Wema sepetu afichua ishu ya kukatwa utumbo

Friday July 13 2018

 

By Rhobi Chacha

ACHANA na timu ya Taifa ya England a.k.a Three Lions kuchapwa na Croatia kule Russia na kukatisha ndoto za kupeleka ndoo ya Dunia pale London, ishu inayotrendi kwa sasa ni shepu ya Malkia wa Bongo Movie, Wema Sepetu.

Kila mtu anasema lake kuhusiana na shepu mpya ya Wema, ambapo kwa sasa anaonekana amepungua kwa kasi. Kwa sasa Wema sio bonge tena kama alivyokuwa zamani.

Ile shepu ya Wema ambayo alibeba nayo taji la Miss Tanzania mwaka 2006 ndio imeanza kurudi unaambiwa, japo haiwezi kuwa kama vile, lakini kidogoooo ameanza kuonekana.

Huko kwenye mitandao ya kijamii ambako Wema ana wafuasi wengi kwelikweli kama jeshi la siafu, ndio usiseme mambo ni moto na kambi kibao zinapambana kutemeana shombo. Wapo wanaosema Wema amefanyiwa upasuaji wa utumbo ikiwa ni mkakati wake wa kujipunguza huku wengine wakipinga, lakini Mwanaspoti ambalo huwa halishindwi kitu kabisa, likaingia mtaani kumsaka na kupiga naye stori mbili tatu.

Ishu ya kukatwa utumbo

Mei 29, mwaka huu, katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, Wema alishindwa kufika mahakamani hapo kuendelea na kesi inayomkabili huku ikielezwa kuwa yuko nje kwa matibabu.

Baadaye zikaibuka taarifa kuwa, Wema alikwenda nchini India na kufanyiwa upasuaji na utumbo wake umekatwa ili kupunguza unene. Pia, wengine wakadai kwamba, amefanyiwa upasuaji ili kumwezesha kupata mtoto.

Lakini, mwenyewe amefunguka mbele ya Mwanaspoti, kwanza amekiri alikwenda nje kwa matibabu lakini hajakatwa utumbo kama inavyodaiwa. Amesema alikwenda kwa ajili ya matibabu mengine tofauti ambayo hata hivyo hakupenda kutaja.

“Unajua nawaangalia tu wataalamu wa kuwasemea watu matatizo binafsi, sikwenda India kwa ajili ya kukatwa utumbo ili nipunguze unene. Kwanini nifikie hatua hiyo, sina ustaa huo kabisa. Nilikwenda kwa matibabu yangu binafsi,” alisema Wema.

Bifu ya Zari na Diamond

Achana kabisa na ishu ya Diamond kuzaa na Hamisa Mobetto, moto unaonekana uliwaka zaidi na kumfanya staa huyo wa Bongo Flava kutwangwa talaka baada ya kusambaa kwa picha za Wema akiwa kwenye mikao ya kimahaba na Diamond.

Ilikuwa kwenye shoo ya kumtambulisha staa mpya wa WCB, Maromboso ambayo Diamond na vijana wale waliangusha shoo moja matata sana na Wema a.k.a Madame alikuwepo ndani ya nyumba pale Hyatt. Picha hizo ziliibua gumzo kwenye mitandao kutokana na namna wawili hao walivyokuwa wakikumbatiana na kupiga stori.

Akizungumza kwenye kipindi cha Dira ya Dunia ya BBC Swahili, Zari alifunguka mazito kuhusiana na talaka yake kwa Diamond: “Tulikuwa tunajaribu kuona namna gani ya kuendelea mbele baada ya hiyo skendo ya kupata mtoto. Lakini, baadaye vinatokea vitu kama hivyo leo unasikia hivi unaona sijui kakumbatiana huko na ma ex kwenye public. Vitu vya kunidhalilisha na watoto wanaona, sio sawa kabisa.”

Hata hivyo, Wema amesema kuwa hausiki na lolote kuhusiana na kupigana chini kwa Diamond na Zari.

“Jamani hili swali nalijibu sana halafu pia sipendi kuulizwa, narudia tena sihusiki na kuachana kwa Nassibu na Zari.

Hizo picha sijui video, niliziona za kawaida sababu sina chuki na Diamond na ndio maana nakuwa naye karibu katika mambo mengi tu au Zari alitaka kuwepo na bifu kati yetu na Diamond?,” alihoji Wema.

Hakuna kama Kanumba unaambiwa

Wema mwenyewe anakiri kuwa, katika ruka ruka yake na wanaume kuna mahali alifika na kutuliza akili kabisa kwani, huyu mwanaume hakuwa na masihara eti. Ndio, Wema anasema kuwa msanii wa Bongo Movie ambaye aliitangaza tasnia hiyo kimataifa, Steven Kanumba ndiye alikuwa mpenzi wake wa ukweli na walipendana sana. “Kanumba (marehemu) alikuwa na penzi la dhati na mwenye nia ya kweli katika kufanya maisha, sio hawa wa sasa wengi wamejawa na sanaa nyingi katika mapenzi,” alisema.