Ajib Yanga, Haruna Niyonzima Simba nani amelamba dume?

Muktasari:

Yanga tayari imemsainisha Ajib mkataba wa miaka miwili baada ya kumng’oa pale Msimbazi na itamtangaza rasmi punde mkataba wake na Simba utakapofikia tamati mwezi ujao. Simba nao wamejibu mapigo kwa kumnasa Niyonzima baada ya kumchomoa pale Yanga, hili limethibitika zaidi baada ya Yanga kutangaza rasmi kuwa haitakuwa naye msimu ujao.

MJADALA unaoendelea mitaani kwa mashabiki wa soka nchini hivi sasa ni kuhusu usajili wa Ligi Kuu Bara, kubwa zaidi ni kuhusiana na Simba na Yanga. Katika hilo kuna swali wadau wanaulizana; nani amenufaika zaidi, Yanga kumsajili straika Ibrahim Ajib au Simba kwa kumsainisha kiungo Mnyarwanda, Haruna Niyonzima?

Yanga tayari imemsainisha Ajib mkataba wa miaka miwili baada ya kumng’oa pale Msimbazi na itamtangaza rasmi punde mkataba wake na Simba utakapofikia tamati mwezi ujao. Simba nao wamejibu mapigo kwa kumnasa Niyonzima baada ya kumchomoa pale Yanga, hili limethibitika zaidi baada ya Yanga kutangaza rasmi kuwa haitakuwa naye msimu ujao.

Usajili huu umekuwa gumzo hasa ikizingatiwa wachezaji hao walikuwa muhimu katika timu wanazotoka. Hakuna asiyefahamu umuhimu wa Niyonzima ndani ya Yanga, na Ajib katika kikosi cha Simba.

Swali na nani amelamba dume, ngoja tulitazamae kwenye jicho la ufundi. Kwanza kabisa hauwezi kuwapambanisha Ajib na Niyonzima. Hawa ni wachezaji wa nafasi mbili tofauti, hivyo hata vigezo vya ubora katika nafasi zao ni tofauti pia. Ajib ni straika, tunampima kwa mabao aliyoyafunga pamoja na pasi za mabao alizotoa. Niyonzima ni kiungo, tunampima kwa namna anavyochezesha timu, pasi zake za mwisho pamoja na uwezo wa kukaba. Kwa Niyonzima kufunga ni kitu cha ziada.

Tukirejea kwenye masuala ya kiufundi, lazima tukubaliane kwa Simba na Yanga kuwanasa wawili hao, zote zimesajili katika maeneo ambayo hayakuwa na upungufu kwao.

Simba haikuwa na tatizo la kiungo. Inao viungo wengi na wenye uwezo wa hali ya juu. Yupo nahodha Jonas Mkude, Mghana James Kotei, Said Ndemla, Mzamiru Yassin, Mwinyi Kazimoto na Mohammed Ibrahim.

Viwango vyao wote hao ni vya daraja la juu kwa hadhi ya soka letu, ni Kazimoto tu ndio ameanza kuzeeka. Kwa kifupi eneo hili la kiungo kwa Simba halikuwa na mapungufu makubwa. Unaweza kusema Simba imeimarisha eneo imara.

Kwa Yanga, safu yake ya ushambuliaji haikuwa na tatizo pia. Ndiyo safu ya ushambuliaji iliyofunga mabao mengi zaidi msimu uliopita. Ina Amissi Tambwe, Donald Ngoma, Obrey Chirwa na Simon Msuva ambaye husaidia kufungua. Halikuwa eneo lenye shida sana. Yanga nao wameimarisha eneo imara.

Kitu cha pili ambacho lazima tukubaliane, ni usajili huu umezibomoa zaidi timu walizotoka wachezaji hao. Simba ilikuwa na tatizo katika safu yake ya ushambuliaji, Ajib ndiye mchezaji aliyekuwa na nafuu. Ndiye mchezaji aliyekuwa na uwezo wa kurudi nyuma na kuwachezesha washambuliaji wenzake. Ndiye mchezaji aliyeweza kufunga na kutoa pasi za mwisho.

Alikuwa na uwezo mkubwa pia wa kupiga mipira ya adhabu. Kwenye safu ya ushambuliaji ya Simba ndiye alikuwa bora zaidi, hivyo kuondoka kwake ni pigo kubwa Msimbazi.

Vivyo hivyo kwa Niyonzima. Yanga ina safu dhaifu ya kiungo na Niyonzima ndiye mchezaji aliyekuwa na ubunifu mkubwa zaidi. Wakati Thaban Kamusoko akishuka makali yake, Niyonzima alisimama na kuibeba timu. Alikuwa hodari wa kufungua uwanja na kupiga pasi za mwisho.

Kwa kifupi tunasema Niyonzima kwenda Simba, kumeacha pigo kubwa kwa Yanga. Anaweza asiisaidie sana Simba lakini atakuwa ameiumiza zaidi Yanga ambayo sasa lazima itafute mbadala wake.

Kitu cha tatu ambacho lazima tukubaliane ni kwenye uwezo wa mchezaji mmoja mmoja. Wachezaji wote hao ni watu wenye vipaji vikubwa vya soka.

Rafiki yangu Abdul Mkeyenge huwa anasema kwa wachezaji wa Ligi Kuu Bara hauwezi kumfananisha Niyonzima na mchezaji mwingine. Niyonzima anafananishwa na Niyonzima mwenyewe. Unajua huwa anamaanisha nini? Ni kwamba, aina yake ya uchezaji anayo mwenyewe tu.

Ana ubunifu wa aina yake. Ana uwezo wa kuwahadaa mabeki na kutoa pasi. Ana uwezo mkubwa wa kuchezesha timu na kulazimisha matokeo. Mechi dhidi ya Simba tu ndiyo ilikuwa ikimpa wakati mgumu.

Kwa upande wa pili, Ajib naye hauwezi kumfananisha na mchezaji mwingine wa Ligi Kuu Bara. Licha ya kwamba Yanga ina washambuliaji hatari, lakini hakuna mwenye kipaji kama cha Ajib.

Ajib anaweza kupunguza mabeki wawili hadi watatu na kufunga. Donald Ngoma hawezi kufanya hivyo. Amissi Tambwe na Obrey Chirwa hawawezi kazi hiyo. Hapa ndiyo tunapomfananisha Ajib na Ajib mwenyewe. Tatizo kubwa la Ajib ni kwamba hayupo siriazi sana na mambo yake.

Huwa anacheza vizuri pindi anapojisikia. Kuna nyakati anakuwa kama hataki kucheza, nyakati nyingine anacheza kwa kiwango cha juu. Kama atabadilika, ataisaidia Yanga.

Mwisho wa siku tofauti kubwa ambayo ipo baina yao ni umri. Niyonzima ni mchezaji mkongwe na Ajib ni mchezaji chipukizi. Niyonzima amecheza Ligi Kuu ya Rwanda kwa miaka sita kabla ya kuja Tanzania ambako pia amecheza kwa miaka sita. Hivyo, amecheza ngazi ya Ligi Kuu kwa miaka 12.

Ajib ndiyo kwanza amecheza misimu mitatu tu Ligi Kuu. Aliibuliwa na Simba mwaka 2013 na kumpeleka kwa mkopo Mwadui. Alirejeshwa kwenye kikosi cha Simba mwaka 2014 ambako amedumu mpaka sasa.

Hii inamaanisha kwamba Simba itanufaika na uzoefu wa Niyonzima, lakini ni kwa muda mfupi, wakati Yanga itanufaika na uchanga wa Ajib lakini pia inaweza kuwa kwa muda mfupi kwani amesaini mkataba wa miaka miwili tu.

Mpaka hapo unaweza kuona nani amelamba dume katika klabu hizi mbili kubwa katika soka la Tanzania.