Zari: Watu wanapiga kelele tu, hawanijui vizuri

Muktasari:

  • Akiongea na Mwanaspoti jijini Johanesburg hivi karibuni, Zari amedai kwamba licha ya kuishi Tanzania kwa zaidi ya miaka minne lakini Watanzania wengi wanamfahamu zaidi Zari wa Mitandaoni kuliko Zari mjasilimali na amewaahidi kuwaonyesha Zari halisi ni nani.

MPENZI wa zamani wa staa wa muziki wa kizazi kipya, Diamond Platinumz, Zarina Hassan, maarufu kama Zari ‘The Bosslady’ amedai kwamba anasikitishwa na jinsi ambavyo mamilioni ya Watanzania hawamjui yeye kiundani na badala yake wanamzungumzia mtu ambaye ni tofauti na alivyo.

Akiongea na Mwanaspoti jijini Johanesburg hivi karibuni, Zari amedai kwamba licha ya kuishi Tanzania kwa zaidi ya miaka minne lakini Watanzania wengi wanamfahamu zaidi Zari wa Mitandaoni kuliko Zari mjasilimali na amewaahidi kuwaonyesha Zari halisi ni nani.

“Hiki ndicho kinanisikitisha sana. Kila siku kuna umbea mwingi mitandaoni kuhusu mimi. Umbea mwingi unahusu maisha yangu ya mahusiano na Nassib (Diamond) lakini watu hawawezi kuyajua maisha halisi ya Zari,” anasema Zari.

“Mimi ni mwanamke mpambanaji. Nina maisha yangu ambayo hayapo mitandaoni na sihitaji kuyaweka mitandaoni kwa sababu sishindani na mtu mwingine yeyote. Nina biashara zangu nyingi binafsi, nina biashara za baba watoto wangu wa awali, Ivan, nina kipindi natarajia kuanzisha. Nina biashara nataka kufungua. Mambo ni mengi lakini kila siku nahusishwa na maisha ambayo sio yangu.”

Wiki ijayo mwanaspoti itakuletea Makala ya mahojiano baina yake na Zari ambapo anajipambanua yeye ni nani hasa tofauti na ambavyo watu wengi wamekuwa wakimchukulia.