INAWEZEKANA: Riyad Mahrez alipaswa kwenda Manchester City

Muktasari:

Katika saa za mwishoni mwa dirisha hilo, kulikuwa na tetesi nyingi kwamba nyota wa Leicester City, Riyad Mahrez, atajiunga na Manchester City, lakini mwisho wa siku Leicester iliikata ofa ya Man City kumsajili mchezaji huyo kwa Pauni 50 milioni.

MSOMAJI dirisha ndogo la uhamisho kule Ulaya lilifungwa wiki iliyopita na katika siku ya mwisho wa uhamisho maarufu kwa jina la ‘Dead Line Day’, klabu nyingi ziliweza kukamilisha usajili wa wachezaji wazuri.

Katika saa za mwishoni mwa dirisha hilo, kulikuwa na tetesi nyingi kwamba nyota wa Leicester City, Riyad Mahrez, atajiunga na Manchester City, lakini mwisho wa siku Leicester iliikata ofa ya Man City kumsajili mchezaji huyo kwa Pauni 50 milioni.

Uamuzi wa Leicester City umewashangaza wengi kutokana na sababu nyingi.

Kwanza kabisa Pauni 50 milioni ni nyingi kwa mchezaji ambaye kwa kweli hajakuwa katika fomu kali ambayo alikuwa nayo mwaka 2016, pale Leicester iliposhinda Ligi Kuu England.

Hivyo kukataa kumuuza kwa pesa hiyo ndefu hakuingii akilini kirahisi mara moja. Imeshangaza watu wengi.

Lakini, labda kinachoshangaza zaidi ni Mahrez ameomba kuhama klabu ya Leicester katika madirisha mawili mfululizo na klabu hiyo bado imekata kumwachia kuondoka.

Mahrez amejituma sana katika miaka ya hivi karibuni akiivaa jezi ya Leicester na mchezaji mwenye kiwango chake anastahili kucheza katika moja kati ya klabu bora zaidi nchini England.

Naelewa Mahrez ni mchezaji muhimu katika kikosi cha Leicester msimu huu na katika dirisha hili Leicester haikuwa na nafasi ya kusajili mchezaji wa kuziba pengo lake.

Lakini, Leicester ni timu ambayo ipo katika nafasi katika Ligi Kuu ambayo inaruhusu kuumuza Mahrez. Hivi sasa imeshika nafasi ya nane na haipo katika hatari ya kushuka daraja na pia haina uwezo wa kufuzu Ligi ya Mabingwa au Ligi ya Ulaya.

Hivyo huu ulikuwa muda mwafaka wa kuumuza Mahrez kama mchezaji huyu kweli anataka kuhama klabu hiyo.

Mahrez sasa amekasirika kutokana na Leicester kutokubali kuumuza. Huenda hii ilikuwa nafasi yake kubwa kujiunga na timu bora zaidi England hivi sasa na kuendelea zaidi kimpira chini ya uongozi wa Pep Guardiola.

Wiki iliyopita Mahrez alikataa kufanya mazoezi na timu yake na hali katika timu hiyo ni tete. Kwa mtazamo wangu, Leicester imefanya kosa kutomuuza Mahrez kwa kuwa kuna dalili nyingi mchezaji huyu hayupo katika hali nzuri kisaikolojia na kuna uwezekano hatajituma katika mechi zilizobaki msimu huu.

Mahrez hatashiriki katika Kombe la Dunia na nchi yake ya Algeria na hivyo hahitaji kupambana kuhakikisha anapata nafasi katika timu yake ya taifa.

Mahrez pia ameonya hatacheza mechi na Leicester tena na kama mchezaji huyu anashindwa kuwa katika hali nzuri kimpira katika mechi zilizobaki msimu huu, basi Leicester italazimishwa kuumuza kwa bei ndogo katika dirisha kubwa la usajili mwaka huu.

Hivyo, kwa mtazamo wangu mchezaji huyu alipaswa kuwa ameuzwa kwenda Manchester City siku ya mwisho ya dirisha la Januari la sivyo. Leicester itakuja kupata hasara.