Yale mabao 100 ya Messi ndo haya

Muktasari:

Jumatano iliyopita aliwafungashia virago vyao Chelsea huko Nou Camp wakati alipofunga mabao mawili, yote yakipita katikati ya miguu ya kipa Thibaut Courtois na kupika jingine, lililofungwa na Ousmane Dembele.

BARCELONAHISPANIA. JANA, Ijumaa supastaa Lionel Messi alikuwa akisubiri tu kufahamu anapangiwa na timu gani kwenye hatua ya robo fainali ya Ligi ya Mabingwa Ulaya na kikosi chake cha Barcelona ili akaendelee kufanya mambo yake.

Jumatano iliyopita aliwafungashia virago vyao Chelsea huko Nou Camp wakati alipofunga mabao mawili, yote yakipita katikati ya miguu ya kipa Thibaut Courtois na kupika jingine, lililofungwa na Ousmane Dembele.

Hayo yalikuwa maajabu ya mechi, ambaye kwa mabao hayo alikuwa amefikisha 100 kamili kwenye Ligi ya Mabingwa Ulaya. Messi sasa anakuwa mchezaji wa pili kuongoza kwa mabao kwenye michuano hiyo nyuma ya Cristiano Ronaldo, aliyefunga mabao 117.

Kwa Barca, Messi ndiye anaoongoza kwa mabao akimwacha mbali Mbrazili Rivaldo mwenye mabao 22, aliyofunga katika mechi 43 alizocheza kwenye Ligi ya Mabingwa Ulaya akiwa na kikosi hicho.

Messi anashika namba mbili pia kwenye orodha ya wachezaji waliofunga mabao mengi kwenye Ligi ya Mabingwa Ulaya wakiwa na timu moja, akiwa tena nyuma ya Ronaldo, mwenye mabao 102 aliyofunga akiwa na kikosi cha Real Madrid.

Makala haya yanahusu jinsi Messi alivyofunga mabao yake 100 kwenye Ligi ya Mabingwa Ulaya na jana ilitarajiwa kupangwa ratiba ya robo fainali ya wababe hao.

Supastaa huyo wa Kiargentina, katika mabao yake hayo 100 alivyoyafunga, ametikisa nyavu mara 81 kwa mguu wake wa kushoto, mabao 15 kwa mguu wa kulia na mara nne alifunga kwa kichwa, likiwamo lile bao lake matata kabisa alilowafunga Manchester United kwenye fainali iliyofanyika Rome, Italia.

Messi ameonekana kuwa hatari zaidi anapokaribia goli na ndiyo maana mabao yake alifunga, 86 amefanya hivyo akiwa ndani ya boksi, wakati nje ya boksi amefunga mabao 14. Kwenye mabao hayo, Messi amefunga penalti 11 tu na mipira ya adhabu, yaani friikiki amefunga mara tatu. Kwa taarifa yako tu, Messi ni hatari zaidi kwenye kipindi cha pili licha ya kwamba amefunga idadi ya mabao ambayo haikuyaacha sana mabao yake ya kipindi cha kwanza.

Messi amefunga mabao 51 katika kipindi cha pili na mabao 49 katika kipindi cha kwanza.

Staa huyo wanayemwona kuwa mfalme huko Nou Camp, amefunga mabao 57 katika uwanja huo kwa mechi za Ligi ya Mabingwa Ulaya, huku ugenini akifunga 41 na uwanja wa neutro, kafunga mara mbili, yote yakihusisha kwenye fainali dhidi ya Man United ile ya kwanza uwanjani Stadio Olimpico, Rome Italia na Wembley, England.