INANOGA Huu ndo ule utamu wa Ligi Kuu England

Muktasari:

  • Kwa mamilioni ya mashabiki duniani kote, kwao Ligi Kuu England ndiyo inayoonekana kuwa na mvuto zaidi kutokana na kuwa na mambo mengi yanayovutia kwa kila msimu.

LONDON, ENGLAND. KOMBE la Dunia limeshakwisha na sasa mashabiki wa soka duniani kote wamehamishia akili zao kwenye soka la ligi za ndani.

Kwa mamilioni ya mashabiki duniani kote, kwao Ligi Kuu England ndiyo inayoonekana kuwa na mvuto zaidi kutokana na kuwa na mambo mengi yanayovutia kwa kila msimu.

Hizi hapa data matata kabisa zilizoacha kumbukumbu nzuri kwa msimu uliopita kwenye Ligi Kuu England, huku Manchester City iliyokuwa bingwa ikiweka rekodi ya kufikia pointi 100, wakati Mohamed Salah alikuwa bize tu kutupia mipira kwenye nyavu za wapinzani.

1.Manchester United ilishinda kila mechi ya Ligi Kuu England ambayo ilikuwa ya kwanza kufunga bao kwenye mechi husika. Ilifanya hivyo kwenye mechi 21 na hivyo kuwa timu ya kwanza kufanya hivyo tangu Portsmouth kwenye 2007-08. Yenyewe ilishinda kwenye mechi 14 ilizotangulia kupata bao kwenye Ligi Kuu England.

2.Mohamed Salah alikuwa mchezaji wa kwanza kufunga mabao manne katika mashuti yake manne aliyopiga kulenga goli la wapinzani kwenye Ligi Kuu England tangu alipofanya hivyo staa wa zamani wa Arsenal, Andrey Arshavin kwenye mechi dhidi ya Liverpoo, Aprili 2009.

3.Jamie Vardy amekuwa mchezaji wa kwanza kuzifunga timu zote zilizomaliza Top Six kwenye Ligi Kuu England ndani ya msimu mmoja, baada ya staa huyo wa Leicester City, kuweka kwenye kamba katika mechi dhidi ya Arsenal, Chelsea, Liverpool, Manchester City, Manchester United na Tottenham Hotspur.

4.Mechi baina ya Arsenal na Chelsea, London derby iliyopigwa uwanjani Emirates Januari mwaka huu, ilikuwa ni mchezo wa 500 kumalizika kwa sare ya 2-2 kwenye historia ya Ligi Kuu England. Hiyo ni rekodi tamu kabisa kwenye historia ya ligi hiyo huku Arsenal na Leicester City zikiwa sehemu ya rekodi.

5.Kiungo wa Leicester City, Wilfred Ndidi alikuwa mchezaji wa kwanza kuonyeshwa kadi nyekundu kwenye mchezo wa Ligi Kuu England siku yake ya kuzaliwa tangu ilipowahi kutokea hivyo kwa Dwight Gayle wa Crystal Palace kwenye mechi dhidi ya West Ham United iliyofanyika Oktoba 17, 2015.

6.Frank de Boer aliweka rekodi ya kuwa kocha mkuu wa kwanza kwenye historia ya Ligi Kuu England akishuhudia timu yake ikishindwa kufunga bao katika kipindi chake cha ukocha kwenye kikosi cha Crystal Palace. De Boer alisaini mkataba wa miaka mitatu, lakini alidumu na timu hiyo kwa wiki 10 tu, akatimuliwa baada ya timu kucheza dakika 450 bila bao hata moja.

7.Wanasema mtoto wa nyoka ni nyota. Kasper Schmeichel aliweka rekodi ya kuokoa penalti nyingi kwenye Uwanja wa Old Trafford kwenye mechi ya Ligi Kuu England kuliko ilivyowahi kutokea kwa Peter Schmeichel, ambaye ni baba yake na alikuwa akiidakia Manchester United.

Ina maana, Kasper wa Leicester City ameokoa penalti moja kwenye mechi ya ligi iliyofanyika uwanjani Old Trafford, wakati Schmeichel baba ameokoa penalti 0.

8.Straika Wayne Rooney, ambaye msimu ujao hatakuwapo kwenye Ligi Kuu England, ameweka rekodi mpya kwenye ligi hiyo baada ya kusubiri kwa muda mrefu zaidi wa kufunga bao kwenye timu moja.

Rooney alikutwa na ukame wa kufunga bao kwa siku 4869.