JICHO LA MWEWE: Cheki maisha yanavyokwenda kasi kwa Chirwa

Muktasari:

  • Inaonekana labda kuna kitu kilikuwa kinamsumbua Chirwa. Labda hali ya hewa ilikuwa inamsumbua. Labda chakula kilikuwa kinamsumbua. 

MAISHA yanakwenda kasi kwa Obrey Chirwa. Inashangaza sana. Namkumbuka Chirwa aliyekosa mabao mengi ya wazi katika pambano dhidi ya Mo Bejai. Ilikuwa ni mechi ya makundi michuano ya Kombe la Shirikisho.

Watu wa Yanga wakaanza kujiuliza walikuwa wamenunua mchezaji wa aina gani kutoka Platinum ya Zimbabwe.

Wakaanza kuguna zaidi na zaidi. Haikuonekana kama Chirwa alikuwa na maisha marefu Jangwani. Hasa kwa tabia za watu wa Jangwani.

Inaonekana labda kuna kitu kilikuwa kinamsumbua Chirwa. Labda hali ya hewa ilikuwa inamsumbua. Labda chakula kilikuwa kinamsumbua. Labda maisha ya Kitanzania nje ya uwanja yalikuwa yanamvuruga kwa kiasi kikubwa.

Labda maisha ya wachezaji wenzake yalikuwa yanamvuruga. Inadaiwa alikuwa analalamika anarogwa. Chirwa huwa ana hisia hizo. Inatokea kwa wanasoka wengi wa Kiafrika. Waafrika huwa tunajuana wenyewe.

Lakini kwa sasa Chirwa ni staa sana. Ustaa wake umekuja zaidi kutokana na majeraha ya Amiss Tambwe. Lakini ustaa wake umekuja zaidi na zaidi kutokana na tabia za ajabu za Donald Ngoma. Mzimbabwe huyu anaonekana kama vile hataki kuichezea Yanga kwa sasa.

Hii ilimfanya Chirwa amalize msimu uliopita akiwa imara. Msimu huu ameanza kuwa imara zaidi kando ya Ibrahim Ajib Migomba. Maisha yanataka nini zaidi ukiwa staa wa Yanga?  Chirwa wa leo sio yule aliyekuja mnyonge. Ana uwezo hata wa kumpiga mpigapicha na kesi ikaisha kimyakimya. Angekuwa Chirwa yule aliyekosa mabao dhidi ya Mo Bejaia basi hata viongozi wake wangemgeuka.

Sasa Chirwa amekuwa staa kiasi kama kawaida viongozi wa Yanga wapo tayari kuliingilia kazi ya benchi la ufundi ili Chirwa aiokoe timu. Anaonekana kama vile ndiye mwokozi wa Yanga kwa sasa. Jaribu kuangalia jinsi ambavyo viongozi wa Yanga na mashabiki wao walivyoshangilia Chirwa alipowasili majuzi akitokea kwao Zambia akiwa amechelewa.

Jaribu kuangalia jinsi ambavyo aliharakishiwa kwenda Zanzibar akiwa na rundo la mabosi wa Yanga ambao badala ya kufikiria namna ya kumwadhibu kwa utovu wa nidhamu wao wakageuka kuwa walinzi binafsi wa Chirwa kwenda kambini Zanzibar.

Ndani ya saa 12 tu, Chirwa ambaye alikuwa akiweka picha akiwa analima kwao Zambia akawekwa katika benchi la Yanga katika pambano dhidi ya URA. Siamini kama yalikuwa maamuzi ya Kocha Msaidizi, Shadrack Nsajigwa.

Ninachofahamu Nsajigwa, ambaye ni mchezaji aliyekuwa akicheza soka angali akiwa fiti, anaujua umuhimu wa kumpanga mchezaji aliye fiti katika mechi ya nusu fainali. Lazima alipewa shinikizo na mabosi.

Hisia zangu zinaelekea kuwa sahihi kwa sababu Kocha George Lwandamina hakujihusisha na michuano hii na kama angehusika asingekubali kumpanga Chirwa ambaye hakuwa fiti huku kukiwa na wachezaji waliokuwa wameifikisha Yanga nusu fainali.

Matokeo yake, Chirwa alikuwa anaanguka tu katika mechi dhidi ya URA. Mabosi wa Yanga walikuwa jukwaa kubwa wakisubiri abadilishe matokeo. Iliwahi kuwatokea Simba miaka ya karibuni.

Walimpeleka Emmanuel Okwi katika michuano kama hii akiwa amewasili saa 24 zilizopita kutoka kwao Uganda. Akaishia kuangukaanguka uwanjani timu ikatolewa katika michuano.

Hata penalti aliyopiga Chirwa ilitokana na kukosa hofu dhidi ya mabosi wake na mashabiki wake. Alijua tu hata kama mipango yake itakataa bado hakuna ambaye anayeweza kumfanya kitu. Kama Chirwa angekosa penalti ile akiwa Chirwa yule aliyeingia Yanga akiwa ovyo, basi si ajabu sasa hivi angekuwa kwao.

Sijui lini tutakuja kufahamu soka la kisasa katika nchi hii. Siku tukifahamu tutafika mbali sana. Tutafuta misingi ya soka. Wachezaji nao watafuata misingi ya soka. Kwa sasa inaonekana tunaendeshwa kwa mihemko ya soka na tunaweka kando weledi.

Kilichotokea kwa Chirwa ni maisha ya kawaida ya mastaa wa klabu zetu kubwa na ndogo. Wanageuzwa kuwa miungu watu na tunaweka weledi pembeni.

 Hakukuwa na sababu yoyote ya msingi ya Yanga kumpanga Chirwa katika pambano dhidi ya URA.

Pamoja na yote binafsi nampongeza Chirwa kwa upande mmoja.

Jinsi ambavyo amewaonyesha wachezaji wetu jinsi ambavyo unaweza kuingia katika timu usiwe si lolote, halafu ukaibuka kuwa mchezaji muhimu kuliko wote klabuni na kuiendesha timu puta.

Imetokea kwake. Maisha yameenda kasi sana kwake. Hakuna ubishi.