Hii Singida United isiposhtuka, imeumia

Muktasari:

  • Msimu huo, Mbeya City (MCC) ilishiriki Ligi Kuu kwa mara ya kwanza na kuleta ushindani mkali kwa timu zote ilizokutana nazo. Haikujalisha ilikutana na Simba ama Yanga, Mbeya City ilipambana na ilipata ushindi iwe nyumbani ama ugenini.

MSIMU wa 2013/14 ulikuwa ni wenye mageuzi kwenye soka nchini hasa Ligi Kuu Bara.

Msimu huo, Mbeya City (MCC) ilishiriki Ligi Kuu kwa mara ya kwanza na kuleta ushindani mkali kwa timu zote ilizokutana nazo. Haikujalisha ilikutana na Simba ama Yanga, Mbeya City ilipambana na ilipata ushindi iwe nyumbani ama ugenini.

Mbeya City ilitamba na kuanza kutoa ahadi kibao. Jezi yake ikawavutia mashabiki kibao. Ikawa na basi lake la maana. Ikajipanga kujenga uwanja wa kisasa Mbeya na mikakati kibao ambayo mingine imebakia kuwa stori.

Kwa msimu mmoja tu ilianza kuporomoka na hadi sasa imepoteza mwelekeo wake kabisa. Heshima iliyobaki Mbeya City ni kutokushuka daraja kwa kudura za Mwenyezi Mungu tu, vinginevyo ingekuwa inapigana vikumbo Ligi Daraja la Kwanza (FDL).

Wachezaji wake nyota wengi walikimbia baada ya timu kongwe za Simba na Yanga kuwalaghai kwa pesa na kuanza maisha mapya. Kikosi cha kwanza chote cha Mbeya City kiliondoka na hapo ndipo ulipokuwa mwanzo wa kuporomoka hadi sasa imebakiwa na wachezaji wasiozidi wawili walioipandisha Ligi Kuu. Wachezaji hao ni Hassan Mwasapili na John Kabanda.

SINGIDA UNITED SASA

Msimu wa 2018/19, Singida United ilianza kushiriki Ligi Kuu, ilifanya usajili kwa kishindo, ilitumia pesa nyingi kupata wachezaji bora ambao wamesaidia kumaliza ligi katika nafasi ya tano.

Ikiwa ni msimu mmoja pekee lakini ilionyesha dalili ambazo sio nzuri na inapaswa kuzifanyia kazi haraka ili isirudi nyuma kama ilivyo kwa Mbeya City iliyokuja moto na sasa inapoa taratibu.

Dalili za kuyumba zinaanza kunukia Singida United na kusababisha anguko la kutofanya vizuri kwenye ligi kadiri siku zinavyosonga.

HANS PLUIJM

Singida United ilimpa mkataba Kocha Mholanzi, Hans Pluijm ikiachana na kocha wake aliyeipandisha daraja, Fred Felix Minziro, ilishiriki Ligi Kuu (VPL) na Kombe la Mapinduzi.

Ilifanya vizuri japokuwa haikubahatika kutwaa ubingwa. Ghafla, Pluijm amepata dili la maana la kuifundisha Azam FC na hivyo kuachana na Singida United ambayo sasa inafundishwa na Hemed Morocco.

Pluijm alikuwa na mfumo wake na uliisaidia timu kufanya vizuri ingawa malengo yake ya kwanza ya kutwaa ubingwa wa VPL ulifeli.

Kitu pekee ambacho Pluijm alifanikiwa na kuiacha Singida United kama alama ya mafanikio ni kuifikisha fainali ya Azam Sports Confederation Cup (Kombe la FA) na ilicheza na Mtibwa Sugar iliyochukua ubingwa huo.

Pia, aliiwezesha timu hiyo kuwa kwenye tano bora ya VPL.

Kuletwa kwa Morocco aliyeanza kuifundisha timu kwenye mashindano ya SportPesa pamoja na Klabu Bingwa Afrika Mashariki (Kombe la Kagame), mashindano yote hayo hakufanya vizuri sana. Ilitolewa katika hatua ya robo fainali katika mashindano yote.

Kazi kubwa ya Morocco ni kuhakikisha timu hiyo inafanya vizuri na kurudisha imani kwa mashabiki wake kama msimu uliopita ambapo ilianza kwa kutikisa.

USAJILI WA KUKURUPUKA

Tatizo kubwa la uongozi wa Singida United ni kama vile haukujipanga na kuwa na malengo na usajili.

Viongozi kwa kushirikiana na kocha bado hawajaangalia nafasi za kuziboresha kikosi ndio maana msimu uliopita ilisajili wachezaji 11 wa kigeni ikiwa ni sawa na kikosi kizima cha kwanza na baadaye ilianza kuwapeleka wengine kwa mkopo katika timu nyingine.

Sasa hivi usajili unaendelea lakini nyota saba waliokuwa kikosi cha kwanza wametimka ambao ni washambuliaji Danny Usengimana na Nhivi Simbarashe, beki, Michael Rushengonga, winga, Kiggi Makasi na Deus Kaseke, viungo Tafadzwa Kutinyu na Mudathir Yahya.

Wachezaji wengine wa kigeni waliosajiliwa dirisha kubwa na dogo ni Wisdom Mtasa aliyetolewa kwa mkopo Stand United, Shaffiq Batambuze, Elisha Muroiwa, Gentil Kambale (DR Congo), Antil Marik (Ghana), Lubinda Mundia (Zambia) na Michelle Katsvairo.

Usajili huu haukuwa na malengo ya kuzingatia vipaji vya Mkoa wa Singida na nchi kwa jumla. Unaweza kusema pia kuwa, haukuwa usajili wenye tija kwa klabu pamoja na kuwa wa kifahari sana.

Pluijm ameondoka na wachezaji wawili kwenda Azam FC ambao ni Kutinyu na Mudathir huku Kaseke akitajwa kurejea Yanga, Makassi aliomba kuvunja mkataba akajaribu sehemu nyingine baada ya kushindwa kutimiziwa makubaliano ya mkataba wake.

UONGOZI SIO SHIRIKISHI

Uongozi wa Singida United hadi sasa sio rafiki kwa baadhi yao baada ya baadhi ya viongozi kutokuwa na nguvu hasa upande wa Katibu Mkuu ambaye ndiye mtendaji wa klabu.

Majukumu mengi hufanywa na mtu mmoja ambaye hushikiria nafasi zote, mtu mmoja hufanya kazi za Mkurugenzi wa timu, Katibu Mkuu, Afisa Habari, Mwenyekiti wa Kamati ya Usajili.

Singida United inapaswa kugawa madaraka kwa viongozi wengine ama kuunda kamati ili kila mmoja afanye majukumu yake, vinginevyo itajimaliza yenyewe.

MATUMIZI MABAYA YA FEDHA

Singida United ni timu ambayo haina njaa ya pesa. Haijawahi kulia ukata tangu ianze kushiriki ligi. Ni timu ambayo ina wadhamini wengi kati ya timu zote za Ligi Kuu hapa nchini. Lakini matumizi yake yamekuwa makubwa pasipo sababu za msingi. Mfano wa matumizi mabaya ni kuigawa timu katika makundi ili kuweka kambi wakati wa maandalizi ya fainali za Kombe la FA, haikuwa na sababu ya kufanya hivyo.

WAGENI NI BORA KULIKO WAZAWA

Inawezekana ni kawaida kwa klabu kutoa huduma bora kwa wachezaji wa kigeni na kuwadharau wazawa.

Inaelezwa ndani ya Singida United kuna malezi ya makundi mawili. Wazawa na wa kigeni. Huduma ni tofauti kabisa, wageni hupewa huduma bora tangu wanapoingia ukilinganisha na wazawa ambao wanawekwa sehemu moja.

Wageni hupewa nyumba ambazo zina kila kitu ndani. Na kila nyumba huishi wachezaji wawili tofauti na wazawa ambao kwa nyumba moja huishi zaidi ya wachezaji watatu na ni nyumba ambazo hazina ubora kama nyumba za wachezaji wa kigeni jambo ambalo huleta mpasuka kwa wachezaji.

Bado Singida United inaweza kuwa timu ya maana inaweza isipotee katika ramani ya soka la Tanzania kama itasahihisha makosa yake.