MTU WA PWANI: Akili za Tenga zinavyohitajika TFF

Muktasari:

Ni wazi kuwa hatuwezi kumpata Rais wa TFF atakayekuwa kama Tenga, lakini tunaamini wajumbe wanaweza kutupatia kiongozi, ambaye atajaribu kuenenda sawa na mtazamo wa Tenga.

KESHO Jumamosi Shirikisho la Soka la Tanzania (TFF), litafanya mkutano mkuu wake utakaofanyika mjini Dodoma ambao, ajenda yake kuu ni uchaguzi wa viongozi watakaoliongoza shirikisho hilo kwa miaka minne ijayo.

Ni uchaguzi utakaoshirikisha zaidi ya wagombea 60 ambao wamejitokeza kuwania nafasi za Rais, Makamu Rais na Ujumbe wa Kamati ya Utendaji kuwakiwakilisha kanda 13 za kisoka zilizopo Tanzania Bara.

Vita kubwa inaonekana ipo kwa wagombea wanaowania urais ambapo, kuna wagombea sita. Wagombea hao ni Katibu Mkuu wa zamani wa TFF, Fredrick Mwakalebela, nahodha wa zamani wa Yanga na Taifa Stars, Ally Mayay na aliyewahi kuwa Mweka Hazina wa Chama cha Waandishi wa Habari za Michezo Tanzania (Taswa), Shija Richard.

Wengine ni Kaimu Rais wa sasa wa TFF, Wallace Karia, Mwenyekiti wa zamani wa Yanga, Iman Madega pamoja na Katibu Mkuu wa klabu ya Mbeya City, Emmanuel Kimbe.

Kuanzia Jumatatu ya wiki hii, wagombea hao na wale wa nafasi nyingine, walikuwa wakizunguka huku na kule kunadi sera, mipango na mikakati yao waliyopanga kulifanyia soka la Tanzania iwapo wakipata fursa ya kuchaguliwa kushika nafasi wanazowania.

Baada ya kampeni hizo ambazo leo Ijumaa zipo katika siku ya tatU, ni wazi kuwa kazi sasa imebakia mikononi mwa wajumbe wa mkutano mkuu ambao, wenyewe ndio wameshika mpini wa kuamua nani anafaa na nani hafai kuwemo katika safu ya uongozi wa TFF.

Tunapoingia katika uchaguzi huo ni vyema wajumbe wa mkutano mkuu wakakumbushwa ni aina gani ya kiongozi anayehitajika katika kuusimamia mchezo huo.

Watanzania wanahitaji kiongozi atakayeondoa ombwe lililoonekana katika uongozi wa awamu inayomaliza muda wake na kuleta matumaini mapya kwa wadau wa soka nchini. Watanzania wanamtaka kiongozi atakayevaa viatu vya aliyewahi kuwa Rais wa TFF, Leodegar Tenga.

Tenga alilitoa soka letu kuzimu na kuleta mwanga wa matumaini kutokana na uongozi wake imara uliozingatia misingi ya utawala bora tofauti na nyakati nyingine ndani ya shirikisho hilo.

Alihakikisha misingi ya uwazi na uwajibikaji inafuatwa na kila mtendaji ndani ya shirikisho jambo lililoifanya TFF iwe na mahusiano bora na wadau wa soka, serikali na kampuni mbalimbali ambazo ziliamua kudhamini soka letu.

Hii yote ilitokana na Tenga kuheshimu misingi ya weledi na uadilifu katika kuisimamia TFF. Ni wazi kuwa hatuwezi kumpata Rais wa TFF atakayekuwa kama Tenga, lakini tunaamini wajumbe wanaweza kutupatia kiongozi, ambaye atajaribu kuenenda sawa na mtazamo wa Tenga.

Kuvaa viatu vya Tenga kunahitaji mtu mwenye rekodi nzuri ya utendaji na uadilifu katika nafasi alizoongoza iwe ndani ya shirikisho au katika taasisi nyingine za umma ama binafsi.

Haipaswi kumchagua mtu kwa kigezo cha ukanda, urafiki au rushwa kama ambavyo utamaduni wa chaguzi za shirikisho hilo unavyokuwa.

Wajumbe wa mkutano mkuu wanapaswa kutambua kuwa, wamebeba hatima ya soka la Tanzania kwa miaka minne ijayo na historia inaweza kuwahukumu kwa aina ya uamuzi watakaoufanya kwa kiongozi watakayemchagua.

Watanzania wanahitaji Rais, ambaye atakuja na mpango mkakati wa kulitoa soka letu kaburini badala ya yule atakayetengeneza mazingira ya uwepo wake TFF kujinufaisha binafsi, jambo ambalo limekuwa likifanywa na kundi kubwa la watu wanaopewa nafasi ya kuongoza soka nchini.

Utawala wa Tenga haukuweza kutupatia kila tulichotarajia kukipata kwenye soka, lakini ulifanikiwa kutengeneza njia ambayo kama ingefuatwa na aliyekuja baada yake, pengine leo Tanzania ingekuwa imesogea mbele kidogo.

Ndiyo maana hata baada ya kuamua kutoendelea tena na nafasi ya urais, Tenga bado ameendelea kuteuliwa katika nyadhifa mbalimbali za soka Fifa na hata Caf, hii yote ni kutokana na heshima aliyoiacha katika uongozi wa TFF.

Tunaamini wajumbe wanafahamu fika kiu ya Watanzania kutaka kuona mpira wa miguu unapata mafanikio, hivyo watuletee kiongozi bora. Watanzania ni wanazi wa soka na ndio sababu viwanja vya Tanzania vinafurika mashabiki kuliko nchi zote Ukanda wa Afrika Mashariki na Kati.

Hivyo, wajumbe watambue soka ni ajira kubwa ambayo inaweza kuongeza kasi ya uchumi wa taifa hivyo, wafanye maamuzi makini.