HISIA ZANGU: Soka letu limejaa mameneja feki wa wachezaji wa mitaani

Muktasari:

Neno ‘meneja’ limeanza kushika kasi kwa wachezaji wetu na hata katika vyombo vya habari.

INAFURAHISHA sana siku hizi. Mkamate mkono mchezaji yeyote yule wa Ligi Kuu, hasa katika klabu za juu lazima atakwambia ana meneja wake. Neno ‘meneja’ limeanza kushika kasi kwa wachezaji wetu na hata katika vyombo vya habari.

Utaelezwa mchezaji fulani meneja wake ni jamaa fulani hivi. Kimekuwa kitu cha kawaida. Kwanini mameneja wameibuka kwa kasi? Ni kwa sababu mchezo wa soka nchini nao umeanza kubadilika. Siku hizi wachezaji wana mikataba tofauti na zama za kina Zamoyoni Mogella.

Hata hivyo, mameneja wa wachezaji wetu ni tofauti na mameneja wa nchi za wenzetu. Mameneja wetu wana tabia tofauti. Kwanza huwa wanajitokeza pindi wanaponusa kuwa mchezaji wake anatakiwa na klabu nyingine. Inakuwa raha anapotakiwa na Simba, Yanga au Azam.

Kama hatakiwi na klabu hizo basi hauwezi kumjua meneja wa mchezaji husika. Lakini hapo hapo nikachunguza jinsi wachezaji wanavyowapata mameneja wetu. Nimegundua kuwa ni washkaji tu ambao wana uwezo kidogo wa pesa mtaani ambao wanaweza kuwaongezea pesa ya kodi ya nyumba au kuwanunulia viatu vya mpira. Baada ya hapo wanajiita mameneja.

Kuna mambo yanakera kutoka kwa mameneja hawa. Kwanza kabisa huwa hawajui mipango ya soka inavyokwenda. Meneja hajui jinsi ya kumpatia mchezaji wake timu nje ya nchi, hajui kutumia mtandao.

Meneja hajui kufungua mawasiliano na timu za nje. Meneja hana hata barua pepe. Lakini bado anajiita meneja. Meneja hafahamu hata mawasiliano ya mawakala wa nje wanaosaka wachezaji lakini bado anajiita meneja. Matokeo yake kipaji cha mchezaji wake kinafia mikononi mwake.

Kwa namna hii, mchezaji anajiona yupo salama katika mikono ya meneja ambaye kumbe anadumaza kipaji chake. Anamuamini sana kwa sababu anamsaidia katika pesa ndogondogo pindi akiishiwa. Mchezaji anaendelea kukaa chini ya meneja feki ambaye hana hata mkanda wake unaomuonyesha akitamba uwanjani.

Ukitaka kwenda kumsaidia mchezaji husika baada ya kuona ana kipaji cha kufanya mambo makubwa siku za usoni atakwambia ana meneja wake. Ukienda kwa meneja wake anaanza kukudanganya mambo mengi ya uongo. Lakini wakati mwingine afadhali hata anayedanganya kuliko ambaye hajui lolote kuhusu namna ya kumsaidia mchezaji wake.

Hapo hapo kuna mameneja wengine ambao wapo kwa ajili ya zile siku za mchezaji kusaini mkataba mpya. Hana mpango wowote wa kumtafutia mchezaji wake timu ya nje ya nchi, lakini akisikia mchezaji wake anamaliza mkataba wake na klabu yake inataka kumuongezea mkataba mpya, basi meneja anaibuka ghafla.

Wakati umefika sasa wachezaji wetu watafutiwe miongozo na watu ambao wanafahamu mambo haya. Soka ni biashara kama zilivyo biashara nyingine. Tuache masihara katika mambo ya msingi. Katika nchi za wenzetu, meneja anaacha kila kitu kwa ajili ya kufanya kazi ya mteja wake ili apate pesa ya uhakika. Hakuna muda wa kuzuga. Jaribu kuona jinsi wachezaji wetu walivyo na nidhamu mbovu, lakini bado wanadai wana mameneja. Meneja wa uhakika unaruhusu vipi mchezaji wako awe na nidhamu ya ovyo wakati unajua wazi kwamba kipaji chake ni biashara yako?

Umefika wakati sasa tuache masihara katika mchezo huu. Meneja wa kweli lazima atahaha katika mambo mawili. Kwanza kabisa atahakikisha mchezaji wake yupo katika kiwango bora muda wote. Lakini pia atahakikisha anamtafutia timu nje ya nchi kwa ajili ya mkataba mnono au kwa ajili ya kuhakikisha kipaji chake kinafika mbali zaidi.

Jaribu kuchunguza. Barani Ulaya mchezaji akiwekwa sana benchi meneja wake au wakala wake anaibuka na kulalamika hadharani kwamba mchezaji wake anabaniwa. Hapa nchini haijawahi kutokea hata siku moja meneja wa mchezaji akajitokeza hadharani kudai mchezaji wake anabaniwa au anaonewa. Hata hivyo, wakati wa pesa ya mkataba mpya ikikaribia basi anaonekana.

Nawaomba watu wanajiofahamu sana, waliokwenda shule, waanze kuangalia fursa upya katika soko hili la wachezaji. Wasitishwe na mameneja wengi feki waliopo mitaani ambao hawana msaada wowote. Hawawezi kuwapeleka wachezaji wetu mbali zaidi ya kuwadanganya tu na visenti vidogo.