Hii ya De Gea ni aibu ya waziwazi kwa Man United

Muktasari:

  • Kikosi hicho kimedhihirisha kwanini Man City ni mabingwa, kwenye kikosi hicho kuna wachezaji wao watano.

LIGI Kuu England imetangaza majina ya wachezaji wanaounda Kikosi cha Kwanza cha msimu huu. Umekiona?

Kikosi hicho kimedhihirisha kwanini Man City ni mabingwa, kwenye kikosi hicho kuna wachezaji wao watano.

Nicholas Otamendi, Kyle Walker, David Silva, Kevin De Bruyne na Sergio Aguero, akitajwa kwa mara yake ya kwanza baada ya miaka saba.

Hiyo siyo ishu. Tottenham Hotspur, inayoshika nafasi ya nne kwenye msimamo, imeingiza wachezaji wawili.

Jan Vertonghen na Harry Kane. Siyo ishu pia.

Liverpool kwa upande wao, ingeshangaza sana kama Mohamed Salah angekosekana kwenye timu hiyo. Lakini, hakukuwa na nafasi kwa Roberto Firmino.

Nayo siyo ishu. Ishu ni hii hapa. Man United, ambao wanashika nafasi ya pili kwenye msimamo wa ligi wanaoamini kwamba wao ndio bora kwa wengine wote waliobaki ukiwaondoa Man City, wameingiza mchezaji mmoja tu.

Tena huyo mchezaji ni kipa, David De Gea. Hiki si kitu kizuri kabisa. Jambo hilo linamuumbua Jose Mourinho.

Kwamba pamoja na uwekezaji mkubwa aliofanya kwenye kikosi hicho katika madirisha makubwa mawili ya usajili na dogo moja, mchezaji bora aliyeonekana kwenye kikosi chake ni De Gea, aliyemrithi kutoka kwa Sir Alex Ferguson.

Vipi kuhusu wachezaji wengine kwenye kikosi hicho? Kama siyo aibu ni kitu gani? Cheki kwanza, Spurs ipo namba sita ina wachezaji wawili kwenye kikosi hicho,

Man United wanaoshika namba mbili, hawana hata mchezaji mmoja wa ndani ya uwanja. Mourinho anapaswa kujitazama.

Ina maana ameshindwa kuwatumia vizuri wachezaji wake aliokuwa nao kwenye kikosi. Ameshindwa kuwafanya wachezaji hao wacheze kwa kujinafasi ndani ya uwanja.

Shida kubwa iliyomkabili Mourinho na kushindwa kuvuna matokeo mazuri, wachezaji kucheza kwa kiwango bora ni ile staili yake ya kutaka kupaki basi.

Kuna mechi ambazo alistahili kumwaachia kiungo anayenyumbulika Ander Herrera acheze mpira wake.

Lakini, alimpiga kufuli mchezaji huyo na kumtaka acheze kwenye eneo la juu, asivuke mstari wa katikati.

Kwa staili hiyo ya kiuchezaji, huwezi kumtarajia mchezaji huyo kumwona kwenye kikosi bora cha msimu.

Kukaba sio kazi ya Herrera. Una mchezaji kama Paul Pogba lakini hayupo kwenye kikosi. Unaye Alexis Sanchez hayupo. Hata Juan Mata hayupo.

Wakali wote hao wangekuwa chini ya kocha Pep Guardiola, usingeshangaa kuwaona kwenye kikosi hicho.

Kwa sababu kitu ambacho angekifanya ni kuwaacha wachezaji wanavyoweza na kisha angewaongezea jambo moja tu, namna ya kutumia vipaji vyao kwa wakati mwafaka.

Hivi, Raheem Sterling ni bora kiasi gani?

Kweli ukiambiwa uchague yeye na Juan Mata utamchagua nani? Hii leo, Sterling angekuwa chini ya Mourinho, nadhani angekuwa anasugua benchi tu kama kinachomtokea Anthony Martial kwa sasa.

Pengine, De Gea amefanikiwa kuingia kwenye kikosi hicho kwa sababu si mmoja kati ya wale wanaopokea maelekezo ya kucheza moja kwa moja kutoka kwa Mourinho kama ilivyo kwa wachezaji wa ndani.

Huo ndio ukweli. Hii ni aibu kubwa kwa Man United, kuzidiwa hadi na timu inayoshika nafasi ya nne kwenye msimamo kwa kutoa wachezaji wengi kwenye kikosi hicho.

Man United hawana tofauti na Chelsea, tena kikosi hicho cha Antonio Conte ni afadhali kwa sababu chenyewe kimetoa mchezaji wa ndani, Marcos Alonso.

Kwa De Gea, hakuna ubishi hata kama kitatakiwa kuchaguliwa kikosi cha Ulaya, hawezi kukosa nafasi. Kiwango chake kipo mbali sana, amewazidi wengi kuanzia kwenye Ligi Kuu England na ligi nyingine za Ulaya. Ni yeye tu anayetamba tangu Manuel Neuer alipoumia.

Lakini, yote kwa yote ni aibu kwa Mourinho na Man United yake. Amewanyima mastaa wake fursa ya kucheza mpira.