NINACHOKIAMINI: Eti Chalenji! Ndio michuano gani, kwani inafanyika wapi?

Muktasari:

Ushindani huu umewafanya watu kupoteza utu na badala yake fedha inaonekana ndio msingi wa maendeleo. Katika dunia ya sasa hilo halikwepeki.

KATIKA dunia ya kibepari tunayoishi, maisha si lele mama. Ushindani wa maisha umekuwa mkubwa kiasi kwamba utu unapotea miongoni mwa watu.

Ushindani huu umewafanya watu kupoteza utu na badala yake fedha inaonekana ndio msingi wa maendeleo. Katika dunia ya sasa hilo halikwepeki.

Ubepari umeifanya dunia ikimbie kwa kasi, watu wanakimbia na teknolojia inakimbia zaidi kuliko kitu kingine chochote.Huwezi kubishana na hali halisi inayoendelea sasa.

Na ili kwenda sambamba na hali hiyo ubunifu umekuwa mkubwa kiasi kwamba watu wanataka kuona bidhaa mpya kila siku.

Tumeshuhudia hilo katika makampuni ya simu; yanazalisha matoleo ya aina tofauti kila siku, na kila toleo linakuwa na teknolojia mpya na nzuri kuliko iliyopita.

Wafanyabiashara wamejikuta wakiwa na hali ngumu zaidi, kwani wanatakiwa kushindana na kuhakikisha bidhaa zao zinapata soko. Lakini soko lenyewe linataka bidhaa mpya kila siku.

Ili kupambana na hali hiyo, njia pekee ambayo inaonekana kufanya vizuri ili kupata soko ni mhusika kuwa mbunifu. Soko linataka kuona vitu vizuri, tena vyenye utofauti na jana.

Kwa bahati mbaya, hakuna bidhaa ambayo imeachwa salama, zote zimeingia kwenye ushindani na zote zinatakiwa ziwe katika ubunifu wa hali ya juu ili zikubalike.

Tunaona jinsi Ligi Kuu England inavyobadika kila msimu. Tunaangalia jinsi wachambuzi kwenye televisheni zao wanavyobadilika na hata jinsi wanavyobadilisha studio zao ili kuvutia watazamaji.

Na hilo linafanya ligi hiyo isichoshe hata kidogo kwa sababu ina ubunifu mkubwa ambao unamfanya mtazamaji atamani kuangalia tena na tena.

Umaarufu wa ligi hiyo duniani unatokana na ubunifu wa klabu, bodi ya ligi, televisheni na matangazo yao kwa jumla.

Watu wengi wanatamani wikiendi ziwe zinafika haraka ili waone mechi za Ligi Kuu England. Zina mvuto kwanini usiwe na hamu nayo?

Na ndio maana si ajabu kuona viwanja vyote vinajaza mashabiki kwa sababu bidhaa inavutia na inamfanya mteja ajione hajaibiwa licha ya kiingilio kuwa kikubwa.

Ukiangalia hapo jirani Kenya ambako kuna michuano ya Kombe la Chalenji hakuna kinachoendelea. Hakuna mashabiki uwanjani, michuano haina mvuto, kila kitu kimedorora.

Itavutia vipi wakati kila mwaka ratiba ni ileile, timu zilezile, porojo zilezile na mbaya zaidi hakuna ubunifu hata kidogo.

Makocha wengi wababaishaji, hawajui kuchambua mpira, hawajui falsafa zao, hawana dira wala hawajui wana malengo gani?

Waite makocha hao walio na timu za taifa katika michuano ya Chalenji halafu waulize malengo yao katika timu, dira na falsafa zao.

Hutapata majibu badala yake utaishia kuambiwa kuwa unawachokonoa kutokana na chuki binafsi. Hawapendi kuguswa.

Viongozi wa soka la Cecafa badala ya kutoka nje na kuangalia mambo yanavyoendelea, wamebaki wamejifungia tu ndani, hawajui wanachokifanya.

Na ndio maana michuano yenyewe haina mvuto, watu hawaendi uwanjani. Huwezi kulaumu watu hawa kwa sababu wanataka vitu vipya na vyenye ubunifu.

Unaweza kuwauliza watu michuano hiyo mwaka huu inafanyika wapi na wasijue kwa sababu imepoteza mvuto.