Hapa kwa Bale! inaweza kula kwako tu

Muktasari:

Unaambiwa staa huyo anatia hasara tu kwani, katika mechi 60 za mwisho ilizocheza Real Madrid, yeye amekosa mechi 40.

MADRID, HISPANIA. WANASEMA ukienda na pesa zako kumnunua Gareth Bale kwa sasa, basi ujue utauziwa mbuzi kwenye gunia. Unaambiwa staa huyo anatia hasara tu kwani, katika mechi 60 za mwisho ilizocheza Real Madrid, yeye amekosa mechi 40.

Bale amekuwa majeruhi mara 11 katika kipindi chake alichokuwa kwenye kikosi cha Real Madrid, amekuwa akiumia mara kwa mara na hata hivi karibuni akiwa kwenye mazoezi ya kujiweka fiti, aliumia tena misuli ya nyuma ya paja. Haya hapa majeruhi yanayomsumbua Bale na mechi alizozikosa.

Okt 3 – 17, 2013 (paja, mechi mbili)

Akiwa hana siku nyingi kwenye kikosi cha Real Madrid, Bale alikumbwa na maumivu ya paja ambayo yalimweka nje ya uwanja kwa siku 14, kuanzia Oktoba 3 hadi Oktoba 17, 2013. Majeraha hayo yalimfanya Bale akose mechi mbili katika kikosi hicho cha Real Madrid.

Okt 20 – 30, 2014 (misuli, mechi tatu)

Oktoba nyingine ya mwaka uliofuatia, Bale aliingia tena kwenye benchi la wagonjwa kwenye kikosi hicho cha Santiago Bernabeu. Safari hii staa huyo alikumbwa na maumivu ya misuli ya nyuma ya paja, ambapo alikaa nje ya uwanja kuanzia Oktoba 20 hadi 30, 2014 na hivyo kukosa mechi tatu.

Sept 17 – 28, 2015 (kigimbi, mechi tatu)

Miezi ya majeruhi ya Bale inaonekana kuwa ni ile ile, safari hii, staa huyo wa Wales alipata majeraha ya kigimbi na kuwa nje kuanzia Septemba 17 hadi 28, 2015. Maumivu hayo yalimfanya Bale kuwa nje ya uwanja kwa siku zote hizo 11 na kujikuta akishindwa kuichezea Real Madrid mechi tatu.

Okt 19 – Nov 5, 2015 (kigimbi, mechi nne)

Baada ya kurudi uwanjani tu, Bale hakudumu sana akarudi tena kwenye wodi ya wagonjwa katika kikosi hicho cha Bernabeu huku miezi yake ikiwa ile ile ya kuumia baada ya kusumbuliwa tena na maumivu ya kigimbi kuanzia Oktoba 19 hadi Novemba 5, 2015. Maumini hayo yalimfanya Bale akose mechi nne katika kikosi cha Madrid.

Januari 18 – Machi 3, 2016 (kigimbi, mechi nane)

Haya yalikuwa maumivu ya muda mrefu kidogo, lakini kubwa yaliendelea kuwa yale yale ya kuumwa misuli ya kigimbi. Safari hii, Bale alikaa nje ya uwanja kuanzia Januari 18, 2016 hadi Machi 3, mwaka huo huo na kumfanya akose mechi nane za Real Madrid, timu ambayo ilitumia pesa nyingi kumnasa alipotokea Tottenham Hotspur.

Sept 15 – 22, 2016 (nyonga, mechi mbili)

Mwili wa Bale una maumivu karibu kila sehemu. Septemba 15 hadi Septemba 22, 2016 aliingia tena kwenye benchi la wagonjwa kwenye kikosi cha Real Madrid baada ya kupata maumivu tofauti wakati aliposumbuliwa na nyonga. Maumivu hayo ya siku saba yalimfanya Bale akose mechi mbili.

Novemba 24, 2016 – Februari 16, 2017 (enka, mechi 17)

Hiki ni kipindi ambacho hata Real Madrid wenyewe imani iliwashinda na kufikiria mpango wa kumpiga bei staa huyo. Bale alikuwa nje ya uwanja akisumbuliwa na maumivu ya enka kuanzia Novemba 24, 2016 hadi Februari 16, mwaka huu, na kipindi hicho alichokuwa nje ya uwanja staa huyo alikosa mechi 17 za kuitumikia timu yake.

Aprili 13 – 20, 2017 (kigimbi, mechi mbili)

Akirejea uwanjani baada ya kutoka kuuguza maumivu ya enka, Bale alirudi tena kwenye benchi la wagonjwa baada ya kupata maumivu ya kigimbi Aprili 13, 2017 ambayo yalimweka nje ya uwanja hadi Aprili 20 na hivyo kukosa mechi mbili katika kikosi hicho chenye maskani yake huko Bernabeu.

Aprili 24 – Juni 1, 2017 (Kigimbi, mechi nane)

Siku nne tangu alipotangazwa kwamba amepona, Bale alirejea tena kwenye benchi la wagonjwa katika kikosi cha Real Madrid, akiendelea kusumbuliwa na tatizo lile lile la maumivu ya kigimbi. Bale alipata maumivu hayo Aprili 24 na kukaa nje ya uwanja hadi Juni Mosi, mwaka huu na kumfanya kwa kipindi hicho kukosa mechi nane za Real Madrid.

Sept 27 – Novemba 6, 2017 (kigimbi, mechi nane)

Mwaka wa shida kwa Bale. Staa huyo ameonekana kusumbuliwa mara nyingi zaidi na maumivu ya kigimbi, ambapo yalimfanya awe nje ya uwanja kwa siku kibao na kushuhudia akikosa mechi nane za kuitumikia timu yake ya Real Madrid iliyomsajili kwa Pauni 85 milioni mwaka 2013.