STRAIKA WA MWANASPOTI: Ajabu, Mchezaji Bora kakosekana timu ya taifa!

Muktasari:

Kwanza naomba ieleweke kuwa binafsi nimewahi kuichezea Stars. Kipindi hicho nikiwa mchezaji, niseme wazi tu kuwa kulikuwa na baadhi ya makocha ambao kwa leo sitawataja majina waliokuwa wakifanya uteuzi kwa upendeleo.

WIKIENDI iliyopita kilitajwa kikosi cha timu ya taifa ya soka, Harambee Stars, kilichowajumuisha wachezaji kadhaa huku baadhi yao uteuzi wao ukizua utata wa hapa na pale.

Kwanza naomba ieleweke kuwa binafsi nimewahi kuichezea Stars. Kipindi hicho nikiwa mchezaji, niseme wazi tu kuwa kulikuwa na baadhi ya makocha ambao kwa leo sitawataja majina waliokuwa wakifanya uteuzi kwa upendeleo.

Ninachokisema hapa kinatokana na uzoefu wangu halisia na wala si jambo la kuhadithiwa. Kikosi kilikuwa kinaitwa kwa kujuana, ilishangaza. Kuna wachezaji walikuwa wanaitwa timu ya taifa wakati kwenye klabu zao hata namna walikuwa hawapati.

Wengi wao walikuwa wanakula benchi tu, lakini ukifika ni wakati wa kuitwa timu ya taifa hawakuwa wanakosa. Jambo lilikuwa likinitatiza sana, lakini kwa vile sikuwa na la kufanya zaidi ya kucheza, iliishia hivyo.

Nakumbuka kuna wengine ilikuwa wanaitwa hata wakiwa wako na majeraha. Hivi mchezaji kama huyo unategemea atakusadia nini? Ndio maana hatukuwahi kuwa na mafanikio makubwa sana ya kujivunia.

Lakini kati ya makocha niliotokea kuwafahamu katika soka letu hapa Kenya, kuna huyu Reinhard Fabisch, hakika kazi aliifanya na Mungu ailaze roho yake mahali pema peponi.

Yeye ni miongoni mwa makocha ninaowaheshimu sana. Alikuwa anafanya utafiti wake wa kiundani sana kabla ya kumuita mchezaji katika timu ya taifa. Ukiangalia kwa kweli alikuwa na kikosi hatari.Yeye alikuwa tofauti na makocha wengine. Utofauti wake uliendelea kwa miaka mingi, angalau kidogo sasa kuna mabadiliko katika Harambee Stars ya sasa iliyotangazwa.

Tangu kutangazwa tena kwa Stars wikiendi iliyopita, jambo ambalo bado nalifikiria ni kutoitwa kambini kwa aliyeibuka Mchezaji Bora wa msimu uliopita, Michael Madoya. Hakuna vile mtaniambia niwaelewe Mchezaji Bora kukosa kuitwa timu ya taifa. Haipo popote pale duniani, labda Kenya tu.

Ninachofahamua, mchezaji wa aina hiyo anaweza kukosa iwapo ni majeruhi au anazo sababu nyingine za kibinafsi.

Cha ajabu zaidi ni kwamba, timu zote mbili za taifa (kikosi cha vijana wasiozidi umri wa miaka 23 na timu ya wakubwa, Harambee Stars) zinaingia kambini, lakini cha kufurahisha ni kwamba hayupo pahali popote kwenye vikosi hivyo vyote viwili. Hapo basi narudia kwa mjadala wangu wa hapo awali. Je? Ilikuwa haki kwa yeye kupata kura kutoka kwa makocha na manahodha wa klabu zilizomfanya kutwaa tuzo ya Mchezaji Bora ama walitumia njia za panya kupeana tuzo?

Ukiangalia kiumri, ni wazi Madoya yupo katika anastahili kuitwa katika timu ya ya vijana wasiozidi miaka 23. Kukosa kwake kunanishangaza. Inamaana hakustahili kupewa hiyo tuzo ya Mchezaji Bora? Ama alipewa kimakosa? Ni maswali ambayo yanawaacha watu vinywa wazi. Ndio maana kila wakati mimi husema soka letu ni balaa.

Jambo jingine linaloleta utata ni kurejeshwa kwa aliyekuwa nahodha wa timu ya Taifa, McDonald Mariga, ndani ya kikosi hicho. Kwa upande wangu sioni sababu kwanini tupige kelele.

Mariga anacheza Ligi Daraja la Pili huko Hispania. Kimsingi daraja hilo hauwezi kulilinganisha na hata Ligi Daraja la Kwanza ya hapa, achilia mbali Ligi Kuu. Daraja hilo lipo juu. Kwa maana hiyo, uzoefu ambao Mariga anao, hakuna hata mchezaji mmoja kati ya walioitwa Stars anayemfikia. Kama huko Hispania anapiga soka lake vizuri tu, ni jambo gani litamzuia? Saa nyingine wapenzi wa soka lazima tuheshimu wachezaji wetu.

Kutowaheshimu wachezaji wetu ndio kunakoua soka letu polepole. Angalia kikosi hicho. Ni wachezaji wangapi wazoefu walioitwa. Wachache mno, Mariga akiwa mmoja wao.

Ni lazima kikosi chetu kiundwe na wachezaji wazoefu na wale chipukizi ambao wanaibuka sasa ili pia nao wajifunze mambo mawili matatu hivi. Timu yetu kwa muda sasa unapoitazama inaonyesha wazi kukosa kiongozi.

Kiongozi ninayemzungumzia hapa ni yule mwenye uwezo wa kusikilizwa na yeyote kikosini. Ni mchezaji ambaye mambo yakiharibika uwanjani yupo tayari kuita wenzake na kuwaelekeza huk nao wakiwa tayari kumsikiliza.

Ndugu zanguni, kwangu sioni tatizo lolote kwa Mariga kujumuishwa Harambee Stars. Ujana na uzee lazima uchanganywe katika kila jambo. Kuna semi husema ‘Palipo na wazee haliharibiki jambo’.

Wakenya mkae mkitambua kwamba kikosi kilichoteuliwa ni kizuri tu. Kina ule mchanganyiko wa wachezaji wengi wa kulipwa ambao wote natumaini wanacheza katika klabu zao. Utata ni pale tu Mchezaji Bora anapokosa kuitwa.

Lakini pamoja na ukweli kwamba kocha ndiye mteuzi na anafanya kazi kwa maono yake, pia tukumbuke kulikuwa na utata wakati tuzo hilo ikitolewa kwake. Wengi walisema hakustahili.

Kwa leo naomba kuishia hapa na mengine tutaongea wiki ijayo.