Baada Kombe la Dunia 2018 mambo ni bata kwenda mbele

Muktasari:

  • Huo utakuwa mtoko wa siku nane ambao Dele ameamua kwenda kujifurahisha na wenzake baada ya kutokea kwenye fainali za Kombe la Dunia 2018 ambako alisaidia England kumaliza kwenye nafasi ya nne bora huko Russia.

LONDON, ENGLAND. DELE Alli amewabeba marafiki zake wanne, akiwamo Harry Hickford, aliyewahi kucheza naye huko MK Dons kisha akakodi ndege binafsi kwa ajili ya kwenda kula bata Los Angeles, Marekani kisha Ibiza.

Huo utakuwa mtoko wa siku nane ambao Dele ameamua kwenda kujifurahisha na wenzake baada ya kutokea kwenye fainali za Kombe la Dunia 2018 ambako alisaidia England kumaliza kwenye nafasi ya nne bora huko Russia.

Dele atalipia kila kitu kwenye mtoko huo na hilo halionekani kuwa na tatizo baada ya kuripotiwa hivi karibuni atasaini dili jipya huko Tottenham Hotspur ambalo litamshuhudia akiwa analipwa Pauni 100,000 kwa wiki.

Hata hivyo, Dele Alli na marafiki zake hao si wao tu, ambao wameamua kutumia vizuri mapumziko yao wakitokea kwenye fainali za Kombe la Dunia kwa kipindi hiki wakati timu zao zikianza mazoezi kwa ajili ya msimu mpya wa ligi mbalimbali za Ulaya.

Mo Salah anachezea maji ufukweni

Wakati chama lake la Liverpool likiwa kwenye maandalizi makali ya msimu mpya huku Kocha Jurgen Klopp akifanya usajili wa maana, supastaa wa timu hiyo, Mohamed Salah yupo zake huko ufukweni akicheza na maji tu.

Mo Salah alionekana akinywa juisi ya dafu kabla ya kuonekana kwenye mtumbwi huku picha nyingine zikimwonyesha akiwa kwenye ufukwe ameketi kitako kwenye mchanga.

Salah anavuta nguvu na kujipumzisha baada ya kutokea kwenye fainali za Kombe la Dunia huko Russia akiwa na kikosi cha Misri kabla ya kurudi Anfield kwenda kuonyesha makali yake ya msimu uliopita, ambapo aliweka rekodi kwa kufunga mabao 32 kwa msimu mmoja kwenye Ligi Kuu England yenye mechi 38.

Chicharito yupo na mchumba huko Miami

Kwa sasa ni mwendo wa kujiachia tu kwa mastaa waliokuwa kwenye fainali za Kombe la Dunia huko Russia. Straika wa Mexico, Javier Hernandez aka Chicharito alibeba mchumba wake, mwanamitindo matata kabisa, Sarah Kohan na kwenda naye kuponda raha huko kwenye fukwe za Miami, Marekani.

Akiwa kwenye mwonekano mpya kabisa wa kublichi nywele zake, Chicharito alionekana akiwa kwenye mapenzi motomoto na mrembo Sarah, huku mwanamitindo huyo akiwarusha roho waliokuwa kwenye ufukwe huo kutokana na vivazi vyake vya hatari.

Si unajua, mrembo Sarah ni mwanamitindo, hivyo suala la kuyaacha wazi baadhi ya maungo yake ya mwili, halijawahi kuwa gumu kwa upande wake. Nakwambia waliipata freshi, hasa kwa aliyekuwa mpenzi wa zamani wa straika hiyo, mrembo Andrea Duro, akiona hizo picha za kitu kipya cha Chicharito, atalamba ndimu.

Messi na mkewe bata kama kawa

Kutolewa mapema kwenye fainali za huko Russia hakukumtia presha Lionel Messi na kumkosesha raha, kwani alirudi nyumbani tu akamchukua mkewe, mrembo Antonella Roccuzzo kisha wakaenda kula zao raha na boti yao huko Formentera.

Messi na familia yake waliamua kwenda kujisahaulisha habari za Kombe la Dunia huko kwenye Visiwa vya Balearic vilivyopo kwenye Pwani ya Hispania na mambo yalikuwa moto huko wakati supastaa huyo wa Argentina alipoonekana akipiga mbizi kutoka kwenye boti. Kulikuwa na watu wengine walioandamana na familia hiyo ya Messi, ambapo mkewe kama kawaida yake alitupia mavazi ya kuwaumiza shingo wanaume wengine waliokuwa kwenye eneo hilo la karibu.

Hazard yuko Marbella

Si unajua kinachozungumzwa kwa sasa ni kuhusu Real Madrid na mpango wa kumsajili staa wa Chelsea, Eden Hazard.

Baada ya kukamilika kwa fainali za Kombe la Dunia ambapo nahodha huyo wa Ubelgiji aliiwezesha timu hiyo kushika nafasi ya mshindi wa tatu, Hazard aliwabeba marafiki zake na kwenda kwenye Fukwe za Marbella huko Hispania.

Hataki kujiweka mbali sana na Hispania, akisikia tu mambo yamekwenda vizuri, basi anaruka fasta Bernabeu kwenda kukamilisha mambo mengine ikiwamo ya kupima afya.