Hebu cheki Diamond anavyofukuzia anga za Mo Salah huko Insta

Muktasari:

Hata hivyo, hayupo pekee yake na hii ndio orodha ya watu maarufu wanasoka na wanamuziki wanaoongoza kwa kuwa na wafuasi wengi huko Insta.

SUPASTAA wa Liverpool na timu ya taifa ya Misri, Mohamed Salah ndiye mwanasoka wa Afrika mwenye wafuasi wengi zaidi kwenye mitandao ya kijamii, kwa mujibu wa ripoti iliyotolewa na African Social Media Power. Staa huyo ndiye mwafrika mwenye wafuasi wengi kwenye mtandao wa Instagram.

Hata hivyo, hayupo pekee yake na hii ndio orodha ya watu maarufu wanasoka na wanamuziki wanaoongoza kwa kuwa na wafuasi wengi huko Insta.

7.Diamond Platnumz - 4.9 milioni

Supastaa Diamond Platnumz ni mkali wa Tanzania kwenye muziki wa Bongo Fleva. Ametamba na nyimbo zake nyingi ikiwamo wa “Ukimwona” na nyingine nyingi alizoshirikiana na mastaa wengine mahiri akiwamo Omarion wa Marekani. Kwenye Insta ana wafuasi 4.9 milioni.

6.Tiwa Savage -5 milioni

Tiwa Savage ni mwimbaji wa Kinigeria, mburudishaji na pia ni mwigizaji. Kwa sasa yupo kwenye dili matata kabisa na Sony/ATV Music Publishing. Umaarufu wake umemfanya kuwa miongoni mwa watu wenye wafuasi wengi kwenye Insta kwa upande wa Afrika, akiwa na wafuasi 5 milioni. Nyimbo zake anaimba kwa lugha ya Kingereza na Yoruba.

5.Wizkid -5.5 milioni

Wizkid ni mwimbaji na mtunzi kutoka Nigeria. Anashika namba tano kwenye chati za Forbes na Channel O’s kwa mwaka 2013 kwenye orodha ya wasanii wa Kiafrika matajiri. Mwaka 2014, Wizkid alikuwa mwanamuziki wa kwanza wa Nigeria kuwa na wafuasi zaidi ya 1 milioni kwenye Twitter. Ameingia pia kwenye rekodi za Guinness na wimbo wake aliofanya na Drake wa “One Dance”. Ana wafuasi 5.5 milioni kwenye Instagram.

4.Didier Drogba -6.3 milioni

Baada ya kudumu kwa miaka minane kwenye kikosi cha Chelsea na kufunga mabao 157 katika mechi 341 alizocheza hapo na kuisaidia timu hiyo kubeba mataji 10 ikiwamo la Ligi ya Mabingwa Ulaya mwaka 2012, straika huyo wa Ivory Coast haihitaji maelezo marefu kumtambulisha. Drogba anajulikana na kila mtu, pengine hata wale wasiokuwa mashabiki wa mpira. Umaarufu huo umemfanya Drogba kuwa na wafuasi wapatao 6.3 milioni kwenye mtandao wa Instagram.

3.Davido Adeleke -7 milioni

David Adedeji Adeleke ni mwimbaji wa Kinigeria, mtunzi na mtayarishaji wa nyimbo. Wimbo wake aliotoa mwaka 2011 uliokwenda kwa jina la “Dami Duro” ulipokewa vizuri kwelikweli huko Nigeria na sehemu nyingi za Afrika. Kwa kushirikiana na kaka yake, Adewale Adeleke, Davido anamiliki kampuni ya HKN Music. Amewahi kutayarisha nyimbo za wasanii Naeto C, Skales, Tiwa Savage na Sauce Kid. Umaarufu wake umemfanya kujikusajia wafuasi 7 milioni kwenye mtandao wa kijamii wa Insta.

2.Pierre-Emerick Aubameyang -7.2 milioni

Pierre-Emerick Aubameyang ameingia kwenye rekodi za kuwa mchezaji ghali kwenye kikosi cha Arsenal wakati aliponaswa na timu hiyo akitokea Borussia Dortmund katika dirisha la Januari. Ndani ya uwanja, Aubameyang anafahamika kwa kasi yake anapokuwa na mpira na kuwakwepa mabeki na kusukumia mipira wavuni. Lakini, nje ya uwanja staa huyo wa Gabon ni maarufu sana kwa magari ya kifahari. Mambo hayo kwa pamoja yamemfanya kuwa na wafuasi wengi kwenye mtandao wa kijamii hasa ule wa Insta.

1.Mohamed Salah - 18.3 milioni

Mo Salah, ndiye Mwanasoka Bora wa Mwaka wa Afrika, ndiye Mchezaji Bora wa Mwaka wa Ligi Kuu England. Ndiye mwanasoka anayeongoza kwenye orodha hii baada ya kuwa na wafuasi 18 milioni. Umaarufu wake umeongezeka zaidi kwa msimu uliopita tu kutokana na kile alichokuwa akikifanya huko Liverpool kiasi cha kumfanya hata achaguliwe kwenye uchaguzi wa siasa huko kwao Misri bila hata kuwa mgombea.

Mo Salah ni mchezaji maarufu kweli kweli kwa sasa Afrika na duniani kwa ujumla ndio maana amekuwa na wafuasi 18.3 milioni kwenye Insta.