Hii ndio mitihani ya Alliance

Muktasari:

  • Tayari Shirikisho la Soka la Tanzania (TFF) limeshatoa ratiba,ambapo kila klabu imeshajua nani wa kuanza naye na tunaamini kila timu inaendelea kujiandaa ili kutoshuka daraja.

MSIMU wa Ligi Kuu Tanzania Bara unatarajia kuanza Agosti 22 kwa timu 20 kuwasha moto kuwania ubingwa ili kuwakilisha nchi kwenye michuano ya Kimataifa.

Tayari Shirikisho la Soka la Tanzania (TFF) limeshatoa ratiba,ambapo kila klabu imeshajua nani wa kuanza naye na tunaamini kila timu inaendelea kujiandaa ili kutoshuka daraja.

Tulishuhudia msimu uliopita ambao ulizishirikisha timu 16, klabu za Njombe Mji na Majimaji zikishindwa kufurukuta na kujikuta zikishuka daraja na msimu ujao zitacheza la Kwanza.

Wakati tukisubiri kuona uwezo na kandanda safi kutoka kwa timu hizo zitakazochuana msimu ujao zikiwamo baadhi ambazo ni mara ya kwanza kuonja Ligi Kuu,ukweli unabaki palepale kwamba lazima pawepo za kushuka daraja.

Mwanaspoti inaangazia timu ya Alliance FC ambayo kwa mara ya kwanza inatarajia kuonja ladha ya Ligi Kuu na kukuletea baadhi ya mambo yanayoweza kuishusha haraka yasipofanyiwa kazi.

Ugeni wa Ligi

Moja ya timu changa au chipukizi na ngeni kwenye Mashindano haya makubwa ni Alliance FC yenye makazi yake Mtaa wa Mahina jijini Mwanza.

Ukifuatilia kwa undani timu nyingi zinazoanza Ligi kubwa huwa zinapata wakati mgumu sana kutokana na presha wanayokuwa nayo ikilinganishwa na timu zenye uzoefu.

Tulishuhudia kama Njombe Mji ambayo ilikuwa imepanda kwa mara ya kwanza iliweza kushuka haraka kabla hata ya Ligi kumalizika, hivyo na Alliance inaweza kushuka mapema.

Ukizingatia na mfumo mpya ulioanzishwa na Shirikisho la Soka nchini kwamba timu itakayoshika nafasi ya 17 na 18 zitashindanishwa na za Daraja la Kwanza nafasi ya pili na tatu kwa kila kundi,inaweza isiiache Alliance salama.

Uongozi

Timu hii ni ya mtu binafsi licha ya kwamba mmiliki wake,James Bwire anapambana lakini anaweza kukwama kutokana na kila kitu kusimamia yeye.Hana kikosi kazi anachoamini.

Bwire ni kiongozi wa Serikali ambaye ni Meya wa Jiji la Mwanza na ni Diwani wa Kata ya Mahina,hivyo majukumu hayo yanaweza kusababisha anakosa kufikia malengo kwenye timu yake.

Waswahili husema ‘Mshika mawili moja humponyoka’ ndicho kinaweza kumtokea Kigogo huyu kwani kutokana na majukumu aliyonayo (Siasa na Michezo) huenda moja wapo likakwama kati ya hayo.

Itafikia hatua anahitajika kwenye majukumu ya Chama huku timu yake ikipaswa kusafiri katika moja ya mechi muhimu hivyo kumpa wakati mgumu kufanya maamuzi.

Ni wazi kwamba hadi sasa Bwire hajawa na wasimamizi mbadala ambao akitoka wanaweza kuendesha timu bila tatizo kutokana na kwamba huduma zote za Taasisi yake humtegemea yeye.

Bwire ambaye ni Meneja wa timu,anaweza kusababisha hata wachezaji kukosa morari pindi atakapokosa kwenye mchezo kwani zile motisha wanazopata anapokuwapo kwenye Benchi la Ufundi zitakapokosekana.

Bado kiongozi huyo ni mtu anayetaka matokeo na hivyo iwapo Alliance itapoteza pengine mechi tano mfululizo anaweza kufanya maamuzi magumu na kuidhohofisha zaidi timu.

Ukimya kwenye timu

Hadi sasa Klabu hiyo iliyopanda Ligi Kuu suala la maandalizi ni kimya na hakuna taarifa mpya yoyote inayoeelezea hatua ilipofikia timu hiyo kuelekea michuano hiyo.

Mambo kama hayo yanaweza kuiathiri timu kutokana na wadau Jijini Mwanza au hata kwingine kukata tamaa kutokana na kuhisi kwamba haitaki kuingiliwa wala kushauriwa.

Bado timu hiyo inaweza kujikuta inakosa sapoti yoyote kutokana na mwenendo wake wa kujificha na kutotoa ushirikiano wowote na mwishowe kujikuta ikishuka Daraja na kufikia hatua ya kujilaumu wao.

Tunashuhudia kila siku usajili kwa baadhi ya timu zikiwamo kongwe zikiweka wazi zilio wasajili na kuelezea mikakati na mipango yao kuelekea msimu ujao wa Ligi Kuu,lakini kwa Alliance imekuwa tofauti.

Kujiamini

Timu hii ya vijana wadogo wanampira mzuri wa darasani,lakini kinachoweza kuwaangusha ni kujiamini kupitiliza kama walivyozoea kwenye mashindano ya Ligi Daraja la Kwanza.

Katika badhi ya mechi kwenye msimu uliopita,Alliance ilikuwa ikicheza kwa kujiamini kwamba inaweza kushinda,ambapo nyingine iliweza kupoteza kwa mfumo huo.

Mara kadhaa timu hii ilipokuwa ikipata mabao ilikuwa ikicheza kwa kuridhika,jambo ambalo linaweza kuiathiri kwenye Ligi Kuu wakikariri kama ilivyokuwa Daraja la Kwanza.

Ipo mechi moja ambayo walipoteza kizembe wakati wakicheza Daraja la Kwanza dhidi ya Trans Camp,vijana walionekana kudharau na kujiamini zaidi kwamba lazima washinde,lakini dakika 90 walilala bao 1-0 wakiwa uwanja wao wa Nyamagana.

Kukamia

Kama ilivyo kawaida ya timu zingine kukamia kwa baadhi ya mechi haswa Simba na Yanga,Alliance nao wanaweza kujikuta mtegoni kwa kukamia Klabu hizo kongwe nchini na kujutia.

Mara nyingi hata kama timu haina uwezo inapokutana na timu kati ya Simba au Yanga wachezaji hujiandaa kwa nguvu zote,huku wakisapotiwa na viongozi wao,hivyo kama itakamia baadhi ya mechi inaweza kuaga Ligi mapema.

Na niwazi kwamba kila mchezaji ndoto yake ni kuzichezea Simba na Yanga,hivyo hata Alliance wanaweza kuonyesha ubabe kwa kuzikamia timu hizo ili kusaka nafasi kwa vigogo hao wa Ligi Kuu.

Uhaba wa Mashabiki

Timu hii changa bado inakabiliwa na uhaba wa mashabiki ni tofauti na Mbao,Pamba na Toto Africans,ambazo zenyewe zina mtaji wa Wanachama na Mashabiki wa kutosha.

Klabu hii ina wanafunzi pekee ambao mara nyingi ndio hufurika uwanjani pindi timu hiyo inapokuwa inacheza,lakini si mashabiki wa kusema wanakuja kuiunga mkono Alliance.

Jambo hili litawaathiri Vijana hawa iwapo watakutana na timu zenye mashabiki na kujikuta wanakosa sapoti na mwishowe kukata tamaa na kupoteza mechi zake.

Lazima Uongozi ufanye mipango na mikakati ya kuhakikisha wanaandaa mashabiki sehemu mbalimbali za mikoani ili kuweza kupata sapoti kutokana na ugeni wao kwenye Ligi.