INAWEZEKANA: Hizi ndio mechi ambazo PSG inahitaji kushinda

Tuesday February 13 2018Olle Bergdahl Mjengwa

Olle Bergdahl Mjengwa 

By Olle Bergdahl Mjengwa

MSOMAJI, Ligi ya Mabingwa Ulaya, inaendelea tena wiki hii. Hatua ya pili ya ligi hii inaleta mechi nyingi kali huku klabu nyingi kubwa zikikutana.

Lakini katika mechi zote zitakazochezwa katika mzunguko huu, naamini macho ya mashabiki wengi wa soka yatakuwa katika mechi mbili za PSG na Real Madrid.

Katika miaka ya hivi karibuni, PSG imetaabika kufika mbali katika Ligi ya Mabingwa Ulaya na msimu uliopita ilitolewa mzunguko wa pili ilipoumana na Barcelona.

Hata hivyo, ni wazi PSG ni klabu yenye malengo makubwa. Tangu iliponunuliwa na kampuni ya Qatar Sports Investment, PSG, wamekuwa na uwezo wa kusajili kati ya wachezaji bora duniani. Ni wachezaji kama Mbappe, Edinson Cavani, Di Maria na Neymar.

Kutokana na uwezo huu wa kusajili wachezaji wenye kiwango kikubwa, basi PSG imetawala soka la Ufaransa.

Timu hii imeshinda Ligi Kuu Ufaransa mara nne katika misimu mitano ya mwisho na imeshinda Kombe la Ufaransa mara nne mfululizo. Hivyo, ni wazi kuna klabu chache zinazoweza kuipa PSG upinzani nchini Ufaransa.

Na ndio maana PSG kwa muda mrefu pia imetaka kupata mafanikio makubwa nje ya mipaka ya Ufaransa. Ina hamu kubwa sana ya kutawala soka la Ulaya na kushinda Ligi ya Mabingwa. Na bodi ya PSG ina lengo la kuijenga klabu yao kuwa kati ya klabu kubwa zaidi duniani.

Kabla msimu uliopita, PSG iliteua kocha mwenye uzoefu mkubwa wa kupata mafanikio makubwa katika Ligi ya Ulaya ‘Europa League’.

Ni Unai Emery ambaye alishinda Europa League mara tatu mfululizo na kikosi cha Sevilla na kujiandikia ufalme wake ulimtangaza zaidi.

Hakika, Ligi ya Mabingwa ni mashindano magumu kuliko Europa League, hata hivyo, mafanikio makubwa ya Emery katika Europa League ni dalili kwamba kocha huyu pia ana uwezo wa kufanya makubwa katika Ligi ya Mabingwa.

Katika hatua ya kwanza ya Ligi ya Mabingwa msimu huu, PSG ilionyesha kwamba timu yao imeendelea sana kimpira huku ikishinda kundi lao ambalo pia ilikuwa na timu kongwe kama Bayern Munich.

Kwa mtazamo wangu, Real Madrid ni timu ngumu zaidi kuifunga kuliko Bayern Munich hususan katika Ligi ya Mabingwa, lakini kikosi cha Zinedine Zidane hakijakuwa katika hali nzuri kimpira katika mechi nyingi msimu huu.

Imekuwa ikitaabika kwao Hispania ikiwachwa pointi kadhaa nyuma na wababe wenzao kwenye msimamo wa Ligi Kuu Hispania. Wakati Barcelona inazo 58 yenyewe ndio kwanza imekusanya alama 42 tu huku zote zikiwa zimecheza sawa, mechi 22.

Hivyo, nashawishika kuamini PSG inayo nafasi ya kuitoa Real Madrid katika Ligi ya Mabingwa.

PSG pia ina wachezaji ambao wanaweza kulinganishwa na wale wa Real Madrid katika nafasi nyingi. Na kama PSG kweli inataka kupiga hatua kubwa na kutawala soka la Ulaya, basi ni lazima washinde mechi za aina hii.