NYUMA YA PAZIA: Hakuna aibu tukimuomba msamaha Pep Guardiola

Muktasari:

  • Lakini kuna yule Mwanafsala mwingine aliyewahi kusema ‘Mwanaume shujaa ni yule anayesimama peke yake.’. ndiyo, kuna wakati unaamini unachokifanya. Unakisimamia unachokifanya. Unafia kwa unachokifanya.

SENECA the Younger, Mwanafalsafa wa Kirumi aliyezaliwa Hispania akafia Italia miaka mingi kabla ya Yesu, aliwahi kusema ‘Moto unaijaribu dhahabu, mateso yanajaribu wanaume mashujaa.. nadhani alisema kweli.

Lakini kuna yule Mwanafsala mwingine aliyewahi kusema ‘Mwanaume shujaa ni yule anayesimama peke yake.’. ndiyo, kuna wakati unaamini unachokifanya. Unakisimamia unachokifanya. Unafia kwa unachokifanya.

Wakati Manchester City ikifa mabao 4-0 jioni ya Januari 15 mwaka jana pale Goodson Park niliamini kwamba falsafa za soka la Pep Guardiola zisingeweza kufanya kazi tena soka la Kiingereza. City ilikuwa imetota kwa mabao ya Romelu Lukaku, Kevin Mirallas, Tom Davies na kinda Ademola Lookman.

Mateso kama haya ndio yanawaweka mashujaa majaribuni. Mateso kama haya ndio ambayo yalikuwa yanamuweka Pep katika majaribu ya kuachana na falsafa zake. Kumbe moyoni aliamua kusimama peke yake na kuamini alichokiamini

Kuanzia pale mpaka wikiendi iliyopita wakati Tottenham alipokufa mabao 3-0 pale Wembley na kuipa City ubingwa wake wa tano wa kihistoria, ni wakati wa kuinamisha kichwa, kufuata miguu ya Guardiola ilipo na kusema ‘Samahani’.

Ndiyo, ni kweli kwamba Jurgen Klopp ameonyesha kuwa kocha mwanaume kwa kumchapa Guardiola mara tatu ndani ya msimu mmoja. Mara moja katika ligi na mara mbili katika mechi za Ligi ya Mabingwa wa Ulaya. Hata hivyo, haibadili dhamira yangu ya kumuomba msamaha Pep kwa kumdhania tofauti.

Nilikuwa mmoja kati ya watu ambao waliamini kwamba Pep angefeli England na falsafa yake ya soka la Tikat. Soka Kiguardiola ambalo kila mmoja analifahamu. Mawazo yaliimarika wakati Pep alipoondoka katika msimu wake wa kwanza bila ya taji.

Msimu huu Pep ameondoka na mataji mawili akiwa katika falafsa ile ile. Kombe moja ni gumu zaidi. Ligi Kuu ya England. Amefanya nini zaidi? Kuna siri za ndani ambazo yeye anazifahamu zaidi. Binafsi nimegundua machache tu. Kwanza kabisa ukuta wake wa msimu uliopita wa kina Bacary Sagna, Pablo Zabaleta, Gael Clichy na Aleksander Kolarov ulikuwa umezeeka. Kila mmoja alikuwa amevuka miaka 30. Kazi yao ya kupanda na kushuka ilikuwa imepungua.

Pep aliingiza pesa nyingi katika ukuta, halafu kule mbele akawanunua Gabriel Jesus na Bernardo Silva. Zaidi nilichoona ni kwamba City waliongeza zaidi kasi ya mashambulizi na kuacha kuremba kwa pasi zaidi katika eneo la mwisho.

Wakati Barca ya Lionel Messi, Andres Iniesta na Xavi Hernandez ilikuwa ikikusogelea kwa pasi nyingi na wakiufungua ukuta wa jirani taratibu na kutumia akili nyingi, hawa kina Kevin de Bruyne, Raheem Sterling na Leroy Sane wana kasi zaidi na wanalazimisha zaidi katika eneo la hatari. Guardiola alishaona kwamba ni vigumu kupata kitu katika soka la Kiingereza bila ya kutumia mabavu (Aggressive football) katika eneo la mwisho. Maeneo mengine yote Pep aliendelea kutengeneza kikosi kinachomilika mpira na kuutawala kwa dakika zote 90 kama alivyofanya kwa Barca na Bayern Munich.

Guardiola anakaribia kuvunja kila rekodi katika Ligi Kuu ya England linapokuja suala la ubingwa. Ameitawala ligi hii na wengi tunaweza kuwa wanafiki kwa sasa lakini awali hatukuamini kama angeweza kufanya hivi katika soka la Kiingereza.

Waingereza walikuwa na maswali kuhusu Guardiola na staa wake Lionel Messi. Walikuwa wanauliza kama aina ya soka ya Pep ingeweza kufanya kazi katika usiku wa baridi siku ya Jumatatu katika pambano dhidi ya Stoke City. Amethibitisha kwamba ni kitu rahisi tu.

Na mpaka sasa wengi wamekuwa wakijiuliza kama Lionel Messi anaweza kung’ara katika Ligi Kuu ya England, hasa katika usiku wa baridi, ugenini katika uwanja wa Stoke City? Pep anaonekana kuwakilisha majibu ya swali hili. Kumbe inawezekana halafu ni rahisi tu.

Kwa mpira ambao Pep amecheza msimu huu na City kama ingekuwa mpira huo umechezwa na Liverpool, Arsenal, Man United au Chelsea basi si ajabu tusingelala mitaani. Ni vile tu City haina mashabiki wengi katika Afrika hasa Afrika Mashariki na kati.

Vinginevyo, City ni mabingwa waliostahili. Waliimaliza ligi mapema sana Novemba mwaka jana wakati Jose Mourinho alipoanza kulalamika kila kitu kuhusu mechi zake. Mara alalamikie wachezaji wake, waamuzi, makocha wa timu pinzani, mashabiki wake na kila kitu. Ilikuwa wazi kwamba asingewezeka kukimbizana na City mpaka mwisho wa safari.

Wakati akiwa Ujerumani bado sikumuamini Pep kwa sababu alikwenda katika ligi ambayo hata kocha wa Afrika angeweza kuchukua ubingwa na Bayern Munich.