Ishu ya Niyonzima Msimbazi ipo hivi

Muktasari:

  • Anafichua sababu zilizowafanya nyota hao kuwa nje na hata kurejeshwa kwao huku akifichua masharti waliyopewa. Pia anafichua njia ambazo watani wao Yanga wanaweza kujiponya kupitia hali ya ukata. Ni njia ipi? Endelea naye kuhitimisha mahojiano nayo...Endelea!

KATIKA kuhitimisha mfululizo wa makala za Kaimu Rais wa Simba, Salim Abdallah ‘Try Again’, aliyefanya mahojiano maalum na Mwanaspoti, leo Jumamosi anaendelea kufafanua mambo mbalimbali ndani ya klabu hiyo.

Anaeleza sababu zilizomfanya kiungo Haruna Niyonzima na beki Juuko Murshid waliokuwa nje ya kikosi hicho na jinsi walivyorejeshwa kuungana na wenzao.

Anafichua sababu zilizowafanya nyota hao kuwa nje na hata kurejeshwa kwao huku akifichua masharti waliyopewa. Pia anafichua njia ambazo watani wao Yanga wanaweza kujiponya kupitia hali ya ukata. Ni njia ipi? Endelea naye kuhitimisha mahojiano nayo...Endelea!

WAMTEGA AUSSEMS

Julai mwaka huu, Simba ilimleta Kocha Mkuu mpya, Patrick Aussems kutoka Ubelgiji ili kuchukua nafasi ya Mfaransa, Pierre Lenchatre. Mwanaspoti lilitaka kujua masharti waliyompa kocha huyo katika kazi yake ndani ya Simba.

Try Again anaeleza jukumu ambalo Aussems anatakiwa kulitekeleza kama malengo makuu katika ajira yake ni kuhakikisha anaifanya Simba inakuwa tishio ndani na nje ya nchi.

“Klabu yetu ina malengo na la kwanza ni kutetea ubingwa wetu na mashindano mengine ambayo yapo, kuna Kombe la Mapinduzi, Kagame, FA na Sportpesa.

“Kocha anajua hayo mashindano yote tunatakiwa kufanya vizuri, ila malego yetu mawili makubwa tuliyompa ni kuhakikisha kutetea taji la Ligi Kuu Bara na kuifikisha Simba hatua ya makundi kule CAF.

“Msimu uliopita tulishiriki Kombe la Shirikisho Afrika, lakini hatukufika mbali, ila kuna kitu tumejifunza kama uongozi jambo zuri mpaka tunatolewa Simba hatukufungwa tulitolewa kwa kanuni safari hii tumejianga katika Ligi ya Mabingwa Afrika.”

KAULI YA JPM

Alipoulizwa kama klabu yao imeifanyia kazi kauli ya Rais John Magufuli wakati akiwakabidhi taji la Ligi Kuu Bara pale Uwanja wa Taifa na kuutaka uongozi kusuka timu ya ushindi kwani, waliyokuwa nayo isingefika kokote.

Try Again alikiri waliifanyia kazi kauli hiyo kwa vitendo ndio maana ilifanya usajili wa maana dirisha lililopita ili kuifanya imara.

“Tulisajili timu kwa kuwa tuna malengo, nadhani kila mdau wa soka anakumbuka rai tuliyopewa na Rais Magufuli sasa unaweza kuona aina ya timu ikiwa na kiu ya kufikia malengo,” anasema na kuongeza;

“Wachezaji waliosajiliwa kwa sasa ni wa kiwango cha hali ya juu, tumefanya haya ili kuweza kukidhi kiu ya mashabiki wetu, Watanzania na hata kufanyia kazi Rais alichotueleza, tunaamini tutafanikisha kila tulilolipanga.”

KIKOSI GHALI

Simba imekuwa ikijinasibu kuwa msimu uliopita ilisajili kikosi cha Sh 1.3 bilioni, hata hivyo Try Again anapoulizwa kama ni kweli walitumia kiasi hicho cha fedha na kama hata kikosi chao cha sasa kina thamani hiyo anajibu;

“Kusema tumefaya usajili wa kikosi hiki tukitumia kiasi cha Sh 1 bilioni hapana jamani, ni vigumu kusema kikosi hiki kina thamani gani kwa kuwa takwimu kamili sina hapa, lakini ninachokuthibitishia hiki ni kikosi bora, kikosi cha gharama itoshe na Simba hii ni moja kati ya vikosi bora nchi hii.”

ISHU YA NIYONZIMA IKOJE?

Haruna Niyonzima, mmoja ya viungo mahiri waliowahi kucheza nchini kwa miaka ya karibuni akitokea nje, sambamba na beki Mganda, Juuko Murshid walikuwa nje ya Simba kwa muda mrefu, lakini ghafla juzi kati imetangazwa kurejeshwa kikosini na bosi huyo anafafanua ishu nzima ilivyokuwa.

“Haruna (Niyonzima) alikuwa ana shida kidogo baada ya kuanza kazi alipata majereha yaliyomweka nje kwa muda.

Yalihitaji matibabu ya kina, klabu tulichukua hatua za kumtibu, lakini baadaye kuna tabia ya utovu wa nidhamu aliionyesha.

“Kama uongozi tulisimama imara kuhakikisha tunamrudisha kwenye mstari na sasa Haruna amerudi kikosini, baada ya kukaa naye chini na kuwekana sawa kwa kutotaka mambo ya nyuma kujirudia tena. Lakini, sio Haruna pekee hata Juuko (Murshid) naye alikuwa na tatizo kama hilo la nidhamu.” anafafanua.

“Kurudi kwao kwetu ni wazi walitambua walichokosea kwani, waliandika barua za kuomba radhi na sisi kama uongozi tunahitaji huduma zao tukaona ni vyema tuwasamehe, ila tumewaonya na tumewaelekeza wote wataripoti kambini kuendelea na kazi.

JUUKO NAYE ASHANGAZA

Mashabiki wa Simba wamekuwa wakishangazwa na viwango viwili tofauti vya Juuko Murshid. Yule mkali anayekuwa timu ya taifa ya kwao Uganda ‘The Cranes’ na yule wa ovyo akikipiga Msimbazi. Try Again anakiri walimbana beki huyo kutaka kujua inakuwaje.

“Kwa Juuko pia tulihitaji kumuuliza na kumfahamisha kwamba, wanachama wetu wanalalamika akiwa timu ya taifa anaonekana imara, lakini unaporudi Simba kiwango chake kinaporomoka, naye ametueleza inatokana na nini.

“Lakini kwetu viongozi tunaridhika na kiwango chake. Angalia Juuko aliyecheza na Al Masry kiwango chake kilikuwaje mkumbuke Juuko aliyecheza na Gendamarie alikuwaje wakati mwingine mashabiki wetu wanatakiwa kutambua kwamba, hakuna kinachokaa katika kiwango cha juu wakati wote kuna wakati mchezaji anashuka kidogo.

MOTO WA

LIGI KUU

Try Again amefichua namna walivyoanza msimu mpya wa Ligi Kuu Bara kwa kusema; “Timu imeanza vyema ligi, kama mnavyojua kocha wetu ni mpya kuna mambo yanaendelea kubadilishwa taratibu uongozi tumewaachia makocha waendelee na kazi na kama kuna kitu wataona kinahitaji kuboreshwa tutasubiri ripoti yao, unajua makocha nao wanahitaji muda kuwasoma wachezaji wao.

MO Dewji MTU WA AINA GANI?

“MO Dewji anaipenda Simba, fikra zake wakati wote ni kutamani kwamba Simba inakuja kuwa klabu kubwa Afrika, akili yake yote akilala akiamka ni Simba ya Afrika ni mtu anayekuja kufanya biashara Simba amekuja kwa mapenzi ya klabu kuhakikisha anaisaidia Simba.

“Nimefanya kazi naye kwa karibu namuona ndoto zake na haya yote ambayo watu wanaona Simba inapata mafanikio kwa sababu naye anaweka juhudi za kusukuma maendeleo kwa kweli MO anafanya kazi kubwa.”

SIMBA IKIPIGWA?

Alipoulizwa pale Simba inapochemsha, Mo Dewji anakuwaje kama mtu mwenye mapenzi ya dhati na klabu hiyo?

“Ikitokea Simba inafanya vibaya MO anakuwa katika wakati mgumu, nashindwa nikuelezaje, lakini kama viongozi wenzake inabidi tupeane moyo kwa kumfariji kwamba, sawa hili limetokea ni matokeo ya soka, hivyo inafika wakati anaelewa kwani yeye ni mtu wa mpira.

“MO ni mfanyabiashara kuna wakati anapata faida kuna wakati anapata hasara na kwenye soka ni hivyo hivyo, kuna wakati utafanya vizuri na kuna wakati utatoa sare au kupoteza klabu gani haifungwi, kama ambavyo mashabiki wanaumia na hata yeye anaumia tunatoautiana maumivu.”

MCHANGO WAKE UKOJE?

“ Mchango wa MO sasa katka klabu yetu ni mkubwa sana, mafanikio yote unayoyaona sasa ni kwa sababu ya nguvu yake, amekuwa akihakikisha timu inacheza, inasafiri, inakula, tunafanya naye kazi kwa karibu tunashauriana kila wakati.”

Alipoulizwa kama Mo Dewji ni mtu sahihi ndani ya Simba katika mabadiliko ya mfumo mpya wa uendeshaji wa klabu hiyo? Try Again anajibu; “Kwa maana ya MO nafikiri hakuna mtu mwingine anaweza kufanya zaidi ya hiki, nafikiri watu wanakumbuka Simba ilipotoka na sasa mambo yakoje ukikumbuka maisha yale na haa nafikiri utaelewa nguvu ya MO.

WITO KWA

WANASIMBA

“Simba bado ipo katika kipindi cha mpito wito wangu kwa wanachama na mashabiki utulivu uliopo sasa unapaswa kuongezeka ili kusudi kuwapa nafasi viongozi kuwatumikia. Simba ipo katika mikono ya viongozi salama na tunafanya kazi kwa kutanguliza maslahi ya klabu.”

MISHAHARA VIPI?

“Kusema ukweli fedha za mishahara zimepanda, mishahara ni mikubwa unajua sio vyema kuweka wazi mshahara wa mtu, lakini Simba ya sasa ni moja ya kikosi ghali nadhani tunaweza kuwa ndiyo kikosi ghali zaidi.

Juu ya mapato ya klabu, Try Again anasema; “Mapato yameshuka hata sasa bado yako chini na yameshuka sababu kubwa ni kukuwa kwa teknolojia hivyo, hali ya uwanjani kwa kweli ni mbaya, kuandaa mechi moja ya Simba inagharimu kiasi cha sh 20 milioni lakini unachokuja kupata mwisho wa mechi ni kuanzia Sh 5-7 milioni unaweza kuona hali ilivyo.

Zipo changamoto nyingi moja ni upatikanaji wa tiketi hasa hapa Dar es Salaam na hili linatokana na hii teknolojia wakati fulani mfumo uliopo unamkatisa tamaa mtu anayetaka kuja uwanjani mtu anaamua kuangala kwenye televisheni.

Lingine ni suala la kupangwa kwa mechi muda ambao, sio rafiki kwa wengine chukulia mfano kuna mechi zinachezwa katikati ya wiki kumbuka watu wengi muda huo wanakuwa katika majukumu watakaoweza kuja ni wale wachache.

Bado kama klabu tunakusudia kuchukua hatua zaidi kuwavuta wanachama na mashabiki wetu kuja viwanjani uwepo wao uwanjani una faida kubwa, kwanza klabu itapata mapato lakini pili shabiki naye ni mchezaji anatakiwa kushangilia ili yule mchezaji wa uwanjani aweze kujituma zaidi.

MRADI WA JEZI

“Mradi wa jezi unaendelea tumepata mwekezaji tumemkabidhi jukumu mauzo yanaendelea kwa sasa sina takwimu sahihi, lakini nafikiri tunakwenda vizuri.

Kazi hii kama klabu tumeianza msimu huu, msimu uliopita tulianza kwa kujaribu kwa kumpa mtu afanye biashara hii tunaangalia changamoto zake kama mnavyojua bado mwamko wa watu kutambua umuhimu wa kununua mali ya klabu ni mdogo, lakini tunaendelea kupanua masoko ili kuwafikia walaji tusisahau changamoto ya wale wanaotoa jezi feki lakini tutapambana nao.

LIGI BILA MDHAMINI IKOJE?

“Ligi kuanza bila mdhamini hii ni changamoto kubwa kwa sababu tulikuwa tunapata vifaa, safari hii hakuna tumelazimika kununua. Tulikuwa tunapata fedha kila baada ya muda fulani maingizo hayo hayapo sasa.

Nadhani sio Simba tu klabu zote zitaathirika na hili kwa hivyo TFF waendeleze jitihada kuhakikisha mdhamini anapatikana haraka ili kuleta ubora wa ushindani.

YANGA IPITE

WAPI

Klabu ya Yanga tangu msimu uliopita iliyumba kiuchumi na kusababisha kwa sasa kutembeza bakuli, hata hivyo Try Again ameipa akili klabu hiyo ili kuweza kurejea kwenye mstari.

“Yanga ni klabu kubwa na wala Yanga haijawahi kuwa klabu ndogo au dhaifu hili tusidanganye.

Yanga iko imara na najua kwamba klabu hiyo ina viongozi ambao, wanakaa na kuzungumza klabu yao inatoka katika matatizo waliyokuwa nayo, lakini kikubwa Simba tunaona Yanga wanatakiwa kufanya utayari wa mabadiliko ya mfumo ili waweze kwenda katika mfumo wa kisasa hapo ndipo watakapotoka walipo.

“Kwa ilivyo sasa Yanga hawana uhakika wa mdhamini ukiondoa Sportpesa hawana mtu, ambaye anaweza kujitolea kwa kiwango kikubwa kwa ajili ya kutoa fedha wakati mwingine huwezi kutegemea fedha za mtu sana kila wakati hivyo lazima Yanga iwe kama taasisi, ni vizuri viongozi wa Yanga wakae chini na waangalie wapi mapungufu yapo naamini watapata majibu ili kuhakikisha wanatoka walipo.