INAWEZEKANA: Nini? Morocco wapo vizuri

Tuesday November 14 2017Olle Bergdahl Mjengwa

Olle Bergdahl Mjengwa 

By Olle Bergdhal Mjengwa

MSOMAJI, sasa tunazifahamu timu tano ambazo zitaiwakilisha Afrika katika Kombe la Dunia kule Urusi mwakani.

Timu hizo ni Morocco, Misri, Tunisia, Senegal na Nigeria. Hivyo, wakongwe kutoka Afrika kama Ghana, Cameroon na Ivory Coast wote wamekosa tiketi ya kwenda Urusi mwakani.

Kabla mzunguko wa mwisho wa mechi za kufuzu Kombe la Dunia, Ghana na Cameroon walikuwa wameshakosa nafasi ya kufuzu kushiriki michuano hiyo mikubwa zaidi Ulimwenguni. Kwa upande wa Ivory Coast bado walikuwa na nafasi kubwa, lakini ni wazi kwamba walishindwa kabisa kuitumia nafasi hiyo.

Katika mechi yao ya mwisho, Ivory Coast walihitaji kuwafunga Morocco, lakini mambo yakawa tofauti. Ifahamike wazi kuwa mechi hiyo ilichezwa katika uwanja wa nyumbani wa Ivory Coast.

Kutokana na umuhimu wa mechi hiyo, niliamini Ivory Coast wangefanya kila wanachoweza kuhakikisha wanapata ushindi, lakini, kutoka mwanzo wa mechi nilishaangaa jinsi wachezaji wao walivyocheza kwa kujiachia kama vile haukuwa mchezo muhimu.

Morocco ilikuwa timu iliyocheza kwa moyo mkubwa na matokeo yake Ivory Coast walifungwa 2-0. Rekodi mpya ikaandikwa kwani ni kwa mara ya kwanza tangu mwaka 2006 Ivory Coast haitashiriki fainali za Kombe la Dunia.

Ni wazi kwamba Ivory Coast wapo katika mchakato wa kubadilisha kizazi. Na hivi sasa hakuna wachezaji wenye uwezo wa kuziba pengo la kizazi cha dhahabu cha Ivory Coast iliyokuwa na wachezaji kama Didider Drogba, Yaya Toure, Kolo Toure, na Emmanuel Eboue.

Lakini, yumkin wachezaji kama Wilfred Zaha na Eric Bailly wataendelea kimpira wanaweza kurudisha heshima ya Ivory Coast ndani ya miaka michache tu ijayo. Wachezaji hawa bado wana umri mdogo na naamini watakuwa viongozi wapya katika kikosi cha Ivory Coast.

Kwa upande wa Morocco naamini watawakilisha bara la Africa vizuri katika Kombe la Dunia. Timu hiyo ilihitaji tu sare ili wafuzu Kombe la Dunia lakini Morocco walisafiri nchini Ivory Coast na nia ya kushinda mchezo huo na walicheza mpira wa kushambulia katika mechi nzima.

Kocha wa Morocco, Herve Renard ni mwanaharakati na ni kocha ambaye atasakwa na timu nyingi za taifa barani Afrika bada ya mkataba wake na Morocco kuisha.

Kocha huyu sasa ameshinda Kombe la Afrika mara mbili na ameipeleka Morocco Kombe la Afrika na sasa Kombe la Dunia.

Morocco hawana kikosi bora barani Afrika katika karatasi, lakini chini ya uongozi wa Renard timu hiyo sasa ina umoja mzuri na wanacheza kwa kujituma sana hivyo nasubiri kwa hamu kuona jinsi watakavyo pambana na timu kubwa kabisa ulimwenguni katika Kombe la Dunia mwakani.