JICHO LA MWEWE: Akina Okwi 10, kuna sura nyingi tu ndani

Emmanuel Okwi

Muktasari:

  • Kocha alikuwa Mtaliano Gianluca Vialli.
  • Miaka mitano baadaye, Arsene Wenger, alijibu mapigo. Arsenal ilikuwa timu ya kwanza katika historia ya Ligi Kuu England kupanga kikosi kizima cha wachezaji wageni wakiwemo wale waliokalia benchi katika pambano dhidi ya Crystal Palace.

DESEMBA 26, 1999 siku moja baada ya Sikukuu ya Mwisho ya Krismasi kwa karne iliyopita, Chelsea ikicheza ugenini mbele ya Southampton iliweka historia ya kuwa timu ya kwanza ya England, kuanzisha kikosi cha kwanza cha wachezaji wa kigeni tupu. Kocha alikuwa Mtaliano Gianluca Vialli.

Miaka mitano baadaye, Arsene Wenger, alijibu mapigo. Arsenal ilikuwa timu ya kwanza katika historia ya Ligi Kuu England kupanga kikosi kizima cha wachezaji wageni wakiwemo wale waliokalia benchi katika pambano dhidi ya Crystal Palace.

Ilikuwa Jumatatu usiku Februari 14, 2005. Siku ya Wapendanao. Patamu hapo.

Miaka minne baadaye ikawa zamu ya Sir Alex Ferguson. Pamoja na Uingereza wake wote, aliingia katika historia ya kuwa kocha wa tatu kuchezesha wachezaji wote wa kigeni ndani ya uwanja. Ilikuwa ni Mei 12, 2009.

Nasi tumeanza kuwafuata Waingereza katika staili hii. Wiki iliyopita Shirikisho la Soka la Tanzania (TFF) liliongeza idadi ya wachezaji wa kigeni kwa Ligi Kuu Bara. Kila timu sasa inaruhusiwa kusajili wachezaji 10 wa aina hiyo, na ikiwezekana wote wanaruhusiwa kupangwa katika mchezo mmoja.

Kwa sababu ni wachezaji 10, tunasubiri kuona historia ikiwekwa kwa timu zetu tajiri, Simba, Yanga au Azam kupanga wachezaji 10 wa kigeni uwanjani na mmoja mzawa. Itatoa picha yenye kutafakarisha sana kwa sababu kuna mambo mengi nyuma yake.

Kwanza kabisa, tawala zinazokuja na kuondoka TFF huwa zinapandisha na kushusha idadi kutokana na tu na matakwa ya utawala uliopo. Inatokea tu na uimara au udhaifu wa viongozi waliopo. Mara nyingi ni klabu tatu za Simba, Yanga na Azam ndizo zinazoshinikiza idadi fulani kutokana na matakwa binafsi.

Lakini, pili tunarudi katika hoja ya msingi na kuamini kwamba, tumeamua kuwa Waingereza. Kuna hoja kwamba kutakuwa na msisimko. Kampuni zitavutika zaidi. Sawa kupanga ni kuchagua. Waingereza walipanga hivyo na kuamua kutoijali sana timu ya taifa. Leo wana timu ya taifa dhaifu huku wakiwa na ligi yenye msisimko mkubwa sana duniani.

Inakanganya kuona tangu mwaka 1992 wakati walipoipa Ligi Kuu yao muundo mpya, kila baada ya miaka minne ya Kombe la Dunia wamekuwa wakiwapokea wachezaji wa ligi yao wanaotoka mataifa mengine wakirudi na medali za ubingwa wa Kombe la Dunia. Wao ni watupu.

Tumechagua uwingi wa wageni lakini hatujui tunasimama wapi katika kulinda vipaji vya ndani. Waingereza wameanza kurudi nyuma na kufumua muundo wa soka lao la vijana ingawa bado wamewaachia wageni watambe.

Pamoja na yote hayo lakini uwepo wa wachezaji 10 wa kigeni umesababishwa na kila mmoja wetu. Kuanzia wachezaji wetu wenyewe, klabu zetu, TFF, Serikali na wengineo. Tusiilaumu TFF peke yake.

Kuna sehemu tumekosea. Kwanza nataka kuwalaumu zaidi wachezaji wetu. Vipaji bado vipo. Tatizo vipaji vyetu havijitambui. Wachezaji wetu wamekawaribisha wageni. Katika kuliona lango, Amiss Tambwe ana maajabu gani kuliko Jerson Tegete?

Nini kilimtokea Tegete kuondoka Yanga? Nani anaweza kuchunguza maisha ya nje ya uwanja kati ya Tegete na Tambwe? Lazima kuna sehemu mdogo wetu alikosea. Haiwezi kuwa bure. Pesa na sifa zote alizochuma Tambwe zilipaswa kwenda kwa Tegete.

Ungeweza kumleta mgeni gani kuja kucheza nafasi za kina Mohamed Hussein, Edibily Lunyamila, Hamis Gaga, Edward Chumilla na wengineo? Hapana. Isingewezekana.

Mchezaji wa kigeni alipwe pesa nyingi pale Coastal Union kwa ajili ya kucheza nafasi ya Ally Maumba au Kassa Mussa? Alihitajika kuwa mchezaji wa ajabu ulimwenguni kucheza nafasi ya Maumba.

Kuna mambo mawili katika hili.

Kwanza upatikanaji wa wachezaji hawa. Ilikuaje? Turudi nyuma na kujiuliza. Walikuwa wanapatikana vipi? Mashuleni? Mitaani? Au wapi? Na katika mfumo gani?

Tusisahau pia kuwa upatikanaji nao uliendana na misingi hasa ya mpira.

Washambuliaji walikuwa na maumbo makubwa kama kina Innocent Haule, mabeki wa kati walikuwa na maumbo makubwa. Kamtazame Idd Cheche mpaka sasa pale Azam FC. Anatisha kwelikweli.

Makipa walikuwa warefu na wana uwezo wa kudaka. Tofauti kabisa na makipa wa sasa. Kuanzia kina Mohamed Mwameja, Joseph Katuba, Paul Rwchungura, Riffat Said na wengineo wengi. Hebu nenda kamwangalie Juma Pondamali.

Lakini hapo hapo tujiulize, mbona wachezaji wa zamani walikuwa wanajifua sana. Mbona wachezaji wetu wamekuwa legelege katika dunia ambayo milango mingi ipo wazi? Zamani tulikutana na wachezaji wakifanya mazoezi binafsi Coco Beach. Ni hawa ndio ambao wamefanya Emmanuel Okwi kuwa staa wa kudumu katika ligi yetu.

Vipaji ni vilevile tu tofauti kubwa kati yao na sisi ni kujituma na nidhamu. Wachezaji wetu wajilaumu wenyewe kwa kuongezewa idadi kubwa ya wachezaji wa kigeni kwa sababu ya uvivu wao. Tungeweza kuwa na ligi tamu ya wachezaji wetu wenyewe kama tungeweza kurudisha nyuma zama za akina Hamis Gaga na pesa iliyopo nchini kwa sasa.

Matokeo yake pesa nyingi itakwenda kwa wachezaji 10 wa kigeni ndani ya klabu moja pengine kuliko pesa itakayokwenda kwa wachezaji wengine 15 wazawa ndani ya klabu hiyo.