MAONI: Hili la Mbeya City na Yanga lije na majibu yanayoeleweka

Muktasari:

Tunasema wachezaji 12 kwa maana kuwa uwanjani walikuwa 11 halafu mchezaji mmoja tayari alikuwa ameonyeshwa kadi nyekundu hivyo anahesabika kama sehemu ya mchezo huo. Kikanuni timu ilikuwa na wachezaji 12.

SAKATA linaloendelea sasa huko mtaani ni klabu ya Mbeya City kutumia wachezaji 12 kwa wakati mmoja kwenye mchezo dhidi ya Yanga juzi Jumapili.

Tunasema wachezaji 12 kwa maana kuwa uwanjani walikuwa 11 halafu mchezaji mmoja tayari alikuwa ameonyeshwa kadi nyekundu hivyo anahesabika kama sehemu ya mchezo huo. Kikanuni timu ilikuwa na wachezaji 12.

Japokuwa bado haijathibitika kuwa Mbeya City ilitumia wachezaji zaidi kwenye mchezo dhidi ya Yanga uliomalizika kwa sare ya bao 1-1, ipo haja ya uchunguzi wa kina kufanyika.

Bahati nzuri ni kwamba picha za video zipo na zinaweza kuthibitisha kuwa timu hiyo ilitumia mchezaji wa ziada ama la kwenye mchezo huo uliokuwa na presha kubwa huku ukiambatana na vurugu za hapa na pale kutoka kwa mashabiki.

Sheria namba tatu ya soka ya Shirikisho la Soka la Kimataifa (Fifa) iko wazi kuwa kila timu inapaswa kuwa na wachezaji 11 tu uwanjani na ikitokea timu imezidisha zipo hatua za kuchukuliwa.

Sheria hiyo inampa mamlaka Mwamuzi kumtoa mchezaji husika na kumwadhibu endapo amebaini kuwa aliingia kimakosa kwenye mchezo huo.

Pia, inampa mamlaka ya kuripoti tukio hiyo kwenye Kamati ya Mashindano endapo aling’amua baadaye wakati muda umeshakwenda.

Kanuni hii ni mama kwenye soka kote duniani lakini inatiwa zaidi nguvu na kanuni ndogo za mashindano katika nchi husika.

Mfano hapa kwetu zipo kanuni za uendeshaji wa Ligi Kuu Bara.

Kanuni hizo siyo kwamba zinaweza kupingana na ile ya Fifa, bali ni kutoa adhabu stahiki endapo tukio la kuzidisha mchezaji limetokea kwenye mchezo.

Kwenye hali ya kawaida, haitarajiwi kwa wakati wowote wa mchezo timu yoyote kuwa na wachezaji zaidi ya 11 ambao wanatakiwa kikanuni.

Kutokana na uzito wa Sheria hiyo namba tatu ya soka duniani, tunapenda kuishauri Bodi ya Ligi Kuu (TPLB) hasa Kamati ya Uendeshaji wa Ligi kuwa wanatakiwa kufanya uchunguzi wa kina ili kubaini kama Mbeya City walifanya hivyo ama la.

Uchunguzi huu ufanyike kwa uwazi na kushirikisha timu zote mbili ili maamuzi ambayo yatatolewa yawe ya haki na yenye manufaa kwa soka letu.

Ifahamike kuwa wakati mwingine kwenye soka uamuzi fulani hutolewa na kuonekana kama unaumiza timu moja lakini kwenye uhalisia ndio haki yenyewe.

Ikumbukwe kuwa mwaka juzi Mbeya City iliwahi kupewa alama za mezani baada ya Azam FC kumtumia mchezaji Erasto Nyoni ambaye kwa sasa yuko Simba akiwa na kadi tatu za njano.

Wakati wa mchezo huo haikufahamika mara moja kama Nyoni ana kadi tatu za njano lakini adhabu ilikuja kutolewa miezi miwili mbele wakati Azam ikipambana kuwania nafasi ya pili Ligi Kuu.

Adhabu kama hizi za kushtua huwa zinatokea hasa pale timu inapokuwa imefanya makosa bila kufahamu.

Kutokana na mazingira ya sakata hili, ni vyema Kamati ya Saa 72 ikautazama kwa kina mchezo huo na kubaini mbivu na mbichi na kutoa adhabu inayotajwa na Kanuni ama kuamua kwa utashi wao endapo Kanuni haizungumzii sakata hilo.

Kwa upande mwingine, tunapenda kuisisitiza Bodi ya Ligi na Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) kuendelea kutoa adhabu kali kwa timu ambazo mashabiki wake wanashindwa kuwa na uungwana mchezoni.

Tuliona kwenye mchezo huo wa juzi mashabiki wakirusha mawe kwenye goli la Yanga ambayo nusura yamjeruhi kipa wao, Youthe Rostand.

Tuliona Mwamuzi, Shomary Lawi na wasaidizi wake wakiwa bize kuokota mawe hayo na kuyaweka kama ushahidi juu ya vitendo hivyo vya utovu wa nidhamu.

Ifike mahala adhabu kama za kucheza mechi bila mashabiki na nyinginezo zikatolewa ili kutoa funzo zaidi kwa timu husika kuliko adhabu hizi za faini ambazo sasa zimeanza kuzoeleka.

Kilichofanywa na mashabiki wa Mbeya City ni kitendo cha kihuni na hakipaswi kuvumiliwa.

Tunadhani wakati umefika sasa kila mameneja wa viwanja vya Ligi Kuu kutengeneza uzio mrefu utakaowapa kazi mashabiki kufanya lolote kuelekea uwanjani.

Pia tunadhani polisi kufanya kazi yao kwa umakini, kuwanasa wale wote wanaoleta vurugu viwanjani.