Young Killer, Young D, Mr.Blue na Roma Mkatoliki kuwarusha roho UMISSETA

Saturday June 9 2018

 

By Saddam Sadick

Mwanza.Wasanii Bongo Fleva, Young Killer,Young D, Mr.Blue na Roma Mkatoliki wanatarajia kutoa burudani katika michuano ya Umoja wa Michezo kwa Shule za Sekondari nchini (UMISSETA) inayoendelea kwenye viwanja vya Shule ya Sekondari Nsumba na Chuo cha Ualimu Butimba jijini Mwanza.
Michezo hiyo ambayo ilianza kurindima tangu Juni 4, imezinduliwa rasmi leo na Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa katika viwanja vya Kirumba.
Ratiba iliyotonywa MCL ni kuwa Juni 12, vijana hao waoimba kwa miondoko ya kufokafoka Young Killer na Young D watakinukisha, huku siku inayofuata Mr.Blue atapanda jukwaani kuwaburudisha Wanafunzi hao.
Kama haitoshi, Rapa mkali, Roma Mkatoliki ndiye atafunga kazi Juni 14, kuhakikisha wadau wa michezo waliojaa katika viwanja vya Butimba wanashuhudia burudani hiyo.
Mapema leo wakati wa uzinduzi wa michezo hiyo, Dogo Janja ambaye pia ni msanii wa Bongo Fleva alifanya kazi nzuri ya kuimba na kuwapagawisha watu mbalimbali waliokuwa kwenye Uwanja wa CCM Kirumba.