Afadhali Yanga imeachana na chui wa karatasi, Ngoma

Muktasari:

  • YANGA imekutana na mshambuliaji wake Mzimbabwe, Donald Dombo Ngoma.

YANGA imekutana na mshambuliaji wake Mzimbabwe, Donald Dombo Ngoma.

Wamekubaliana kuchana mkataba ambao upo mezani kwao na sasa kila mmoja amefuata njia yake. Nadhani ni kitu bora kwa kila mmoja wao.

Donald Ngoma, mshambuliaji mrefu na mwenye uwezo mkubwa alibakia kuwa Chui wa karatasi tu katika orodha ya wachezaji wa timu hiyo. Yeyote aliyemuongezea Ngoma mkataba mpya nadhani atakuwa anajisikia aibu.

Kilichotokea ni kwamba Yanga ilikuwa inajisifu tu kwamba ina mchezaji hatari anayeitwa Donald Ngoma lakini ukweli ni kwamba alibakia kuwa Chui wa karatasi tu. Chui ambaye haumi lakini anatisha kwa kumtazama tu.

Ngoma amecheza mechi nne tu msimu huu unaoelekea ukingoni na kufunga mabao mawili. Mashabiki wa Yanga wengi hawaelewi ni kitu gani kilikuwa kinamtokea Ngoma. Hii ni sifa ya kwanza kwa klabu au mchezaji ambaye anaendesha mipango yake ovyoovyo.

Mashabiki wa Yanga huwa wanalipa viingilio kutazama mechi zao. Viingilio hivyo ndivyo ambayo vinasaidia mishahara ya wachezaji. Uwingi wa mashabiki haohao ndio ambao unasababisha kampuni ziiipe Yanga pesa za udhamini. Kwanini pesa hazipelekwi Mtibwa Sugar? Kwanini iwe Yanga? Ni kwa sababu ya uwingi wa mashabiki.

Kwa heshima ya mashabiki ndio maana makocha wa klabu mbalimbali duniani hufanya mkutano na waandishi wa habari siku moja kabla ya mechi zao kuelezea ni wachezaji gani wanaopatikana katika mechi ya kesho na ni wachezaji gani hawapatikani katika mechi hiyo.

Wanaenda mbali zaidi kwa kusema ni kitu gani kinawasumbua wachezaji wasiokuwapo.

Kwa Ngoma, Yanga ilikuwa na kigugumizi kwa mashabiki na wanachama wake ambao ndio msingi mkuu wa klabu.

Mashabiki na wanachama walikuwa hawajui ni kitu gani kinaendelea kwa Ngoma. Walikuwa hawajui kama ni majeruhi, na kama ana majeraha ni ya aina gani, na yatachukua siku ngapi kumrudisha uwanjani.

Mwishoni walikuwa wamebakiwa na chui wa karatasi mkononi. Kila wakitazama orodha ya wachezaji wao wa msimu huu wanakutana na jina la Donald Dombo Ngoma.

Mshambuliaji hatari kutoka Zimbabwe ambaye ameifanyia makubwa timu hiyo katika miaka ya karibuni. Katika hali halisi maisha hayakuwa hivyo.

Inasemekana kwamba Ngoma ni kama vile alikuwa amesusa kuicheza Yanga. Umaskini wa Yanga hakuweza kukabiliana nao. Niliandika mahala wiki iliyopita jinsi ambayo Ngoma na wachezaji wa kigeni wa sasa walivyokuja na tabia tofauti na staa wa zamani wa Yanga, Nonda Shabani Papii.

Wakati Nonda alikuja nchini kwa ajili ya kupita, Ngoma amekuja nchini akiwa anaamini kwamba kwa Yanga yeye ndio amefika. Anaamini kwamba Yanga ni sehemu ambayo inapaswa kumpatia maisha.

Kwa sisi ambao tupo dunia ya tatu tunajua kwamba klabu zetu ni sehemu ya kupita tu kama alivyopita Nonda na baadaye Simon Msuva.

Wakati mwingine pia ni funzo kwa Yanga yenyewe. Ngoma amekula mishahara yao mingi na pia wanalazimika kumpatia mishahara ya miezi mitatu iliyobaki. Sidhani kama walimpa mkataba mpya kitaalamu kwa sababu walifanya hivyo kishabiki tu kutokana na kukabiliwa na presha kubwa kutoka kwa watu wa Simba ambao inasemekana walikuwa wanamuwinda Ngoma.

Kabla ya kuelekea katika msimu huu, Ngoma alikuwa hajaichezea Yanga kwa muda mrefu kutokana na kuwa na majeruhi kuhusu taarifa mbalimbali zikikinzana kuhusu hali ya majeraha yake.

Wengine walisema asingeweza kucheza tena na wengine walidai angeweza kucheza.