HISIA ZANGU: Ambacho Wazungu wangekifanya kwa Kamusoko

Tuesday March 13 2018

 MCL

NILISOMA mahala kwamba Thabani Kamusoko alicheza ovyo pambano lake la kwanza tangu arejee kutoka katika majeraha. Ilikuwa ni dhidi ya Kagera Sugar. Walitaka afanye nini zaidi? Baada ya kukaa nje kwa muda mrefu angefanya nini zaidi?

Papo hapo nilikumbuka tunavyoishi katika dunia mbili tofauti za soka. Kuna sisi Tanzania halafu kuna wenzetu wa mbali. Wenzetu ninamaanisha wote wale ambao wanaitilia maanani soka. Sisi hatuutilii maanani.

Nimekumbuka ambacho wenzetu, hasa Wazungu wangemfanyia Kamusoko kabla ya kucheza mechi yake ya kwanza. Kwanza kabisa wangeandaa mechi maalumu kwa ajili yake tu kwa ajili ya kumrudisha kuwa fiti.

Mara nyingi mechi hizo zinahusisha wachezaji chipukizi pamoja na wale ambao hawapati nafasi mara kwa mara katika kikosi cha kwanza kama akina Maka Edward. Inakuwa mechi ambayo inamlenga mchezaji mmoja tu ili awe fiti.

Kamusoko au mchezaji yeyote ambaye amekaa nje kwa muda mrefu hawezi kurudi kuwa bora moja kwa moja kwa kutegemea mazoezi ya wachezaji wenzake ambao wakati mwingine huwa wanampisha mazoezini kwa kuhofia kumuumiza tena.

Katika mechi maalumu, mchezaji atahisi presha ya mechi kwa sababu atacheza dhidi ya wachezaji ambao hafahamiani nao. Atahisi kurudi kwa mazingira ya soka. Yanga wamemrudisha mchezaji moja kwa moja wakati ilibidi wamtafutie mechi maalumu za kumuweka fiti.

Angeweza kwanza kucheza mechi za timu ya vijana chini ya umri wa miaka 20. Ingeweza kumuweka kuwa fiti akajihisi amerejea uwanjani.

Kwa mfano, Santi Cazorla ameumia kwa muda mrefu sasa. Kwanza atarudi mazoezini katika kikosi cha wakubwa lakini atatafutiwa mechi katika kikosi cha vijana wa Arsenal ili aanze kujirudisha kuwa fiti.

Wenzetu mpira ni shughuli zao. Jaribu kufikiri watu wanavyoweza kuandaa mechi kwa ajili ya mchezaji mmoja tu. Lakini hata sisi tungeweza kama tungekuwa tunaiga baadhi ya mifumo ya soka la Ulaya.

Lakini hapo hapo nimekumbuka jinsi ambavyo soka letu halina miundo ya soka. Iko wapi timu ya wachezaji wa akiba? Iko wapi timu ya vijana? Inafanya mazoezi wapi kama wachezaji wa timu kubwa hawana uwanja wa kudumu wa mazoezi?

Hii ina maana kwamba mechi dhidi ya Kagera Sugar na kama akipangwa dhidi ya Rollers pale Botswana basi hizi zitakuwa mechi za kumuweka fiti Kamusoko kwa ajili ya mechi za baadaye. Bahati mbaya ni mechi za ushindani.

Wenzetu wanakwenda mbali zaidi. Wakati mwingine sio mchezaji majeruhi tu, lakini wanaweza kumnunua mchezaji mpya kutoka mbali na kuanza kumzoesha mazingira kwa kumpanga katika mechi za wachezaji wa akiba au timu ya vijana.

Mfano mzuri ni mastaa wetu wawili, Mbwana Samatta na Farid Mussa. Samatta alipokwenda Genk hakuanza kucheza timu ya wakubwa moja kwa moja. Kocha wake alimpeleka katika timu ya wachezaji wa akiba kwa ajili ya kuanza kuzoea soka la Ulaya. Alipoonekana yuko fiti na anacheka na vyavu kama kawaida wakampandisha.

Sawa, wanajua uwezo wake, wanajua kitu walichokinunua, lakini wanajua kwamba hayupo fiti kwa asilimia 100 kucheza katika kikosi cha wakubwa. Na alipoitwa katika kikosi cha wakubwa alianza kuingia taratibu dakika za mwisho.

Farid Mussa alipokwenda Tenerife ilimchukua miezi sita akicheza katika kikosi cha vijana chini ya umri wa miaka 23. Walijua kwamba alichukuliwa kwa ajili ya kuwa mchezaji wa timu kubwa, lakini wakaanza kumzoesha soka la Ulaya kwa kupitia vijana.

Tunaweza kushindwa kuiga mambo makubwa ya Ulaya lakini hata haya ya akili ya kawaida kabisa yanatushinda!

Mchezaji aliyekaa nje kwa miezi minne anarudi moja kwa moja katika kikosi cha kwanza na anapangwa kuanzia dakika ya kwanza.

Halafu hapo hapo kuna watu wanalaumu kwamba amecheza ovyo.

Kuna mpira wetu halafu kuna mpira wao. Mpira wetu ni huu hapa ambao Obrey Chirwa anapangwa pale Zanzibar siku moja baada ya kutoka shambani kwao Zambia.

Mpira wa Ulaya ni ule wa kumweka mchezaji fiti katika programu maalumu.

Sijui lini tutabadilika lakini kama tunashindwa kutumia akili za kawaida basi safari ni ndefu.