MAONI: Cannavaro usikate tamaa, angalia mbele

NAHODHA wa zamani wa Taifa Stars, Nadir Haroub ‘Cannavaro’

Muktasari:

Hata hivyo uamuzi wa mchezaji kustaafu kuichezea timu ya taifa kwa kawaida hutokana na sababu kadhaa zikiwamo, umri, majeraha na kiwango cha mchezaji kushuka, hizi ndizo sababu ambazo zimekuwa zikisikika mara kwa mara.

NAHODHA wa zamani wa Taifa Stars, Nadir Haroub ‘Cannavaro’ ametangaza kustaafu kuichezea timu hiyo.

Ni kawaida kusikia mchezaji anastaafu kuichezea timu ya taifa, wengi wameshafanya hivyo kabla yake na hapana shaka wengi wengine watafuata nyayo zake.

Kwa hali hiyo, si Cannavaro tu, kesho na keshokutwa tutasikia nahodha wa sasa wa Stars, Mbwana Samatta au msaidizi wake, John Bocco nao wakitangaza kustaafu kuichezea timu hiyo watakapoona muda wa kufanya hivyo umefika.

Hata hivyo uamuzi wa mchezaji kustaafu kuichezea timu ya taifa kwa kawaida hutokana na sababu kadhaa zikiwamo, umri, majeraha na kiwango cha mchezaji kushuka, hizi ndizo sababu ambazo zimekuwa zikisikika mara kwa mara.

Tofauti na sababu hizo, sababu nyingine huwa ni matatizo yanayojitokeza ambayo humfanya mchezaji kuchoshwa na matatizo hayo na kuamua kupumzika kuichezea timu ya taifa au kuacha kuichezea timu hiyo kwa hasira.

Sababu hii ya mwisho ndiyo aliyoifikia Cannavaro, ameamua kustaafu baada ya kukerwa na kitendo cha kocha wa Stars, Charles Boniface Mkwasa kumvua cheo cha unahodha na kumkabidhi Mbwana Samatta.

Ni kweli kwamba kilichotokea hakikumfurahisha Cannavaro, si Cannavaro tu hata mchezaji mwingine yeyote asingefurahishwa kwa namna ambavyo amenyang’anywa wadhifa wa unahodha bila kuzungumza ana kwa ana na kocha.

Kilichotokea ni kwamba Cannavaro amejiona hana thamani au hathaminiwi na ndio maana uamuzi wa kumtoa katika wadhifa huo ukafikiwa bila ya yeye kuarifiwa.

Hata hivyo tungependa kumkumbusha Cannavaro kwamba matukio kama yaliyomkuta yeye huwakuta watu wengi wakiwamo wanamichezo ambao hukereka lakini mwisho wa siku hukubaliana na hali halisi.

Ukweli ni kwamba hata kama angearifiwa kabla bado asingefurahi kuondolewa katika nafasi aliyoishikilia ya unahodha licha ya ukweli kwamba kuarifiwa kabla ingekuwa ni namna nzuri ya japo kumfariji.

Hata hivyo pamoja na hali hiyo hatudhani kama ni sahihi kwa Cannavaro kufikia hatua ya kuisusa hadi timu ya taifa au kukata tamaa kwa sababu tu ya kunyang’anywa unahodha.

Kwa upande wetu tunaamini mchango wa Cannavaro kama ambavyo umekuwa ukihitajika katika klabu yake ya Yanga, ni hivyo hivyo bado unahitajika Stars.

Kuacha kuichezea Stars kwa sababu ya unahodha au kosa lililofanywa dhidi yake si jambo zuri na halipendezi badala yake Cannavaro alipaswa kukubali hali halisi na kuangalia mbele, kuangalia mambo yake katika soka.

Ni yeye anayejua zaidi kuhusu kipaji chake, ana muda gani wa kuendelea kuichezea Yanga na Stars, muda wake ukifika wa kustaafu hapo atakuwa sahihi kustaafu lakini si kustaafu mapema kwa sababu ya unahodha.

Kufanya hivyo sit u kwamba anajinyima fursa bali pia anawanyima raha mashabiki waliopenda kumuona akiwa anaitumikia Stars.

Pia tunadhani ni muhimu kwa Mkwassa kukaa meza moja na Cannavaro na kuwekana sawa katika jambo hilo kwani kama tulivyosema awali jambo hilo halijampendeza Cannavaro na halijawapendeza wanamichezo wengine.