HISIA ZANGU: Guardiola angekuwa kocha Yanga, angeliogopa kundi lake

Muktasari:

Kauli ya kwanza tu baada ya kuzifahamu timu ambazo wamepangwa nazo katika mechi za makundi za Kombe la Shirikisho Afrika. Unaishia kutabasamu na kisha kucheka.

YANGA wanakwambia wamepangwa katika kundi rahisi.

Kauli ya kwanza tu baada ya kuzifahamu timu ambazo wamepangwa nazo katika mechi za makundi za Kombe la Shirikisho Afrika. Unaishia kutabasamu na kisha kucheka.

Wamepangwa na Rayon Sports ya Rwanda, USM Algers ya Algeria na Gor Mahia ya Kenya. Sijui wanatumia vigezo gani kusema kwamba kundi lao ni rahisi. Labda kwa sababu wamepangwa na majirani zao kwahiyo wanaleta kujuana.

Kuna mambo matatu. Kwanza kabisa Watanzania hatuna heshima na mpira. Laiti kama tungekuwa na mipango halafu tukawa katika viwango vya juu, si ajabu kuna wachezaji au mashabiki ambao wangeingia uwanjani wakiwa uchi kwa dharau.

Ukisikiliza mahojiano ya Arsene Wenger au Sir Alex Ferguson, au Pep Guardiola anayetamba kwa sasa pale Ulaya angekwambia Yanga ipo katika kundi gumu. Anapokuwa kule Ulaya Guardiola akipangwa na timu lenye kundi dhaifu kama Romania, Sweden na Poland bado angesema kundi lake gumu.

Kwanini angesema kundi lake ni gumu? Kwa sababu kwanza hafahamu ubora au udhaifu wa timu anazocheza nazo.

Anafahamu ubora na udhaifu wa Manchester United, Arsenal, Chelsea, Real Madrid, Liverpool na nyinginezo lakini si timu kutoka Poland.

Lakini hapo hapo ukiheshimu wapinzani wako unajiweka katika mazingira mazuri ya kupunguza munkari wa wapinzani wako. Ukiwadharau wapinzani wako, basi wanakuja na hasira za kukuumbua moja kwa moja.

Yanga wanadai kwamba kundi lao ni jepesi lakini hakuna mtu yeyote katika benchi lao la ufundi ambaye anawajua Rayon, USM na Gor Mahia walivyo sasa.

Wanasema tu kwamba kundi lao ni rahisi bila ya kutupatia vigezo vyovyote.

Mbaya zaidi, wanaweza kuanza mechi hizi bila ya kutuma watu wao kwenda Algeria, Rwanda au Kenya kutazama ubora na mapungufu ya wapinzani wao. Bado watatuambia kwamba wapo katika kundi jepesi kwa hisia hisia tu za mtaani.

Lakini hapo hapo unawaza, Yanga wanasema wapo katika kundi rahisi, ni kwa timu gani waliyonayo? Mara kadhaa nawakumbusha jinsi timu yao ilivyomomonyoka kuanzia kipindi cha miezi 24 iliyopita. Bado wanajisahau na kujiona wana timu ileile ambayo ilikaribia kuitoa Al Ahly ugenini. Wanasahau wana timu nyingine kabisa.

Haruna Niyonzima, Vincent Bossou, Simon Msuva wote hawapo kutoka katika Yanga ile imara. Thaban Kamusoko anasuasua, Donald Ngoma (pichani) ni kama vile amegoma kucheza. Hii ni nusu ya timu imara ambayo walikuwa nayo miezi 24 iliyopita. Hapo hujamhesabia Amissi Tambwe.

Wanachojisahau Yanga ni kwamba kama wangekuwa na kikosi hiki imara si ajabu wangewatupa nje Township Rollers na sasa hivi wangekuwa bado wapo katika michuano ya Ligi ya Mabingwa Afrika.

Hata hivyo mwanadamu ana tabia ya kujisahau.

Lakini nje ya hapo ni wakati wa kulitazama soka letu upya. Unapopangwa na timu kutoka Rwanda, Kenya na Algeria ni nchi gani kati ya hizo imepitwa sana kisoka na Tanzania? Wajiulize timu zao za taifa zinafanya nini na sisi tunafanya nini?

Hapo hapo jaribu kujikumbusha jinsi ambavyo miaka michache nyuma Yanga ilipopangwa kundi moja na timu za Medeama, TP Mazembe na MO Bajaia halafu wakasema wapo katika kundi rahisi. Waliishia kushika mkia huko chini. Walishangilia kupangwa na timu kutoka Ghana, DR Congo na Algeria halafu bado wakadai kwamba kundi ni rahisi.

Kocha wao, Mzambia, George Lwandamina ameikimbia timu kwa sababu ya matatizo.

Halafu juu ya yote haya, Yanga wanaambizana kwamba wapo katika kundi rahisi huku wakiwa wanaogelea katika mto wa tabu. Wachezaji hawalipwi kwa wakati, pamoja na shida nyingine kibao lakini bado wanakwambia wapo katika kundi rahisi. Kundi rahisi kivipi?

Yanga wanatakiwa kujipanga na kujua shida zao kwanza kabla ya kulihukumu kundi lao kuwa ni jepesi.