Ibrahim Ajibu, Mkude hawana kasoro hizo

Saturday October 7 2017Joseph Kanakamfumu

Joseph Kanakamfumu 

By Joseph Kanakamfumu

ETI, Ibrahim Ajibu ni mvivu wa mazoezi asiyependa kujituma akiamini ameshaujua mpira tayari. Anafananishwa na mwendesha baiskeli asiyehitaji kurudia kujifunza baada ya kujua tayari.

Hata Jonas Mkude anasemwa kuwa si mzuri katika kupiga pasi ndefu kwa kuwa huwa anajiwekea kijieneo chake cha kukimbia uwanjani, hivyo si mzuri wa pasi unapomlinganisha na James Kotei au Mzamiru Yassini.

Haya ni maneno yaliyoandaliwa na baadhi ya mashabiki wa soka wasiowatakia mema wawili hao, hasa walipokuwa pamoja pale Simba. Kwa sasa Ajibu yupo zake Yanga. Ni maneno yaliyolenga kuwavuruga kutokana na kilichotafsiriwa kiburi chao walipokataa kusaini mikataba mipya kwa maslahi madogo. Ndipo baadhi ya viongozi walipowapandikizia mbegu mbaya kwa mashabiki.

Kulikuwa na mkakati wa kuhakikisha wawili hao wanapunguzwa viwango kwa kuwaweka benchi pia. Iliwatokea msimu huo ulipita Simba ilipoenda Kanda ya Ziwa kwa mechi dhidi ya Kagera Sugar na Mbao FC, waliwekwa benchi dhidi ya Mbao.

Kuelekea usajili mkubwa, Simba ilimleta kiungo Mghana, James Kotei ili kuja kumchangamsha Mkude.

Kwa ujumla, wadau hasa mashabiki wa Simba, waliwavisha tabia hizo wawili hao ili tu umma ujue wana makosa ya kiufundi kuhalalisha makosa ya kutowatumia kwa dakika zote tisini, kubwa ilikuwa ni kupunguza uwezo wao uwanjani.

Hadi sasa bado kuna wadau wengi wa soka wakiwamo baadhi ya waandishi wa habari wanaoendelea kutoa sababu hizo dhidi ya Mkude na Ajibu. Binafsi naamini huo ni mwendelezo tu wa chuki binafsi.

Bahati mbaya kwa Mkude bado yupo Simba ambako wamekwenda mbali zaidi hadi kumvua kitambaa cha unahodha. Mkude licha ya kudaiwa kucheza chini ya kiwango, pia anadaiwa kuonekana sehemu nyingi a starehe hadi usiku wa manane.

Sikubaliani na sababu hata moja kati ya hizi zinazosemwa kwa Mkude na Ajibu kwani hazina hata chembe ya ukweli. Tuache ushabiki tuzungumze ukweli.

Kwanza si kweli kuwa Mkude hucheza katika eneo dogo, si kweli pia kwamba yeye si mpigaji wa pasi ndefu. Ilikuwa kawaida kuiona Simba ikicheza mfumo wa kuwa na viungo wengi hadi kufikia watano. Hii ilimaanisha haikuwa na sababu ya kuwategemea washambuliaji wa pembeni wenye kasi, hii ilikuwa kabla ya msimu uliopita uliomleta Shiza Kichuya.

Kwa hapa ilimaanisha si Mkude, si Mwinyi Kazimoto na wala si Said Ndemla waliojenga tabia ya kupiga pasi ndefu kwa washambuliaji wao, timu nzima ilicheza pasi fupi nyingi hadi eneo la ushambuliaji. Ulikuwa mfumo wa timu.

Pili si kweli Ajibu ni mvivu asiyependa mazoezi. Kwenye soka kuna aina mbili za wachezaji, kwanza ni wale wasio na vipaji halisi. Hawa hulazimika kufanya mazoezi mengi na kujituma mno mazoezini na kwenye mechi. Wachezaji wa aina hii wakikosa mazoezi ya siku mbili tu, ufanisi wao uwanjani hupotea kabisa.

Aina ya pili ya wachezaji ni wale wenye vipaji halisi vya kuzaliwa. Wachezaji aina hii si kwamba hawahitaji mazoezi, hujifua pamoja na wenzao kama kawaida lakini kwao mpira huwa rahisi. Ukiwakuta mazoezini, unaweza kudhani hawajitumi, lakini hufanya mambo yote kwa ufasaha mkubwa.

Ajibu anaangukia kwenye aina hii ya pili ya wachezaji, ana kipaji halisi. Ajibu si mvivu kwani angekuwa hivyo, kocha asingeweza kumpa nafasi ya kucheza dakika 90.

Mwangalie Ajibu huyu aliyepo Yanga. Katika mechi tano ambazo wameshacheza hadi sasa msimu huu wa Ligi Kuu Bara, ametumika kikamilifu dakika zote 90 katika michezo minne dhidi ya Njombe Mji, Majimaji, Ndanda FC na Mtibwa Sugar, tena hakuwahi kuonyesha dalili ya kuchoka. Angekuwa mvivu kweli ingewezekana?

Kwa hiyo watu wasitumie chuki walizonazo kueneza sababu za kuwatenga baadhi ya wachezaji ili kuwatoa kwenye vikosi bila sababu za maana za kiufundi.