Watanzania tunasubiri medali, Bayi ametuletea zawadi!

Muktasari:

  • Tunaridhika tu tukiwasikia wawikilishi wetu wanaokwenda kushiriki mashindano ya kimataifa wakirudi huku wakijitetea kwa visingizio kibao. Hapo tunakuwa tumesharidhika hatutaki kujisumbua kuhoji wajipange kivipi na kwa mikakati gani?

KUNA muda mwingine huwa najiuliza hivi sisi Watanzania tuna tatizo gani? Mbona tunaridhika kirahisi bila kuhoji!

Tunaridhika tu tukiwasikia wawikilishi wetu wanaokwenda kushiriki mashindano ya kimataifa wakirudi huku wakijitetea kwa visingizio kibao. Hapo tunakuwa tumesharidhika hatutaki kujisumbua kuhoji wajipange kivipi na kwa mikakati gani?

Kuna sehemu Watanzania tunatakiwa tuikumbushe serikali kuwa michezo ni sehemu sahihi ya maendeleo kama ilivyo zilivyo nyanja nyingine.

Nakumbuka Mwalimu Nyerere aliwahi kusema: ‘Nchi inatakiwa kujikomboa katika nyanja tatu kubwa za kiuchumi, kijamii na kisiasa.’

Huku kwenye siasa na kiuchumi kunaeleweka lakini hii ya tatu ‘kijamii’ unaitoa vipi michezo kwenye nyanja hiyo? Kwa hivyo, nchi inatakiwa itupie macho ya karibu kufuatilia maendeleo ya michezo nchini na faida zake.

Hakuna ubishi serikali inatakiwa iisaidie nyanja hii ya michezo na kuhakikisha uwakilishi wowote wa kikundi kimojawapo cha michezo iwe soka, mpira wa pete, wavu sarakasi na mchezo mwingine unaofanywa kimataifa unakuwa chini ya uangalizi na usimamizi wa serikali kwa nanma yoyote ile.

Kwa hiyo maandalizi ya vikundi vya michezo kama vile vinavyokwenda kushiriki Olimpiki, Jumuiya ya Madola, Kombe la Dunia au lile la Afrika yote yanatakiwa kuratibiwa na kusimamiwa na serikali kwa ukaribu.

Hapo ndipo nchi inapoweza kuchukua hatua na rungu la kuviwajibisha vikundi hivyo vya michezo kwa kushindwa kutoa mafanikio chanya.

Hata hivyo, kuna vitu ambavyo sisi kama wasimamizi wa vikundi hivyo kwa maana ya vyama, mashirikisho na klabu tunatakiwa tuongeze moja kabla ya kupata mbili kutoka serikalini. Kwa mfano sisi makocha tunatakiwa tuzalishe wachezaji mahiri wa viwango cha dunia kuweza kufanya vizuri kwenye michuano ya ndani na nje ya nchi.

Ni vizuri kocha wa mpira wa miguu kujivunia vijana kadhaa ambao wanaweza kuwa wamepitia kwenye mikono yake na vijana hao kufanya vizuri kitaifa na kimataifa.

Mfano tunao watu wazee wetu wengi maarufu kwenye michezo wachache kwa kuwataja ni Kanali Mstaafu wa Jeshi la Wananchi wa Tanzania, Idd Omary Kipingu na Mwanariadha wa zamani, Filbert Bayi.

Hawa wote wameweza kuziongoza taasisi za shule ambazo ndani yake kuna chimbuko la wanamichezo, kwa kifupi shule za michezo za Kipingu akiwa na Makongo kwa sasa anaiongoza Shule ya Lord Baden Powell huku Bayi akiwa na shule yake ya Filbert Bayi.

Kipingu alikuwa ni mwanasoka ambapo kupitia eneo lake kwa jumla amekuwa mkombozi mkubwa wa soka la Tanzania kwa sehemu kubwa baada ya kuwatengeneza wachezaji wengi mashuhuri wa soka kupitia shule yake.

Soka ni mchezo wa pamoja ambao matokeo ya timu ndio huonyesha ufanisi wa wachezaji hao. Kwa Kipingu anaweza kuwa kwa asilimia kubwa ameilipa fadhila nchi kwa kuwa wengi wa wanafunzi wake wamekuwa chachu kubwa ya ujenzi wa mafanikio ya Timu ya Taifa, Taifa Stars.

Mwaka 2009 Tanzania iliposhiriki fainali za Chan kule Ivory Coast idadi kubwa ya wachezaji waliounda timu ya taifa walipitia na kuimarishwa kwenye mikono ya Kanali Kipingu, wachezaji kama Juma Jabu, Henry Joseph, Haruna Moshi, Jerry Tegete, Kigi Makasi na wengineo huyu ameilipa nchi vizuri.

Kwa upande wa Filbert Bayi bado ana deni na si kwa sababu yeye ni Katibu Mkuu wa Olimpiki tu, ikionekana ndipo awajibike hapana!

Bayi hivi majuzi ametuletea zawadi ya nishani ya heshima kutokana na ushiriki wake hususan ule wa mwaka 1974 alipovunja rekodi kwenye mbio za mita 1500 na kuipa nchi medali ya dhahabu.

Ametuletea zawadi hiyo ikiwa imepita miaka zaidi ya 40 sasa. Lakini Watanzania naa wanamichezo tunamuona kiongozi huyo kama vile bado ana deni la kuipa urithi nchi kwenye eneo hilo.

Sisi hatukuwa tunaisubiri nishani yake ya heshima pale Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa JN, tulikuwa tunazisubiri medali tu kutoka Austria. Bayi ana deni kwa kuwa hajawahi kumtengeneza Bayi mpya kwa miaka yote hiyo 40. Kuitengeneza timu ya mpira wa miguu ni kazi kubwa kuliko kumtengeneza Bayi kwa miaka 40.

Labda tuamini tu, kiongozi huyo hajaamua kutuachia Bayi mwingine. Tunaamini ana uwezo mkubwa mno hata wa kumgharamia au kuwagharamia vijana hata kumi kwa umaarufu wake akawatafutia wadhamini wakaishi Ethiopia, Kenya hata Marekani wakiwa na umri mdogo miaka hata 12 hivi wakakua na kufanya mazoezi ndani ya miaka mitano tayari watakuwa wameshaanza kupevuka na kuonesha taa ya matumaini ya kumpata Bayi mwingine.

Nasema kwa miaka yote hii Bayi na wenzake kina Mzee Gidmas Shahanga na wengineo wengi hivi leo Watanzania wapenda michezo tusingefika uwanja wa ndege kumpokea Bayi na kumpa mashada ya maua mengi badala yake mashada hayo tungeyajaza shingoni mwa wanamichezo wetu.