JKU, AS Sports zimetuonyesha mfano Kagame

Muktasari:

  • Mashindano haya yaliana kwa kuzijumuisha timu 12 kutoka mataifa tisa ya ukanda huu wa Afrika Mashariki na Kati. Kwa bahati mbaya, safari hii hayakuvutia mashabiki wengi viwanjani, labda walioifuatilia luningani wakiwa majumbani au kwenye vibandaumiza, sababu kubwa ikitajwa kugongana na Kombe la Dunia.

MICHUANO ya Klabu Bingwa Afrika Mashariki na Kati, maarufu kwa jina la Kombe la Kagame, inafika tamati leo Ijumaa ambapo fainali yake inazikutanisha Simba SC na Azam FC, zote za jijini Dar es Salaam.

Mashindano haya yaliana kwa kuzijumuisha timu 12 kutoka mataifa tisa ya ukanda huu wa Afrika Mashariki na Kati. Kwa bahati mbaya, safari hii hayakuvutia mashabiki wengi viwanjani, labda walioifuatilia luningani wakiwa majumbani au kwenye vibandaumiza, sababu kubwa ikitajwa kugongana na Kombe la Dunia.

Hiyo ndio inayotajwa kuwa sababu kubwa ya kufifisha msisimko wa mashindano haya mwaka huu. Mbali ya Kombe la Dunia, inawezekana zipo sababu nyingine za kiufundi kutoka kwa Baraza la Vyama vya Soka vya Afrika Mashariki na Kati (CECAFA) lenye dhamana ya kuandaa, kuratibu na kuendesha michuano hii.

Kwa mtazamo wa haraka, kwa yeyote anayefuatilia masuala ya michezo hususani mashindano haya, anaweza kuziona pia sababu nyingine, mathalani muda mfupi uliotumika katika kufanya maamuzi ya kufanyika kwa michuano hii, hali iliyosababisha kutokuwapo kwa taarifa za kutosha za uwepo wa mashindano.

Sasa ukichanganya na Kombe la Dunia ndio kabisa kwani muda wa mechi za kule Russia umeshabihiana na ule wa mechi za Kagame, lakini pia hapa nyumbani kulikuwa na shughuli za maonyesho ya kimataifa ya biashara katika viwanja vya Sabasaba.

Kwa ujumla mahudhurio ya watazamaji yalikuwa hafifu ukilinganisha na ukubwa pamoja na thamani ya michuano yenyewe, yaani kama mambo yataendelea hivi kwa misimu ijayo, kuna hatari mashindano haya yakapoteza maana siku za usoni. Tuachane na hayo.

Kwa wale mashabiki wachache waliofanikiwa kushuhudia michuano hii kwa tuo, wamejionea wenyewe jinsi timuzilivyokuwa na dhamira ya kushindana kwa ajili ya kupigania ubingwa wa kombe hilo ambalo limekuwa mikononi mwa Azam tangu mwaka 2015.

Kwa kuziangalia timu zote unaweza kuona jinsi zilivyokuwa zimeundwa na wachezaji wengi mahiri na wenye uzoefu katika michezo mikubwa wakiwa wametoka kucheza ligi za ndani.

Hii ina maana kwamba kila timu iliyoshiriki ilikuwa na nafasi sawa na nyingine ya kuchukua ubingwa, ingawa kifalsafa ya michezo, timu zinaposhindana, mwisho wa siku lazima mmoja ndio awe bingwa.

Inafahamika kwamba timu zilizoshiriki kwenye michuano hii zimepata nafasi kutokana na nafasi zao kwenye ligi za nyumbani,ama ni bingwa, au makamu bingwa au mwalikwa. Hoja hapa ni kwamba timu zote zilikuwa kubwa.

Kwa kigezo hicho, ni rahisi mtu kufikiri hata wachezaji waliounda vikosi hivyo ni wakongwe, wakubwa na wazoefu kwa kiasi kikubwa, lakini katika hali halisi haikuwa hivyo.

Kiufundi klabu za Tanzania Bara (Simba, Azam na Singida United), Kenya (Gor Mahia), Rwanda (Rayon Sports na APR), Burundi (Lydia Ludic) na ile ya Uganda (Vipers ), zimeshiriki zikiundwa na wachezaji wazoefu na walio na majina kwenye soka la ukanda huu.

Kwa maana hiyo tulitarajia kuona mbinu na ufundi unaotokana na uzoefu wao katika kushiriki michuano mikubwa dhidi ya timu zilizobeba sura ya uchanga kama vile Kator (Sudan Kusini), AS Ports (Djibouti), Dakadaha (Somalia) na JKU (Zanzibar).

Lakini kiwango kilichooneshwa na vikosi vya JKU na AS Ports, hakika kilikuwa cha kuvutia mno. Sote tunafahanu historia ya nchi ndogo ya Djibouti iliyoko kwenye ncha ya pembe ya Mashariki mwa Afrika, maisha yake ya kijamii yalivyo, uwezo wake kisoka na kadhalika.

Kufikia sasa unapoisoma makala hii, Djibouti, ipo kwenye nafasi ya mwisho katika orodha ya viwango vya ubora wa soka ya Shirikisho la Kimataifa la Vyama vya Soka (FIFA). Lakini, jamaa hawajakata tamaa, wanaendelea kujijenga taratibu.

Katika mechi zao zote, JKU na AS Sport, zilicheza kwa kuwatumia vijana wenye maumbile madogo, lakini yenye muonekano wa kimichezo, kiufundi na waliojaa uthubutu. Walikabiliana na timu pinzani kwa ujasiri wakionesha moyo wa kujituma.

Pia wamecheza kwa nidhamu ya hali ya juu, iliyosheheni ufundi na uwezo wa kucheza kitimu zaidi bila hofu.

Kwa ujumla tumeshuhudia michezo mizuri kutoka kwa timu zote hizi mbili, ambazo kwa pamoja ingawa hazikupata nafasi ya kuongoza kwenye makundi yao, lakini zote zilifanikiwa kuingia kwenye hatua ya robo fainali (AS Sports ikaishia hapo) na JKU ikasonga mbele zaidi hadi nusu fainali na ilikoishia mikononi mwa Simba.

Kiufundi timu hizi mbili zimekuwa kielelezo kizuri kwa wadau na wapenzi wa soka kwamba mafunzo ya mchezo huu yanatakiwa kuanzia kwenye umri mdogo na yawe endelevu. Ni kwa sababu wachezaji wa timu hizi mbili walikuwa na kiwango kizuri cha kumiliki mpira, uelewa wa mchezo kulingana na ulivyokuwa unakwenda pamoja na ufahamu wa stadi mbalimbali za kiufundi.

Tatizo pekee lililokuwa linawasumbua ni matumizi ya nguvu pale walipotakiwa kutumia nguvu.

Kwa ujumla mchezo wa mpira wa miguu unahitaji zaidi maarifa mengi na hii imeonekan pasipo na mashaka yoyote,hivyo tulio wengi wapenzi na mashabiki wa soka tumezidi kutafakari na kufikiria kwamba dhana ya kuibua vipaji, kuvikuza na kuviendeleza kwa kufundisha watoto wadogo misingi ya soka, ni dhana muhimu sana.

Iwapo Djibouti wataendelea kuweka mipango madhubuti na ya muda mrefu, sina shaka kuna siku watakuwa tishio katika eneo hili la nchi za Afrika Mashariki na Kati, hii ni kwa namna walivyocheza mashindano haya.

Kwa JKU wao tayari wanayo mipango mizuri na endelevu kupitia programu zao za Juvenile, ambazo kwa kipindi kirefu zimekuwa chachu ya mpira mzuri unaochezwa na timu nyingi za Zanzibar.