Guardiola awatia nguvu Bayern kuichapa Madrid

TOLEO lililopita kwenye Kitabu cha Pep Confidential, Mwandishi Marti Perarnau alizungumzia maandalizi ya Bayern Munich kuumana na Real Madrid yalivyopamba moto huyu Kocha Pep Guardiola akiwa aliyetatizwa na wachezaji wake wa kikosi chake cha kwanza huku akipewa taarifa za mmoja wa wachezaji wake kufiwa na baba yake mzazi. Endelea…

Kabla ya kuondoka Munich akapata habari baba wa mmoja wa wachezaji wake, Hojbjerg alifariki dunia, katika timu iliyosafiri kuelekea Madrid Alaba pia alikuwa akijisikia kuumwaumwa, Neuer alikuwa na tatizo la mgongo na Gotze hakuwa katika ubora wake.

Kama vile kuongeza tatizo juu ya tatizo, Javi Martinez ambaye angeanza kikosi cha kwanza alikuwa na ugonjwa ambao ulimfanya si tu asiwe katika ubora wake, bali pia alipoteza takriban kilo nne katika kipindi cha wiki moja.

Nje ya hilo hapana shaka wachezaji walikimbia kiasi cha kutosha katika mechi mbili tangu Aprili 14 na kilichoonekana ni kama vile mzuka wa mechi zilizopita waliupa kisogo.

Ukiachana na yote hayo, Bayern walikuwa pale walipodhamiria kufika, wakiwa tayari wana mataji matatu ya msimu uliopita huku na tayari wakiwa na la ligi la msimu uliofuata na kwenye Kombe la Ujerumani wamefikia hatua ya fainali huku kwenye ligi ya mabingwa wakiwa na dakika 180 za kufikia fainali yaani mechi mbili.

Pep aliamua kuikabili Real Madrid kwa ujasiri, akiwa na kumbukumbu ya kupata ushindi dhidi yao wakati akiwa na Barcelona kwenye uwanja huo huo wa Madrid ingawa kwa wakati wote amekuwa akiiheshimu, kwake Madrid wamekuwa ni wapinzani wakuu tangu akiwa mchezaji na hadi baadaye alipokuwa kocha.

Pamoja na matatizo yote yaliyokuwa yakiikabili Bayern, Pep bado alikuwa katika utayari wa hali ya juu kuikabili Real Madrid kwa kujiamini na kujivunia timu yake.

“Tumefanya juhudi kubwa mno hadi kufika hapo,” aliniambia na kuna wakati tumefanya hivyo kwa kufanya kazi kubwa mno tukiwa katika mazingira magumu, kikosi changu kimekuwa vizuri katika wiki tatu za msimu huu, ni wiki tatu tu na hapo tumefanya kazi mfano wa mbwa.

“Hakuna cha kukata tamaa kwa sasa tunatakiwa kuingia uwanjani tukiwa wenye kufurahia tukio hili, hakika niko tayari nawasubiri, tutakwenda uwanjani tukijaribu kuwapora mipira, tunatoka na mipira nyuma na kutawala mchezo kwenye Uwanja wa Bernabeu,’’ alisema Pep.

Na hivyo ndivyo ilivyokuwa hatimaye Bayern ilitawala mchezo, katika dakika 15 za kwanza ilitawala kwa asilimia 80, huku sehemu kubwa ya kutawala huko kukiwa katika eneo la Real Madrid.

Katika mazingira hayo, Schweinsteiger aliunasa mpira wa kichwa na kupiga vizuri lakini kipa Iker Casillas alikuwa makini na kuokoa, kabla ya Robben kufumua shuti jingine ambalo lilikwenda nje.

Baada ya hapo Kroos akafumua shuti lililompita Pepe na mpira kumgonga Benzema, hakuna mchezaji wa Bayern aliyekuwa makini kukaba, dakika 19 baadaye Neuer alijikuta akiuchungulia mpira ulioingia ndani ya nyavu za Bayern. Benzema aliyeanzisha shambulizi hilo kwa pasi ya Fabio Coentrao iliyoanzia katikati, ndiye aliyemtungua akiwa karibu kabisa na lango la Bayern.

Hii ni timu iliyochoka sana ambayo ilifanya kazi kubwa ikiwa nyumbani, ilimiliki mpira, ilionyesha ubora lakini ikajikuta ikifungwa katika mazingira yaliyoonyesha jinsi mpira wa awali ulivyoanzia kwenye lango la wapinzani wao na kuzaa bao.

Katika dakika sita za mwisho Bayern ililisakama lango la Madrid ingawa Madrid nayo ilijibu mapigo kwa kupata nafasi mbili ikiwamo moja ambayo Cristiano Ronaldo alishindwa kuitumia.

Bayern iliwasumbua Madrid kwa maana ya kumiliki mpira kwa muda mrefu hadi dakika ya mwisho ya kipindi cha kwanza Madrid ilipofumania nafasi ambayo Angel di Maria alijikuta akiwa uso kwa uso na Neuer lakini shuti lake lilipaa.

Madrid katika kipindi cha kwanza iliandamwa mno na kuruhusu kona tisa katika lango lakini bado ilifanikiwa kudhibiti juhudi za Bayern kupata bao, kwa ufupi timu ya Pep ilitawala mchezo lakini haikuwa na nafasi ya kumzidi ujanja Casillas.

Itaendelea Jumamosi ijayo…