Media zinachangia kuzibania Simba,Yanga

Tuesday May 8 2018

 

By BONIFACE AMBANI,NAIROBI

YOUNG (Yanga) Africans imeondoka juzi kwenda Algeria kucheza mchezo wake wa hatua ya makundi Kombe la Shirikisho barani Afrika bahati mbaya kwao imekwenda huko bila wachezaji wake wanne muhimu mno kwa sasa kwenye timu hiyo...

Kelvin Yondani, Papy Kabamba Tshishimbi , Obrey Chirwa na Ibrahim Ajibu hawa wote ni wachezaji wa kikosi cha kwanza ( pigo kwao ).

Katika mchezo huo uliochezwa Jumapili usiku, mjini jijini Algeries, Yanga imefungwa mabao 4-0.

Kisa na mkasa ni kukosekana kwa wachezaji hao. Vyombo vya habari vya Tanzania vinafahamu kilichowafanya wachezaji hao wasiongozane na wenzao huko Algeria ni ukata.

Young African kwa sasa imepita kwenye kipindi kigumu mno lakini sioni media zikiwapigia simu wazee wanaopinga mabadiliko kuwauliza wanajisikiaje wachezaji hao kugoma kwa sababu ya kukosa stahiki zao? Wawapigie wasikie wanachangia nini ili kupunguza hata robo ya madai ya wachezaji hao

Msiwe mnawapigia kina Mzee Akilimali pindi anapojitokeza mwekezaji tu, hata timu zinapokumbwa na ukata ili tuwasikie misimamo yao

Media nyingi ndio chanzo cha migogoro kwenye klabu zetu hasa hizi mbili za Simba Sports Club na Young Africans kwa kuwa wao ndo huwapa vichwa kina Katibu wa Baraza la Wazee, Ibrahim Akilimali na Hamisi Kilomoni ambaye alikuwa katika Baraza la Udhamini la Simba na kuwapa nafasi kubwa utadhani wao ndio wamiliki wa klabu hizo.

Mzee Akilimali ni mmoja tu na kura yake ni moja tu kama ilivyo kwa Salum Mkemi au Ally Mayay kumgeuza yeye kama ‘final say’ hamtendi haki zaidi ya kumfanya ajione yeye ni bora na muhimu kuliko wengine kama wachezaji wa zamani kina Kenneth Mkapa, Fredd Felix Minziro, Edibily Lunyamila ambao wao walivuja jasho kwa ajili ya kuipigania Young Africans tena wakati mwingine walilazimika kucheza wakiwa wamedungwa sindano za ganzi.

Simba nayo imepanga kufanya Mkutano Mkuu Mei 20, agenda ya mkutano huo bado haijawekwa wazi lakini media zinahisi moja ya agenda hizo ni suala la kumkabidhi timu hiyo Mwekezaji, Mohammed Dewji ambaye inafahamika uwepo wake unaenda kuipa klabu hiyo ubingwa wa Vodacom baada ya miaka takribani minne.

Lakini cha ajabu watangazaji kama kawaida yao wamempigia simu Mzee Kilomoni ambaye kwa sasa hana cheo chochote ndani ya Simba yupo kama Abubakar Mohamed Mbwana tu

Kwani yeye ndo nani? Hana tofauti gani na Ismail Aden Rage au Mtemi Ramadhani kwa nini hamuwatafuti watu hao!

Hakuna wanachama wengine wanaoweza kutoa maoni yao lazima yeye tu lengo lenu ni nini ? Mnajua kama yeye hataki mabadiliko kwa kuwa maslahi yake yatakuwa shakani, hivyo kumtafuta kwenu mnaonyesha wazi kufurahia kile akisemacho sasa sijui mnafanya hivyo kwa maslahi ya nani ?

Mnazinanga sana Simba na Young Africans kwamba hazina hata viwanja huku zikiwa na zaidi ya miaka themanini (80) lakini mnasahau kama hata nyie ni vikwazo kwa klabu hizo kujikwamua kwa sababu mnawaunga sana mkono watu wanaopingana na mipango yote ya uwekezaji kwenye klabu hizo. Badilikeni.

Lengo la wanachama wengi wa Simba na Yanga ni kuona klabu zao zinapata wawekezaji ili kuvifanya ziweze kujiendesha ndo mana wao wako tayari kuwaachia wawekezaji hao hata 90 % au zaidi kwa kuwa wao furaha yao ni kuona timu zao zinafanya vizuri. Aprili 29, mwaka huu Uwanja wa Taifa ulifurika watu bila shaka mapato ni makubwa lakini hakuna mwanachama au shabiki yeyote mwenye muda wa kutaka kufahamu mapato ni kiasi gani badala yake wale wanachama /wapenzi wa klabu hizo wako busy kuzodoana kuhusu kilichotokea ndani ya uwanja tu.

Hii inamaanisha wao hawana shida na hizo asilimia, wao shida yao ni klabu zao zifanye vizuri tu ndo mana hawana muda wa kujua mapato ni kiasi gani

Kuwawekea vikwazo wawekezaji ni kuwanyima haki wanachama ambao wanatajwa kama wamiliki wa klabu hizo....Mohammed Dewji akitaka 51 apewe na Yusuf Manji akitaka kukodi akodishwe tu Njaa HAIZOELEKI.

Kama Yanga isingekuwa na njaa naamini isingefungwa mabao 4-0 kwenye mchezo wake wa kwanza wa hatua ya makundi ya Kombe la Shirikisho.

Ndio, Yanga imeshafuza mara kadhaa katika miaka ya hivi karibuni lakini haikuwahi kupata kipigo kama hicho ni kwa sababu Manji alikuwapo na timu ilikuwa na pesa.