INAWEZEKANA: Kizazi kipya Hispania kitatisha

Muktasari:

Lakini, katika miaka ya hivi karibuni dalili zote zimeonyesha kwamba timu ya taifa ya Hispania inahitaji mabadiliko.

BILA shaka, timu ya taifa ya Hispania ni timu ambayo imepata mafanikio makubwa.

Tangu mwaka 2008, Hispania wameshinda mashindano ya Euro mara mbili na Kombe la Dunia mara moja.

Lakini, katika miaka ya hivi karibuni dalili zote zimeonyesha kwamba timu ya taifa ya Hispania inahitaji mabadiliko.

Katika mashindano mawili mfululizo Hispania hawajakuwa karibu kabisa kushinda taji.

Katika Kombe la Dunia nchini Brazil mwaka 2014, Hispania walitolewa katika hatua ya kwanza na katika mashindano ya Euro mwaka jana walitolewa hatua ya pili.

Kocha mkongwe wa Hispania, Vincent Del Bosque alijiuzulu baada ya mashindano ya Euro mwaka jana.

Na Julen Lopetegui aliteuliwa kuwa kocha mpya wa timu hiyo. Kocha huyu ana jukumu kubwa la kuirudisha Hispania katika ubora wao.

Umebaki mwaka mmoja tu hadi kufanyika kwa Fainali za Kombe la Dunia zitakazochezwa nchini Urusi mwakani na mechi nyingine za kufuzu kwa fainali hizo zinaanza kufikia mwisho.

Wikiendi iliyopita Hispania waliwafunga Italia magoli 3-0 na hivi sasa Hispania wanaongoza kundi lao kwenye mechi za kufuzu Kombe la Dunia.

Wamepania na wanataka kuhakikisha kuwa wanafika mbali kama si kurudisha heshima ya taifa hilo katika soka.

Ni imani yangu kwamba Hispania wamepata matokeo kutokana na kuwapa kizazi kipya nafasi katika timu ya taifa.

Hakika, wachezaji kama Iniesta, Silva, na Xabi Alonso wameibeba timu ya taifa ya Hispania kwa muda mrefu.

Lakini, wachezaji hawa wameshafikia umri mkubwa na fainali za Kombe la Dunia zitakapochezwa nchini Urusi, mchezaji kama Iniesta atakuwa amechafikia umri wa miaka 34.

Bahati ya timu ya taifa ya Hispania ni kwamba kuna kizazi kipya cha wachezaji wenye uwezo wa kuziba pengo la akina Iniesta.

Ni wachezaji kama Isco na Asensio ambao wote wanachezea Real Madrid, pamoja na Thiago Alcantra ambaye anachezea Bayern Munich, na Alvaro Morata kutoka Chelsea.

Hispania wanacheza mfumo wa mpira ambao unatumia viungo wengi wenye kiwango kikubwa.

Isco na Thiago Alcantra wote ni viungo wenye umri mdogo lakini wana vipaji vikubwa.

Hata hivyo, chini ya kocha wa zamani wa Hispania Vincent Del Bosque, wachezaji hawa hawakupata nafasi nyingi katika kikosi cha kwanza cha Hispania kutokana kuwepo na upinzani mkubwa.

Lakini, kocha mpya wa Hispania, Lopetegui, anataka kukiendeleza kikosi cha Hispania na kuwapa wachezaji wenye umri mdogo nafasi katika timu ya taifa.

Wachezaji kama Isco na Morata hawajawahi kushinda taji na timu yao ya taifa na wana njaa ya kupata mafanikio na timu yao ya taifa.

Bila shaka Hispania wana kizazi kipya ambacho kina uwezo wa kuipeleka Hispania mbali sana katika Kombe la Dunia mwakani lakini pia wanaweza kuibeba nchi hiyo katika mashindano mbalimbali Ulaya.