NYUMA YA PAZIA: Wote mnakaribishwa katika filamu ya Kane

Saturday October 7 2017

 MCL

By Edo Kumwembe

KWA sasa ni kama vile tupo katika ule ukumbi wa sinema wa Mlimani City. Kando yetu tuna pop corn, kando yetu pia tuna juisi. Tumekaa kimya tukisubiri filamu ianze. Filamu ya Harry Kane. Naitazamia kuanza mwishoni mwa msimu huu.

Itakuwa filamu hasa. Kwa sasa hakuna mshambuliaji hatari wa kati duniani zaidi ya Kane. Luis Suarez kashuka. Sergio Aguero na Romelu Lukaku ni hatari, lakini kwa misimu miwili sasa wanacheza ligi moja na Kane ambaye bado anaibuka kuwa mfungaji bora. Namba hazidanganyi.

Unajaribu kumuwaza Pierre-Emerick Aubameyang, akili inakataa. Unamuwaza Pablo Dybala, lakini akili inakataa pia. Kane ni hatari kwa sasa. Ndani ya mwaka huu amefunga hat trick sita. Inabidi ukubali tu kwamba ni mshambuliaji bora wa kati kwa sasa. Kama si Ulaya au duniani, basi hata kwa England.

Ana umri wa miaka 24. Anachezea Tottenham. filamu itaanza pale ambapo Kane ataambiwa kisha kujiambia mwenyewe kuwa hauwezi kuwa staa mkubwa kwa kuchezea Tottenham Hotspur. Lazima uende kwa watu wanaoweza kukupa mataji.

Mara ya mwisho Tottenham kuchukua ubingwa wa England ilikuwa ni Mei 1961, miezi sita kabla ya Uhuru wa Tanganyika. Mara ya mwisho, Tottenham kuchukua Kombe la FA ilikuwa ni Mei 1991, miaka miwili baada ya kuvunjwa kwa Ukuta wa Berlin pale Ujerumani. Mchezaji staa hawezi kucheza timu kama hii.

Lakini hapo hapo kumbuka kuwa mchezaji staa kama yeye hawezi kulipwa mshahara wa Pauni 100,000 tu kwa wiki kama ambavyo Tottenham imeweka katika kiwango cha mwisho kabisa cha mshahara miongoni mwa mastaa wake.

Filamu itakuwa nzuri kwa sababu Kane hatakubali kulipwa kiasi hicho huku akiwa mchezaji mkali zaidi katika Ligi Kuu England wakati akina Paul Pogba na Eden Hazard wanalipwa Pauni 250,000 kwa wiki.

Mwisho wa siku kwa haya mawili, Kane ataianzisha filamu ya kwenda katika timu kubwa zaidi ya Tottenham. Mwanadamu anaishi mara moja tu. Mshambuliaji wa aina ya Kane kwa sasa anastahili kwenda Manchester United, Real Madrid au Barcelona. Samaki mkubwa ananaswa na ndoana kubwa. Baada ya hapo Filamu ya Kane itachagizwa zaidi na Real Madrid. Nasikia imeanza kumzungumzia. Tangu lini Madrid ikamkosa mchezaji inayemtaka? Ilimtaka Luis Figo ikampata, ikamtaka Zinedine Zidane ikampata, ilimtaka Ronaldo orijino ikampata. Ilimtaka Ronaldo wa leo na ikampata.

Kuna kila sababu ya Rais wa Madrid, Florentino Perez, akamtaka Harry Kane. Kwanza kabisa kwa msimu wa nne sasa tangu amsajili Gareth Bale hajaingia sokoni kuionyesha dunia makali yake. Amekaa kimya kama simba aliyeshiba. Na mashabiki wake wamekaa kimya kwa sababu hawana njaa ya mataji tena, hasa lile la Ulaya.

Rekodi nne za dunia zimevunjwa bila ya yeye kuhusika. Bei za Paulo Pogba, Ousmane Dembele, Kylian Mbappe na Neymar zote zimesimama juu ya mchezaji wake wa mwisho ghali ambaye alimnunua, Gareth Bale. Sidhani kama anafurahia ujinga huu.

Kwa sasa kuna kitu kimepungua pale mbele katika safu yake ya BBC ya Bale, Benzema na Cristiano. Hasa Benzema ambaye amekaukiwa mabao tangu msimu uliopita. Hapa ndipo unapoweza kujumlisha moja na moja ukapata mbili. Perez kumtaka Kane inawezekana.

Kitu kikubwa cha kusisimua kinakuja katika upande wa mwisho kabisa wa filamu hii. Tottenham yenyewe. Mwenyekiti wake, Daniel Levy, anatajwa kuwa bosi mgumu zaidi katika mazungumzo ya kuuza mastaa wake kama ilivyo kwa bosi wa Lyon ya Ufaransa, Jean Michael Aulas.

Kawaulize watu wote wanaowataka mastaa wa Tottenham wakwambie jinsi wanavyohenyeka kuzungumza na Levy. Ndio maana kabla hata soko halijaharibika Levy alimuuza Bale kwa dau la Pauni 85 milioni. Hakuwa mchezaji wa bei hiyo.

Ndio maana leo, Kyle Walker, ingawa Kocha Mauricio Pochettino hakumtaka kikosini kwake, lakini Levy kamuuza kwa bei ghali zaidi miongoni mwa mabeki.

Akina Dimitar Berbatov, Luka Modric, Michael Carrick wote walinunuliwa kwa bei rahisi, lakini waliuzwa kwa bei kubwa baada ya mazungumzo ya muda mrefu ya kibishi kati ya Levy na wateja wake. Anajulikana kama ‘The Toughest Negotiator’ katika mambo ya uhamisho.

Sasa hivi mkononi ana mfungaji bora wa Ligi Kuu England mara mbili mfululizo. Ana uwanja mpya unaokuja ambao utahitaji wachezaji wa aina ya Kane kwa ajili ya kuujaza kila wikiendi. Hapo ndipo utakapomtaka Daniel Levy.

Wakati Levy atakapokutana na Perez itakuwa filamu ya kusisimua sana. Wakati Kane atakapomwambia Levy kuwa anataka kuondoka itakuwa filamu ya kusisimua pia. Tumaini pekee ambalo linabakia katika dili hili ni labda kama Levy ataamua kurudisha pesa zake za mkopo wa ujenzi wa uwanja kwa kukubali kumuuza Kane chapuchapu.

Vinginevyo kwa sasa sisi wengine tupo tayari kusubiri kwa hamu filamu hii ya Harry Kane. Tuna pop corn zetu tumetulia katika viti. Kitu ambacho nina uhakika nacho, kama Kane atauzwa, basi atavunja rekodi ya uhamisho wa dunia.