CHAPA MWENDO Ulimwengu akoleza hesabu zake Al Hilal

Thomas Ulimwengu

Muktasari:

  • Huo utakuwa mchezo wa pili kwake kikosini humo, baada ya awali kufunga mabao mawili katika mechi ya Ligi Kuu Sudan walioshinda mabao 4-0 dhidi ya Merreikh El-Fasher.

MGUUU sawa! Ndivyo sasa straika matata wa Kitanzania, Thomas Ulimwengu, anavyojiweka katika kikosi chake kipya cha Al Hilal, ya Sudan Kusini kuelekea mechi ya kwanza ya kimataifa akiwa na jezi za timu hiyo.

Huo utakuwa mchezo wa pili kwake kikosini humo, baada ya awali kufunga mabao mawili katika mechi ya Ligi Kuu Sudan walioshinda mabao 4-0 dhidi ya Merreikh El-Fasher.

Na sasa Ulimwengu ‘Buffalo’ anatagemewa kuiongoza tena Al Hilal keshokutwa Jumatano kwenye mechi ya Kombe la Shirikisho Afrika dhidi ya UD Songo ya Msumbiji.

Al Hilal ambao watakuwa kwenye uwanja wao wa nyumbani wa Omdurman, wanatarajiwa kuwa na mteremko kwenye mchezo huo kutokana na udhaifu wa wapinzani wao ambao hawajavuna pointi hata moja kwenye Kundi B.

UD Songo ndiyo inayoburuza mkia kwenye msimamo wa kundi hilo baada ya kupoteza michezo yote miwili ya awali mbele ya Al Masry na RSB Berkane.

Al Hilal wao wanashika nafasi ya tatu kwenye msimamo wa kundi hilo wakiwa na pointi moja ambayo waliipata katika sare ya bao 1-1 dhidi ya Al Masry ya Misri.

Kundi hilo linaongozwa na RSB Berkane wenye pointi sita ambazo wamezikusanya mbele ya Al Hilal na UD Songo na inafuata Al Masry yenye pointi nne.

MAANDALIZI USIPIME

Al Hilal imejiandaa vya kutosha kuelekea mchezo huo baada ya mechi yao ya ligi iliyotakiwa kuchezwa juzi Jumamosi dhidi ya Al Merreikh kusogezwa mbele kwa sababu za kiusalama.

Ijumaa ya wiki iliyopita, shirikisho la mpira wa miguu la Sudan lilitoa taarifa rasmi za kuusimamisha mchezo huo, muda mchache baada ya kupokea barua kutoka kwa watu wa usalama wa Khartoum.

Benchi la ufundi la Al Hilal limetumia mwanya huo kujiweka sawa na mchezo wa Kombe la Shirikisho Afrika.

ALIPOANZIA

Mzaliwa huyo wa Mkoa wa Tanga, alianza kucheza soka katika akademi ya TSA aliyodumu nayo hadi 2009 ambapo alitolewa kwa mkopo kwenye klabu ya Moro United.

Mara ya baada ya kumaliza muda wake wa kucheza kwa mkopo alirejeshwa tena kwenye akademi yake na kukaa kwa muda mfupi kabla ya kutimkia Sweden kwenye klabu ya Athletic Eskilstuna.

Kutua kwake Athletic Eskilstuna ilikuwa ni kwa mkopo na baada ya mkopo huo muda wake kumalizika, 2010 alirejeshwa tena TSA.

ATUA MAZEMBE

Aprili 2, 2011 Ulimwengu alipata dili lake la kwanza kwa kujiunga na TP Mazembe ya DR Congo aliyoichezea hadi 2016 alipogoma kuongeza mkataba mpya kwa madai ya kutaka kuihama timu hiyo.

Ndani ya miaka mitano, mshambuliaji huyo akiichezea Mazembe aliifunga mabao 33 kwenye michezo 122, huku akitwaa nao taji la Kombe la Shirikisho Afrika 2015.

Baada ya kimya cha muda mrefu bila ya timu tangu 2016 alipoigomea Mazembe, straika huyo akaibukia AFC Eskilstuna ya Sweden kwa mara nyingine tena.

Ulimwengu alitua kwa lengo la kufanya majaribio hata hivyo majeraha yalimfanya atemwa kikosini na kuamua kujitibia na hatimaye akaibukia Bosnia kwenye klabu ya FK Sloboda Tuzla.

Ishu ya kujiunga na klabu hiyo mara baada ya kufanya majaribio ilishindikana licha ya kufuzu majaribio hayo, Ulimwengu alikutana na changamoto ya kupata kibali cha kufanyia kazi nchini humo.

Akiwa kwenye mchakato wa kufuatilia vibali hivyo, Al Hilal ya Sudan ilifanikisha kumnasa, Ulimwengu alikubali kujiunga na timu hiyo kwa lengo la kucheza Afrika ili arejee kwenye makali yake kabla ya kurudi tena Ulaya.