Hawa hawatajenga Mbagala kwetu

Muktasari:

  • Kwa bahati mbaya wengi wanashindwa kutazama suala la ongezeko hilo kwa upande wa matokeo ya nje ya uwanja ambayo nchi na soka letu tutayapata kupitia wageni hao.

MIJADALA mingi inayoendelea juu ya uamuzi wa Shirikisho la Mpira wa Miguu la Tanzania (TFF) kuongeza idadi ya wachezaji wa kigeni kutoka saba hadi kumi, imegusa zaidi faida na hasara za uwanjani.

Kwa bahati mbaya wengi wanashindwa kutazama suala la ongezeko hilo kwa upande wa matokeo ya nje ya uwanja ambayo nchi na soka letu tutayapata kupitia wageni hao.

Kabla ya kuruhusu ongezeko la wachezaji wa kigeni, ni vyema vigogo tuliowapa dhamana ya kusimamiasoka letu, wangetazama upande wa pili wa faida gani na hasara gani ambazo nchi itazipata.

Kwa nchi, ongezeko la wachezaji wa kigeni halina manufaa zaidi ya kuleta hasara ambayo inahitaji jicho la tatu kuigundua. Unapoongeza idadi ya wachezaji wa kigeni maana yake unapunguza fursa ya wazawa kuajiriwa, hilo linapotokea maana yake unapunguza kiasi cha fedha ambacho kingewekezwa ndani na kukipeleka nje ya nchi.

Ukiondoa tozo ya kodi ya kile mtu anacholipwa (PAYE) pamoja na tozo isiyo rasmi kutokana na manunuzi ya bidhaa ambayo mchezaji husika wa kigeni angefanya, maana yake fungu kubwa la fedha atapeleka na kwenda kuliwekeza kwao.

Klabu zitalazimika kuwalipa mishahara wachezaji hao kwa Dola tofauti na wazawa ambao hulipwa kwa Shilingi. Fedha ambayo mchezaji wa kizawa anaipata maana yake yote itaingia kwenye mzunguko wa ndani na hivyo kupandisha thamani ya shilingi yetu.

Kwa kuruhusu ongezeko la wachezaji wa kigeni, maana yake TFF inabariki na kusaidia fungu kubwa la fedha yetu kuondoka kwenye mzunguko wa ndani na kwenda kuwekezwa nje ya nchi.

Tunapoona Ligi Kuu kubwa duniani zimejaza wachezaji wa kigeni, kabla ya kuruhusu hilo, waliandaa kanuni ambazo zinasaidia nchi hizo kuchota kiasi kikubwa cha fedha kutoka kwa wachezaji hao wa kigeni, ni tofauti na hapa kwetu.

Kwenye Ligi Kuu England kwa mfano, mchezaji wa kigeni analazimika kulipa asilimia 48 ya mshahara anaolipwa huku pia akikatwa asilimia 2 ya pato lake ambayo huenda katika mfuko wa taifa wa bima ya afya.

Kodi hii ni tofauti na ile anayokatwa mchezaji mzawa ambapo hutozwa chini ya asilimia 30. Ni kama ilivyo kwa Hispania ambako mchezaji wa kigeni hulazimika kulipa asilimia 50 ya pato lake la mshahara huku wazawa wakiwa na unafuu.

Nchi hizi zimetambua kwamba fedha anayolipwa mzawa inaendelea kubakia ndani tofauti na ile anayopata mgeni inayokwenda nchi nyingine.

Sawa kuna uwezekano klabu zetu zikanufaika ndani ya uwanja kutokana na ongezeko la wageni, lakini pengine kabla ya hapo kungewekwa angalau na kanuni ya kutoza kodi kubwa kwa hao wachezaji wa kigeni ili kufidia sehemu ya fedha ambayo serikali itapoteza kwa wao kutofanya uwekezaji nchini.

Pengine tumejisahau kwamba hawa akina John Bocco na wachezaji wengine wazawa, fedha watakayoipata itabakia hapa na itanufaisha nchi. Fedha hiyo italipa mafundi wa Kitanzania na itanunua vifaa vya ujenzi kwa ajili ya kujengea nyumba zao ambazo baadaye watazilipia kodi ya majengo.

Watatumia fedha hizo kuanzisha biashara ambazo watalazimika kuajiri Watanzania wenzao pamoja na kulipa kodi ya moja kwa moja na ile isiyo ya moja kwa moja pamoja tofauti na itakavyokuwa kwa wachezaji wa kigeni.

Tunaweza kufurahia ubora wa akina Emmanuel Okwi, Papy Tshishimbi, Donald Ngoma, Thabani Kamusoko na James Kotei, lakini katu tusitegemee wawekeze hapa nchini kama akina Kelvin Yondani, Nadir Haroub ‘Cannavaro’ na Shiza Kichuya walivyofanya Kigamboni, Mbagala na Morogoro. Wao fedha zao wataenda kuziwekeza Ghana, Uganda, Zimbabwe na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo.