MAONI: Yanga, Simba zipigane kiume kusonga mbele mechi za CAF

Muktasari:

Yanga ipo Botswana ambapo jioni ya leo itakuwa wageni wa Township Rollers mjini Gaborone katika mechi ya marudiano ya raundi ya kwanza ya Ligi ya Mabingwa Afrika.

SIMBA na Yanga zipo ugenini katika nchi tofauti zikitafuta heshima kwenye michuano ya kimataifa, inayosimamiwa na Shirikisho la Soka Afrika (CAF).

Yanga ipo Botswana ambapo jioni ya leo itakuwa wageni wa Township Rollers mjini Gaborone katika mechi ya marudiano ya raundi ya kwanza ya Ligi ya Mabingwa Afrika.

Watani wao, Simba wenyewe watashuka uwanjani usiku kwenye mji wa Port Said, Misri kukabiliana na wenyeji wao Al Masry katika mechi ya Kombe la Shirikisho Afrika.

Kama ilivyo kwa Yanga, Simba nayo ni mchezo wake wa marudiano ya raundi ya kwanza, baada ya awali wiki moja na ushei kulazimishwa sare ya 2-2 nyumbani.

Yanga yenyewe inarudiana na Rollers ikiwa na deni la kipigo cha mabao 2-1 ilichopewa nyumbani katika mechi yao ya kwanza.

Kwa hakika mechi zote ni ngumu kwa wawakilishi wetu kwa kuzingatia matokeo ya mechi zao za awali nyumbani, tena ni angalau Simba wana nafuu kwa sare kuliko kipigo cha Yanga.

Hata hivyo, kwa kurejea rekodi za mechi za klabu zetu dhidi ya timu za Afrika Kaskazini, unaweza kuona jinsi gani Simba ilivyo na mlima mkubwa wa kuupanda kulinganisha na Yanga.

Timu zetu zimeondoka nchini zikipishana saa tu, Yanga ikitangulia kuondoka usiku wa kuamkia Jumanne, ilihali Simba ikitimka kwenda Misri jioni ya Jumatano, huku kila moja ikiwa na matumaini makubwa ya kufanya vema.

Inawezekana wapo wadau wa soka nchini wamezikatia tamaa timu zetu katika kusonga mbele kupitia mechi hizo, lakini ukweli soka ni mchezo wenye maajabu yake na timu zetu zina nafasi ya kusahihisha makosa ya mechi zao za nyumbani.

Tunaamini makocha wa timu zote mbili kwa maana Pierre Lechantre na Msaidizi wake, Masudi Djuma wa Simba na George Lwandamina na Shadrack Nsajigwa wa Yanga waliyasoma makosa yaliyojitokeza katika mechi za awali na kurekebisha.

Kama walibaini makosa yaliyowagharimu katika mechi zao za nyumbani na kisha kuyafanyia kazi mapema kabla ya kusafiri ni dhahiri timu zetu zina nafasi ya kupindua matokeo.

Wachezaji watakaopewa jukumu la kuzipigania timu hizo katika mechi za leo, ni lazima watambue macho na masikio ya Watanzania yapo kwao.

Lazima wajue hatma ya Yanga kuingia makundi au Simba kusonga hatua inayofuata ipo mikononi mwao, hivyo wapambane.

Kama Township iliifunga Yanga Uwanja wa Taifa mbele ya mashabiki wao, kitu gani kitawazuia vijana hao wa Jangwani wasishinde Gaborone?

Iwapo kama Al Masry iliweza kuwabana Simba nyumbani na kupata sare kwa kuchomoa mabao ya Wekundu wa Msimbazi, iweje iwe vigumu kwa wawakilishi wetu hao kupata matokeo chanya?

Tunaamini ushindi katika soka hupatikana kokote bila kujali timu ipo nyumbani au ugenini.

Mara ngapi tumeshuhudia timu zikipata matokeo ya kustaajabisha ugenini? Simba yenyewe mwaka 1979 iliwashangaza Mufulira Wanderers ya Zambia katika michuano hiyo ya Afrika.

Simba ilicharazwa mabao 4-0 jijini Dar es Salaam na kila shabiki aliamini biashara ilishamalizika, lakini Simba iliitoa nishai Mufulira mbele ya Rais wa Zambia wa enzi hizo, Kenneth Kaunda kwa kuwacharaza wenyeji 5-0 na kusonga mbele.

Hivyo, Mwanaspoti tunaungana na wote wanaoamini timu zetu zitavuka salama leo.

Kitu cha muhimu ni namna timu hizo zilivyojipanga na kujiandaa vipi kukabiliana na wenyeji wao, kwani kama kila kitu kitakuwa kimeenda sawa kwanini timu zetu zisishinde?

Bahati nzuri Simba na Yanga zinashiriki michuano kwa msimu huu zote zikiwa chini ya makocha wenye uzoefu wa soka la Afrika.

Rekodi za Lechantre na Lwandamina katika michuano ya Afrika hazidanganyi, ndio maana tunaamini kuwa, Simba na Yanga kuvuka zikiwa ugenini ni suala la nyota wake kuamua uwanjani.

Kama wataingia uwanjani wakiwa na hofu na kukata tamaa, ni rahisi kujikuta wakiishia njiani, hata kama Yanga bado ina nafasi ya kushiriki Kombe la Shirikisho hatua ya 16 Bora.

Vilevile kama watashuka uwanjani wakiamini kuwa wao ni majemedari walioaminiwa na Watanzania katika mechi hizo na hivyo kupambana kiume ni wazi timu zetu zitafuzu. Kazi kwao!