Azam kama inamaanisha kweli, imchukue Maxime

Muktasari:

  • Pengine kuanzia msimu ujao, Azam inaweza kuwa timu shiriki tu ya Ligi Kuu. Itakuwa kama Mtibwa Sugar ama Kagera Sugar, ubingwa kwao haitakuwa lengo kuu.

AZAM FC imenuia kuwa timu ya kawaida kuanzia msimu ujao wa mashindano.

Mabingwa hao wa zamani wa Ligi Kuu wamechoshwa na ubabaishaji wa soka la Bongo na sasa wanataka kuwa timu ya kawaida.

Pengine kuanzia msimu ujao, Azam inaweza kuwa timu shiriki tu ya Ligi Kuu. Itakuwa kama Mtibwa Sugar ama Kagera Sugar, ubingwa kwao haitakuwa lengo kuu.

Wamefikia hatua hiyo baada ya kubaini kuwa mfumo wa soka la Bongo unazibeba zaidi timu za Simba na Yanga. Japo hawajasema hadharani, lakini nafahamu kwamba kitendo cha mwamuzi ‘kuibeba’ Simba katika mechi ya nusu fainali ya Kombe la FA ndicho kilichochea zaidi hasira yao. Chuki zetu zimewafikisha hapa.

Hata hivyo, Azam haitaki kupoteza tu muda, imepanga kuwapa nafasi vijana ili baadaye iweze kuwauza kwingineko huko duniani. Wanataka kufanya kama walivyomtoa Farid Mussa wawatoe pia na wengine.

Ni mpango mzuri na wenye manufaa zaidi kwa klabu na taifa. Kama Azam imeamua kuwa kitovu cha kuibua vipaji nchini na kuuza itakuwa jambo la maana zaidi. Huko Uholanzi kuna timu inaitwa Ajax Amsterdam nayo inafanya hivyo.

Baada ya muda pengine hawa kina Shaban Iddi Chilunda, Abdallah Masoud, Yahya Zaidi na wengineo kutoka Akademia ya Azam wanaweza kuwa nje ya nchi wakicheza soka la kulipwa.

Kwa kifupi, Azam itakuwa timu ya kwanza nchini kujikita kwenye biashara ya kuuza wachezaji nje. Kama watatengeneza miundombinu na chaneli sahihi watanufaika sana.

Kwa sasa tayari wameimarisha timu zao za vijana. Walizunguka nchi nzima kutafuta vipaji vya umri kati ya miaka 12 hadi 17. Kwa hill hakuna mashaka kwamba Azam ina timu bora za vijana sasa.

Wachezaji hao wanaishi katika mazingira mazuri pale Chamazi na wanafundishwa na kocha mzungu. Ni mipango mizuri kwa klabu iliyopanga kuwekeza katika soka la vijana.

Kwa upande wa pili, kama Azam imeamua kweli kuwekeza katika soka la vijana, hakuna haja ya kuwa na kocha mzungu katika timu ya wakubwa.

Kuwa na kocha mzungu wakati lengo kuu la timu ni kutengeneza vipaji, siyo jambo la faida. Tena katika nchi ambayo ina makocha wazuri wazawa.

Kwa walichoamua Azam sioni sababu ya kuendelea kuwa na Mromania, Aristica Cioaba. Kuwa na kocha mzungu wakati wachezaji wake ni Yahya Zaidi na Waziri Junior ni kumpotezea muda.

Ukiwa na kocha mzungu walau uwe unawaza zaidi kutwaa mataji lakini siyo kutengeneza vipaji. Kwa kocha mzungu kwanza atakuwa anaminya wasifu wake kwani hautakuwa ukivutia.

Wakati huu ambao tuna kocha mzawa mwenye sifa ya kuzalisha vipaji kama Mecky Maxime ni bora Azam wakampa timu. Kuna vitu vingi watanufaika wakiwa na Maxime kuliko kocha mzungu.

Kwanza, Maxime atawasaidia katika lengo lao kuu la kukuza vipaji na kuuza. Amewahi kufanya hayo akiwa Mtibwa Sugar na hata Kagera Sugar.

Akiwa Mtibwa alimtengeneza Juma Liuzio, akamuuza kwenda Zesco ya Zambia. Kama siyo kurudi nyuma, pengine Liuzio sasa angekuwa mbali. Kwa

bahati mbaya amerudi hapo Kariakoo na muda si mrefu atarejea Mtibwa. Maxime akawatengeneza Shiza Kichuya, Mzamiru Yassin, Hassan Kessy, Mohammed Ibrahim, Andrew Vincent na wengineo akawauza kwenda Simba na Yanga.

Hao ni wachache kati ya wengi waliopita katika mikono ya Maxime. Kazi ya kukuza vipaji anaiweza sana. Msimu huu tumeona namna alivyopandisha kiwango cha Mbaraka Yussuf ambaye anagombewa na klabu za Ligi Kuu kama njugu.

Kwa Maxime kumpika mchezaji akaiva halijawahi kuwa tatizo. Anaweza kuifanya kazi hii pale Azam kwa umaridadi zaidi. Anaweza kwa kuwa Azam tayari ina miundombinu ya kusapoti soka la vijana.

Ataweza zaidi kwa kuwa lengo kuu la Azam ni kuibua na kukuza vipaji. Atakuwa akipata vijana wengi kutoka timu za vijana na kazi yake itakuwa ni kuwapa mafunzo zaidi na kuwainua.

Sina shaka na Maxime katika kazi hii. Anaweza kuifanya Azam ikawa kama Ajax ya Afrika. Kikubwa ni mabosi wa Azam kumwamini tu.

Pili, Maxime anaweza kuendelea kuifanya Azam kuwa timu ya ushindani wakati huohuo ikikuza vipaji. Aliifanya Mtibwa kuwa ya ushindani wakati akikuza vipaji. Tulishuhudia baadhi ya nyakati ambazo Mtibwa iliuza wachezaji kadhaa na bado haikuathirika.

Msimu uliomalizika tuliona namna Kagera Sugar ilivyofanikiwa kuwa timu ya ushindani wakati ikiwa na wachezaji wa kawaida tu. Kwanini ashindwe kuifanya Azam iwe ya ushindani?

Kikubwa ni kwa mabosi wa Azam kuamua moja kwa moja kwamba timu yao haitaupa kipaumbele ubingwa wa Ligi Kuu tena, ikitokea wameupata iwe ni ziada tu.

Hapo Maxime ataweza kufanya kazi hiyo kwa umahiri mkubwa. Nina imani kwamba baada ya miaka miwili Azam itaanza kuona matunda yake. Hawa kina Shaban Iddi, Yahya Zaidi tutawaona Ulaya mbona.