STRAIKA WA MWANASPOTI: Arsenal hii, yaweza isiingie hata nne bora EPL

Muktasari:

Nitajaribu kugusia kwa undani haswa kwa mtazamo wangu kama mchezaji na kocha na pia kama mchambuzi wa maswala ya kisoka.

Ligi Kuu England inazidi kushika makali kwa kila klabu ikiwa imecheza mechi mitatu kufikia sasa. Hata hivyo, mambo hayajakuwa mazuri sana kwa Arsenal kutokana na vichapo, juzi mabao 4-0 kupitia kwa mikono ya Liverpool FC, Uwanja wa Anfield na kile cha 1-0 cha Stoke City.

Nitajaribu kugusia kwa undani haswa kwa mtazamo wangu kama mchezaji na kocha na pia kama mchambuzi wa maswala ya kisoka.

Kichapo cha mabao 4-0 kilikuwa kichungu sana kwa mashabiki wa klabu hiyo ya Arsenal. Ndugu zanguni kwa mda mrefu kocha Arsene Wenger amekuwa mkono gamu saana saana.

Hapendi kutumia hela wakati wa usajili na inakuwa vigumu yeye kupelekana mbio Ligi Kuu hiyo na wenzake kama Jose Mourinho, Kloop, Conte, Pep Guardiola na kadhalika.

Ukiangalia wakati wowote wa dirisha la usajili liwe ndogo ama kubwa hakuna wakati Wenger ametumia zaidi ya Dola100 milioni kufanya usajili.

Amekuwa mkono gamu sana. Wakati mameneja wengine wanaingia sokoni mapema kusaka wachezaji ambao itawasaidia ndani ya msimu, yeye hubaki kutazama tuu.

Ukiangalia msimu uliopita, kwa kweli chanzo kikubwa cha Arsenal kutomakinika ndugu zangu kilikuwa ni kuwa na safu butu ya ulinzi. Mlinda lango Petr Cech ni mzuri sana lakini shida kubwa kabisa ni ulinzi.

Mabeki wa Arsenali hawajafanya jambo la kuniwezesha kuwakubali kwamba wanaweza fanya kazi nzuri msimu wote.

Inakuwa ni vigumu sana Arsenal kustahimili vipigo. Arsenal ni klabu kubwa lakini muda wa hivi karibuni ndugu zanguni nimekuwa nikiwashuku wanavyotenda mambo yao haswa ya kiusajili.

Wakati klabu zingine zinatumia mamilioni ndani ya usajili kuhakikisha ngome zao zinakaa sawa, Wenger naye amebaki kutazama tu.

Ukitaka kushinda mataji yeyote hii dunia ndugu zanguni, ni lazima uwe na wachezaji wa kutenda hilo jambo. Na wachezaji wa kukuwezesha kushinda mataji sio wachezaji wa kawaida tuu ndugu zanguni.

Ni lazima ununue wachezaji walio ghali. Sio kununua magarasa ndugu zanguni. Sio kununua tu mradi kununua. Ukitaka kushinda mataji lazima uwe na walinda lango hodari, mabeki hodari.

Mabeki ambao hawarusu kupitwa kiholelaholela, viungo wakabaji wazuri na pia washambuliaji wazuri. Ni jambo ambalo tangu msimu uanze hatujalishuhudia pale Emirates ndugu zanguni.

Hebu kumbuka mechi dhidi ya Leicester City. Arsenal ilikubali mabao matatu japo ilishinda 4-3, ikakubali bao moja dhidi ya Stoke City na hatimaye mechi ya tatu imekubali kichapo cha mabao 4-0.

Kwa jumla Arsenal msimu huu ndani tuu ya mechi mitatu washafungwa mabao manane ndugu zangu. Ni jambo ambalo linatia kiwewe mchezaji, kocha na mashabiki wote wa Arsenal.

Ni jambo ambalo Wenger kama mkufunzi wa hiyo klabu atabaki kulaumiwa.

Jambo lingine la kushangaza ni kuwa hadi kufikia msimu ukianza hawakuwa wamefikia makubaliano kamili na mshambulizi wa Alexis Sanchez ambaye juzi katika mechi ya Liverpool alionekana kutokuwa sawa kabisa.

Cha kunishangaza ni kuwa huyo huyo mchezaji, mechi mbili za utangulizi hakucheza. Itakuwaje Wenger amuanzishe katika mechi ya Liverpool.

Cha pili aliacha mshambulizi wake hodari, Alexander Lacazette kwenye benchi. Jambo ambalo linishangaza. Huwezi kununua mchezaji kwa hela zile halafu aanzie benchi ndugu zanguni.

Haiwezekani kabisa. Labda kama ako na jeraha ndugu zanguni. Kuwepo tuu kwake uwanjani tayari hutia timu ambayo unaenda kucheza nayo kiwewe.

Itakuwa vigumu sana kwa |Arsenal kupata wachezaji wenye tajriba ndugu zanguni katika miaka ya karibuni. Arsenal wapo katika nafasi ya 16. Mechi za Arsenal zinazofuata ni kama ifuatavyo. Bournemouth, Chelsea, West Brom, Brighton, na Watford.

Hizo ndio mechi tano ambazo zaja hivi karibuni ndani ya Ligi Kuu England kwa Arsenal. Itabidi wajikakamue sana ndani ya hizo mechi la sivyo itakuwa ngumu kwao msimu huu kumaliza ndani ya nne bora kwa mara nyingine.