KWAKO MWALIMU KASHASHA: Huu usajili wenu wa dirisha dogo unanishangaza

Dhana ya neno usajili inatupeleka kwenye fikra za kuleta uhalali wa jambo jipya, kitu kipya au mtu mpya kwa mantiki ya kuendeleza mfumo na uhai katika utendaji wenye tija .Hivyo mchakato wa usajili unahitaji hufanyika kwa kuzingatia weledi, malengo ,shabaha na tija inayotarajiwa kupatikana au kuonekana.

Kwa miongo kadhaa soka la Tanzania linapita katika mabadiliko mengi mbalimbali kama ilivyo katika nchi nyingine ili kupata sura ya soka la kisasa linalochezwa kwa kasi na mchanganyiko wa mbinu tofauti kulingana na mfumo/mifumo inayoendelea kuibuka kila mara.

Kwa kawaida ujenzi wa timu bora na imara kiwanjani unategemea upatikanaji wa mahitaji muhimu ya wachezaji, miundombinu, wataalamu mbalimbali kama vile afya, lishe na kufundisha lakini pia wachezaji wazuri watakaounda kikosi bora, kizuri na chenye uwezo wa nguvu za kupambana na timu pinzani katika ngazi husika, hapo ndipo dhana ya usajili inapochukua nafasi yake.

Kuanzia mwishoni mwa miaka ya 90 kuelekea 2000 mpaka sasa, usajili wa wachezaji katika soka la Tanzania hususani katika klabu zinavyocheza Ligi Kuu umekumbwa na vituko, vihoja na misukosuko mingi isiyokuwa ya lazima kutokana na njia na mbinu zinazotumika kuwapata wachezaji wa kuzitumikia timu zetu mbalimbali ili kupata mafanikio; ubingwa, kucheza mashindano ya kimataifa,kubaki katika ligi au kukwepa kuteremka daraja.

Wadau, wapenzi na mashabiki wa soka bila kujali itikadi zao wameyaona mengi, lakini hali ni mbaya zaidi katika timu kongwe za Simba na Yanga ambazo imekuwa kama desturi kwamba, kipindi cha usajili kinapoanza hasa katika timu za daraja I, II na Ligi Kuu sinema ya sarakasi za usajili nayo inaanza, bahati nzuri vyombo vyote vya habari navyo vinakaa tayari kwa ajili ya kutuhabarisha na kutuonyesha picha za hatua nzima linavyoanza hadi linapokamilika.

Kwa kiwango kikubwa ni vichekesho vitupu vinavyofanyika wakati huu, swali la tulio wengi ni moja tu, je, ni kanuni ipi na ni utaratibu gani maalumu unawaongoza wale wenye dhamana ya kusajili wachezaji katika klabu?

Nathubutu kusema kwamba binafsi sijapata jibu la moja kwa moja kwa sababu matatizo na malumbano wakati wa usajili ni yale yale yanayojirudia kila msimu iwe ni wakati wa dirisha kubwa au dogo kama hili lililofunguliwa juzi juzi na TFF kwa ajili ya timu za ligi kuu.

Nisingependa kuainisha mifumo na utaratibu unaotumika katika mataifa yaliyoendelea katika soka, kwa sababu mazingira (context) hayafanani katika mambo kadhaa kwa mujibu wa muktadha wa kazi ya usajili wa wachezaji isipokuwa weledi na maarifa yanayohitajika yanaweza yasitofautiane sana kati ya nchi na nchi.

Yapo mengi yanayokera sana katika usajili wa timu zetu kiasi kwamba inaashiria kukosa weledi wa kutosha, kanuni na mfumo mzuri ndani ya klabu wa kubaini vipaji, kutambua mahitaji halisi ya timu ( ni aina gani ya mchezaji anayetakiwa), kuelewa vipaumbele vya mwalimu au benchi la ufundi. Hali hii inaonesha kama vile usajili ni kwa ajili ya fasheni tu au unafanyika kwa lengo la kukomoana au kulipiza kisasi.

Ukiangalia kwa jicho la tatu utaona kuwa nchi yetu ina wachezaji wengi wazuri na wenye vipaji vya kutosha, inakuwaje wakati wa usajili viongozi wanalumbana na kutumia muda mwingi kumgombania mchezaji mmoja? au hata kama ni wa kigeni timu moja ikifanikiwa kufanya mazungumzo na mchezaji X , taarifa zikavuja mara moja utasikia na timu nyingine imewatuma viongozi kwenda kumshawishi mchezaji huyo huyo ili abadili mwelekeo kwa nia ya kujiunga na timu nyingine.

Hii ni ajabu na fedheha katika soka.Mtazamo huu na tabia hizi zipo hata huko ulaya lakini siyo kama jinsi inavyofanyika hapa kwetu.

Kibaya zaidi baadhi ya wachezaji wa ndani au nje wakipata mikataba baada ya kusajiliwa wanaonekana ni wa kawaida mno kiasi cha kushindwa kuzibeba timu zao na hivyo kuzisababishia hasara ya mamilioni ya shillingi, hapa nako kuna maswali tunajiuliza;ni kina nani hasa waliohusika kuwasajili hawa? Kwa maelekezo au ushauri upi wa kitaalamu? ingawa wakati mwingine wapo wachezaji wazuri sana wanaonunuliwa kwa mbembwe nyingi na kauli za majivuni na sifa tele,lakini mara tu wakishapewa mkataba hawapati nafasi ya kucheza hata mechi ni nyepesi mwisho wa siku tunasikia wanalaumiwa na kubezwa kwamba viwango vyao vimeshuka, je? nini chanzo cha kushuka kiwango?

Haituingii akilini mchezaji aliyekuwa nyota wa kutegemewa kwa msimu mzima katika timu yake ya zamani mathalani Mbao, Majimaji, Singida United,Ndanda akihamia Simba au Yanga unashangaa baada ya miezi miwili au mitatu maneno yanaanza kutoka kwa waajiri wake wakijaribu kuushawishi umma hususani wapenzi na wadau wa soka kwamba tayari mchezaji fulani amechuja na hafai hivyo inapendekezwa atolewe kwa mkopo au mkataba wake uvunjwe, ukiuliza sababu oh! hafungi magoli.

Kwa mtindo huu wa kusajili bila kuheshimu ushauri na mapendekezo ya kitaalamu ya benchi la ufundi katika klabu nyingi , timu zitaendelea kupoteza rasilimali fedha, kuua vipaji lakini kibaya zaidi tutazidi kuchelewa kupiga hatua katika soka la ushindani.

Lazima kufanya usajili kila wakati, tunatakiwa kuelewa kwamba timu haijengeki kwa mara moja ,wachezaji wanahitaji mwendelezo wa mafunzo ya mbinu na ufundi,hivyo wanahitaji kuzoeana kwa muda mrefu ili kutengeneza umoja wa hali ya juu nje na ndani ya kiwanja,kwani umoja ni nguzo muhimu sana kwa ajili ya timu kupata ushindi.

Kuna nadharia katika soka inasema (talents win games, but teamwork and intelligence win championship). Kimsingi zoezi zima la usajili linahitaji utulivu na umakini.