Yanga hii dhaifu inastahili pongezi nyingi kwa kweli

Muktasari:

  • Hii si Yanga bora kwa kuiangalia uwanjani kama tulivyowahi kuvishuhudia vikosi matata zilivyopita pale Jangwani. Wala siyo Yanga iliyokuwa na mwalimu au kocha bora sana ukiangalia jinsi inavyocheza uwanjani hasa unapolinganisha na vikosi vingi vilivyopita hapo.

INAWEZA kuwa ni Yanga ya ajabu sana kwa misimu mingi iliyopita ukiilinganisha na vikosi vingi vya timu hiyo hasa kwa miaka ya karibuni.

Hii si Yanga bora kwa kuiangalia uwanjani kama tulivyowahi kuvishuhudia vikosi matata zilivyopita pale Jangwani. Wala siyo Yanga iliyokuwa na mwalimu au kocha bora sana ukiangalia jinsi inavyocheza uwanjani hasa unapolinganisha na vikosi vingi vilivyopita hapo.

Chukua vikosi vya Yanga kwa misimu isiyopungua saba au nane na makocha wenye sifa kubwa wamehusika kama vile Papic, Tom Saintfiet, Ernie Brandts, Marcio Maximo na Hans Van Pluijnm ambao wote hawa wamefaidi rutuba nzuri ndani ya Yanga wakiwa chini ya ufadhili wa bilionea, Yusuf Manji.

Vikosi hivyo vyote chini ya makocha hao wenye uzoefu wakiwa na wachezaji nyota waliokuwa waking’ara na timu hiyo hata kwenye kikosi cha Taifa bado hawakuwahi kuingia hatua ya makundi ya kombe la shirikisho zaidi yam waka juzi wakiwa na Pluijm.

Kumbuka kikosi cha Yanga cha kina Boniface Ambani, Juma Kaseja, Shadrack Nsajigwa, Abdi Kassim, Athumani Idd, Nurdin Bakar, Jerrison Tegete, Mrisho Ngassa, Kigi Makasi ambao hawa wote walikuwa moto kwenye kikosi cha timu ya Taifa ya Tanzania.

Angalia kikosi cha awali cha Pluijm ambacho kilicheza na kuchukua ubingwa wa Ligi Kuu kwa msimu wa 2014/2015 kikijazwa na wachezaji wengi wenye uzoefu kama Nadir Haroub ‘Cannavaro’, Mrisho Ngassa, Amissi Tambwe na wengineo lakini hata hivyo hawakuweza kupenya kwenye hatua kama hii ya makundi kombe la Shirikisho Afrika.

Vipo vikosi vingine bora sana vilivyopita pale Yanga kwa miaka mingi hasa baada ya mfumo wa makundi kuanzishwa kwa mara ya kwanza mwaka 1998 na kuendelea mbele.

Sikumbuki kama kuna mwaka au msimu ambao Yanga haijawahi kuiwakilisha nchi kwenye michuano ya kimataifa iwe ni ya Ligi ya Mabingwa Afrika ama Kombe la Shirikisho bado vikosi hivyo havikuingia hatua kama hii. Kwa nini sasa Yanga hii yenye kusadikika kuwa ina kikosi cha kawaida kisichokuwa na ubora lakini bado kimeweza kupenya hadi hatua ya makundi ya kombe la Shirikisho Afrika kwa mara ya pili ndani ya miaka mitatu isipewe pongezi za dhati kabisa kutoka kwa Watanzania wote wenye itikadi tofauti!

Kwanza lazima tukubali kuwa michuano hii ya Shirikisho na ile ya Ligi ya Mabingwa Afrika ndio michuano mikubwa kuliko yote, ikimanisha kuwa zile klabu bora zote Afrika hushiriki michuano hii mikubwa.

Haijalishi Yanga ilipangwa na nani bado timu zilizocheza na Yanga ni bora kati ya timu kadhaa za Afrika na kwa maana hiyo Yanga hii ina ubora mkubwa ndani ya bara letu.

Lakini pia tukubali kuwa Yanga hii haikuwa na kikosi chenye wachezaji bora kivile.

Iangalie Yanga ile iliyocheza dhidi ya Welaytta Dicha katika mchezo wao wa kwanza hapa Dar es Salaam na ni Ibrahim Ajibu, Hassan Kessy na Rafael Daudi ndio pekee wanaopatikana kwenye kikosi cha timu ya Taifa huku wachezaji wengine wakiwamo hata wale wa kigeni hawapo kabisa hata kwenye vikosi vya akiba vya timu zao za Taifa.

Ukiachana na matatizo ya nje ya uwanja bado kikosi hiki cha Yanga kinaendelea kujengwa na wachezaji wasio na uzoefu na michuano hii labda jina la Yanga lakini ukimuangalia Rafael Daudi, Pius Buswita, Yussuf Mhilu, Emmanel Martin, Abdallah Shaibu, Hassan Kessy, Youthe Rostand na wengineo hawa wote hawajawahi cheza kwa muda zaidi ya msimu mmoja au miwili kwenye michuano hii ya Afrika ingawa ushiriki wao umekuwa wakutukuka.

Swali kubwa kwa sasa ni nini ilikuwa silaha ya kikosi hiki kilichoonekana si cha ushindani machoni mwa watu wengi kuweza kufanya maajabu. Yanga hii baada ya kujitambua na kuona uwezo wao kwa mchezaji mmoja mmoja ni mdogo iliamua kitu kikubwa cha kwanza kuifanya timu kucheza Pamoja.

Yanga hii haikuwa na nyota hata mmoja ndani ya uwanja na wachezaji wote walijituma kucheza kwa umoja na kujituma sana wakitambua kuwa kutolewa kwao kutawafanya wasiwe na kitu cha kufanya huko mbeleni.

Hiyo ni kwa sababu mchuano ya ndani kuanzia Ligi Kuu msimu huu ushindani umekuwa mkubwa na Simba wameshajizatiti kwenye nafasi ya kwanza kwa muda sasa.

Kitu cha pili ambacho unaweza kukiona kwa kikosi hiki cha Yanga haijalishi kuwa leo wanaweza kumkosa mchezaji mmoja wapo muhimu kama ilivyotokea kwenye mchezo wa kwanza wa raundi ya kwanza ya mtoano hapa Dar dhidi ya Dicha wakiwakosa Juma Makapu, Kelvin Yondani, Papy Kabamba na Obrey Chirwa bado wachezaji wanaopewa majukumu ndani ya uwanja wanayatimiza pasipo hofu huku wakijituma sana.

Cha mwisho walichonacho Yanga hii ni kuwa wamekuwa wakiyasahau matatizo yao mengi nje ya uwanja kisha wamekuwa wakicheza kwa mbinu sana ndani ya uwanja, wakiamua kuzuia wanazidi kwa mbinu nyingi wakiamua kushambulia wanashambulia kwa mbinu nzuri huku wakizitumia nafasi chache muhimu wanazo pata kufanikisha ushindi wa timu yao.