Azam FC sasa imerudi njia ya Uzima

Muktasari:

  • Huu ni ukweli ambao hata wadau wakubwa wa timu hiyo wakiongozwa na wanafamilia wa mfanyabiashara mkubwa na maarufu Afrika, Mzee Said Salim Bakhressa wanaufahamu.

AZAM FC haikuwa inakwenda njia sahihi kulingana na malengo na matarajio yake ambayo yalipangwa wakati timu hiyo ilipopanda Ligi Kuu.

Huu ni ukweli ambao hata wadau wakubwa wa timu hiyo wakiongozwa na wanafamilia wa mfanyabiashara mkubwa na maarufu Afrika, Mzee Said Salim Bakhressa wanaufahamu.

Kutokana na nguvu kubwa ya kiuchumi ambayo wanayo, moja ya malengo ya Azam FC lilikuwa ni kufanya vizuri katika mashindano mbalimbali ya ndani na yale ya kimataifa.

Azam FC ilikuja katika kipindi ambacho kundi kubwa la wadau wa soka nchini walikuwa wameshaanza kuchoka na kukinai ubabe wa Simba na Yanga katika soka la Tanzania.

Kabla ya hapo baadhi ya timu zilijitahidi kuleta upinzani kwa Simba na Yanga katika kutwaa mataji mbalimbali hasa yale ya ndani lakini zilichemka na kuishia njiani na sababu kubwa iliyoplekea hilo ilikuwa ni nguvu ndogo ya kifedha.

Mtibwa Sugar walichukua ubingwa wa Ligi Kuu Bara mara mbili mfululizo mwaka 1999 na 2000 lakini hawakuweza kuwa na muendelezo tena kutokana na kutokuwa na misuli ya kifedha kupambana na vigogo vya soka nchini ambavyo vimekuwa vikibebwa na mtaji wa kuwa na idadi kubwa ya mashabiki na wanachama.

Kwa bahati mbaya kile kilichotarajiwa hakikuweza kufanywa na Azam kwani katika miaka 10 ya ushiriki wake kwenye ligi, imetwaa ubingwa mara moja tu huku Yanga ikitwaa mara sita na Simba mara tatu.

Hili halikuwa jambo la kufurahisha.

Kwa timu ambayo ilitumia fedha nyingi kusajili na kulipa mishahara makocha, wachezaji na madaktari wa kiwango cha juu, kuchukua ubingwa mara moja ndani ya misimu kumi, inashangaza kidogo.

Lakini pia Azam FC ilitegemewa kuwa timu itakayotengeneza fursa kwa kundi kubwa la vijana wa Tanzania kwenda nje ya nchi kucheza soka la kulipwa kutokana na uwekezaji mkubwa iliyoufanya kwa kujenga miundombinu kama vile viwanja na hosteli kwa ajili ya kutumiwa na kikosi cha wakubwa na vile vya vijana wadogo. Unapokuwa umefanya uwekezaji mkubwa kwa timu ya vijana watu watahitaji kuona unazalisha nyota ambao watakwenda kucheza soka la kulipwa nje ya nchi

kama ambavyo timu za ASEC Mimosas, WAFA na USM Algers zinafanya.

Kwa bahati mbaya kundi kubwa la wachezaji chipukizi ambao Azam iliwakusanya, hawakupandishwa kwenye kikosi cha wakubwa, hawakuuzwa nje ya nchi na wengi wao waliondoka bure baada ya mikataba yao kumalizika. Inamanisha kwamba Azam ilikuwa inafanya kazi bure.

Msimu uliopita, Azam ndio ilijichanganya zaidi kwa kutowaongezea mikataba kundi kubwa la wachezaji waandamizi ambao walikuwa uti wa mgongo kwenye

kikosi chao na kuwapa nafasi vijana kwa kigezo cha kujenga timu.

Haukuwa uamuzi wenye tija na hata wenyewe Azam wanakiri kuhusu hilo kwani nyota walioondoka ndio waliowanufaisha Simba kutwaa ubingwa wa Ligi Kuu.

Kama kweli walikuwa na nia ya kujenga timu ya muda mrefu, walichotakiwa ni kuwaondoa wakongwe hao taratibu badala ya kuwaondoa kwa mpigo kama walivyofanya wao.

Hata hivyo, inaonekana Azam FC wamejifunza kutokana na makosa yao na sasa wameanza kurejea taratibu kwenye njia na mstari sahihi. Usajili walioufanya kwa kuimarisha benchi la ufundi na kikosi chao unaonekana wazi utairejesha timu hiyo mahala pake msimu ujao.

Hivi karibuni wametangaza kufikia makubaliano na klabu ya Tenerife ili kumhamisha mshambuliaji wao tegemezi Shaaban Idd aliyeibukia kikosi cha vijana. Mauzo ya mshambuliaji huyo ni dalili za mageuzi makubwa ambayo yanafanyika ndani ya Azam kwa kuanza kuwauza nyota wake ambao inawategemea.

Haijawahi kutokea kwa Azam kuuza mchezaji muhimu kama ilivyofanya kwa Shaban Idd ambaye alikuwa mfungaji wao bora msimu uliopita lakini pia hadi sasa

ndiye anayeongoza kwa kupachika mabao Kombe la Kagame.