatizo.

Mwanaspoti: Inaonyesha kabisa hapa hakuna uwanja, unafanyeje mazoezi binafsi?

Kakolanya: Ni kweli unalosema, lakini nina vifaa vyangu nafanyia mazoezi hapa hapa, nyumba ina uwanja mkubwa kama unavyoona hivyo sioni tabu kujifua hapa hapa, kipa sio mbio tu ila kuna mazoezi yetu huwa tunafanya.

Mwanaspoti: Ratiba yako ya mazoezi imekaaje hasa ukiwa nyumbani?

Kakolanya: Huwa nafanya mazoezi mara moja, kama nikifanya asubuhi basi jioni napumzika.

Mwanaspoti: Chakula gani unapendelea unapokuwa nyumbani?

Kakolanya: Ninapenda sana ugali na mboga za majani, hata nikila ndizi basi ziwe na mboga za majani, hapo hunitoi.

Mwanaspoti: Beki gani ambaye akiwepo katika safu yako ya ulinzi unajisikia amani na unajua haupotezi

Kakolanya: Hahaha sikufichi, Yanga ina beki wazuri sana ndio maana hata akikosekana mmoja anayeingia anaziba pengo lake. Lakini mkongwe Kelvin Yondani anapokuwa nyuma anakuwa anawaongezea ujuzi vijana na kuwarekebisha.

Mwanaspoti: Umekosekana kwa muda mrefu katika kikosi cha Yanga, labda nini tatizo hasa kwa upande wako?

Kakolanya: Ni hali ya kawaida kwa mchezaji yeyote anayekuwa katika kikosi chenye ushindani na wachezaji wazuri, naamini wanaocheza wanafanya vizuri, nikipata nafasi nami nitafanya vizuri.

Mwanaspoti: Ulikuwa ukionekana katika kikosi cha timu ya taifa, hujaitwa kwa muda mrefu sasa hivi, pia kitu gani unakikumbuka katika timu hiyo?

Kakolanya: Katika Stars unakutana na nyota wanaocheza ndani na nje unajifunza vitu vingi, pia nakumbuka niliitwa mara ya pili na tukawa washindi wa tatu COSAFA nilijisikia amani sana.

Mwanaspoti: Ulishawahi kujutia kutua Yanga?

Kakolanya: Siwezi kujutia, nilipata nafasi nikacheza na tukawa mabingwa msimu uliopita, ninaamini ni upepo tu unapita kwangu najipanga kurudi vizuri.

Mwanaspoti: Shukrani kaka, nakutakia siku njema na mashabiki wanategemea kukuona tena uwanjani.

Kakolanya: Usijali kaka, naelewa mashabiki wananihitaji nikipata nafasi sitowaangusha.